Benchi La FC Bayern Munich Halikaliki, Kisa Alaba

Author
Mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich wapo katika hasara kubwa ya kuingia majaribuni kufuatia majeraha yanayomsibu beki wa pembeni kutoka nchini Austria, David Olatokunbo Alaba.
Alaba, ambaye yupo kwenye kiwango cha juu msimu huu, amewatia mshawasha viongozi wa benchi la ufundi la klabu hiyo, baada ya kuumia goti la mguu wake wa kushoto, wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya barani Ulaya ambapo Austria walikua na kibarua cha kuwakabili Bosnia and Herzegovina.
Alaba, alipata dhoruba la majeraha ya goti baada ya kuchezewa ndivyo sivyo na beki wa Bosnia and Herzegovina Ermin Bicakcic.
Kutokana na mkasa huo, huenda beki huyo mwenye umri wa miaka 22 akakaa nje ya uwanja kwa kipindi chote cha msimu huu kilichobaki, kutokana na vipimo kuonyesha anahitaji mapumziko ambayo yatakwenda sambamba na matibabu.
Taarifa za awali kutoka ndani ya FC Bayern Munich, zimeeleza kwamba Alaba atapumzika kwa kipindi cha majuma mawili ili kuangalia hali yake itakavyo endelea, na kama itakua tofauti na hapo atabaki chini ya uangalizi wa madaktari kwa zaidi ya majuma saba yajayo.
Kuumia kwa Alaba, kunaaminisha ataukosa mchezo wa hatua ya robo fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya FC Porto utakaochezwa April 15, na subra ya matibabu yake huenda ikaendelea kumuweka nje zaidi na kuukosa mchezo wa mkondo wa pili baina ya klabu hizo ambao utachezwa April 21.
Mbaya zaidi kama mambo yataenda mrama na klabu yake ikifanikiwa kutinga hatua ya fainali, Alaba ataukosa mchezo huo ambao kwa mwaka huu umepangwa kupigwa mjini Berlin nchini Ujerumani, June 6.
Benchi La FC Bayern Munich Halikaliki, Kisa Alaba

0 comments:

Post a Comment