Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Raheem Shaquille Sterling
amezungumza kwa mara ya kwanza tangu alipokataa kusaini mkataba mpya wa
kuendelea kuitumikia klabu hiyo siku kadhaa zilizopita.
Sterling amezungumza jambo hilo baada ya masuala mengi kuibuka ambapo
baadhi ya wadau wa soka nchini England walidiridi kumpachika jina la
mwenye tamaa kutokana na mkataba alioukataa kuwa na ofa ya paund laki
moja kama mshahara wake kwa juma.
Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha England ambacho
kilicheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya barani Ulaya
mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Lithuania na kufanikiwa kufunga
bao lake la kwanza miongoni mwa mabao manne, amesema anashangazwa na
tuhuma zinamuandama, ili hali ana haki ya kufanya maamuzi.
Amesema soka ndio maisha yake na linapokuja suala la mkataba hana
budi kufikiria kwa kina kabla hajafanya maamuzi ya kuusaini, hivyo
amesisitiza suala la kuheshimiwa katika hilo.
Sterling mwenye umri wa miaka 20, amerejesha salamu kwa wanaomponda
wanaomsema vibaya kwa kuwaambia hana tabia ya tamaa na msimamo aliouweka
haumaanishi kama anahitaji kikubwa zaidi kwenye mshahara wake wa juma
kama wadau wengi wanavyodhani.
Amesema lengo lake ni kutaka kucheza soka na mwishowe kutwaa mataji
kama ilivyokua kwa wachezaji waliopita katika mchezo huo ambao unapendwa
ulimwenguni kote, hivyo jambo la pesa si chochote katika maisha yake.
APRIL 02 ------ STERLING 01
Raheem Sterling, akaongeza jambo katika mazungumzo yake wakati
akihojiwa na shirika la utangazaji la Uingereza BBC, kwa kusema wapo
wanaomshauri mema katika maisha yake kama mama yake mzazi pamoja na
wakala wake na siku zote amekua anaamini anayoambia katika mlengwa wa
kulia yana mantiki maisha mwake.
Amesema wapo wengine ambao huenda wakachukizwa na ushauri ama maamuzi
anyoyafanya lakini ukweli ni kwamba yeye ataendelea kuwa binaadamu
ambaye anafanya, anachokitaka kwa maslahi ya soka lake na pale alipo kwa
sasa.
Mkataba wa sasa wa Raheem Sterling unampa fursa ya kulipwa mshahara
wa paund 35,000, kwa juma na upo mbioni kufikia kikomo hali ambayo
inawapa kisulisuli viongozi wa klabu ya Liverpool.
Siku mbili zilizopita taarifa zilizochapishwa katika vyombo vya
habari zilieleza kwamba uongozi wa Liverpool unatarajia kumsainisha
mkataba tofauti na ule wa mshaha wa laki moja kwa juma, na
kinachosemekana huenda mshahara wake ukafikia paund laki moja na
themanini.