YANGA YAJIPANGA ZIMBABWE

Author


 
Iko hivi; Yanga ilimtanguliza mjumbe wake wa kamati ya mashindano, Samuel Lukumay Jumanne iliyopita ambapo alipotua tu kwenye Uwanja wa Ndege wa Bulawayo akagundua kitu.

KATIKA kuthibitisha kwamba imepania kufika kwenye levo nyingine tofauti msimu huu kwenye michuano ya kimataifa, Yanga imeshusha mashushushu wake Zimbabwe ambao wamebaini mitego ya hatari waliyokuwa wamewekewa na wapinzani wao ambao ni FC Platinum.
Iko hivi; Yanga ilimtanguliza mjumbe wake wa kamati ya mashindano, Samuel Lukumay Jumanne iliyopita ambapo alipotua tu kwenye Uwanja wa Ndege wa Bulawayo akagundua kitu.
Wale jamaa wameweka mtego kwamba Mtanzania yeyote atakayetua uwanjani hapo wapate taarifa, unajua alichowazuga ni kuwa yeye ni mfanyabiashara Mtanzania anaishi Afrika Kusini hakai Zimbabwe anapita tu.
Akawachota akili wakajisahau akaingia mjini akaanza kufanya yake akakutana na Watanzania wanaoishi Bulawayo wakampa maelezo muhimu na jinsi watakavyoisaidia Yanga kuanzia kwenye misosi na kila kitu. Lakini kila akizunguka mitaani pamoja na Wabongo wengine hawazungumzi Kiswahili ili wasishtukiwe. Kwahiyo kinachofanyika ni kwamba Yanga ikitua leo itafikia Bulawayo halafu kesho asubuhi itakwenda Zvishavane kwa basi asubuhi ambapo itafikia kwa kushtukiza kwenye hoteli yoyote ili kupumzika kidogo na kupata msosi halafu wakiamka wanapilitiza hadi uwanjani.
Yanga wameafikiana kwamba mbinu hiyo ndiyo pekee inayoweza kuwanusuru na wamepanga kupiga chini hoteli zote walizoandaliwa na wenyewe wao karibu na eneo la uwanja.
Yanga wamegoma kufikia moja kwa moja katika mji huo ambapo sasa kikosi hicho kitaweka kambi ya saa kadhaa jijini Bulawayo kabla ya kwenda Zvishavane ambako kuna umbali utofauti wa kilometa 170 na watakaa kwenye basi saa mbili kabla ya kufika katika uwanja wa Mandava unaochukua jumla ya mashabiki 10,000.
Katibu Mkuu wa Yanga Jonas Tibohora alikiri kupatiwa taarifa hizo ambapo pia alisema wamepata taarifa kuhusu Platinum kuwa wapo katika mazoezi makali wakitaka kulipiza kisasi na tayari makocha wana taarifa zote.
“Unajua wale kule ligi yao ndiyo imeanza sasa hawataki kuweka nguvu nyingi katika ligi ambayo itachukua muda mrefu, wameona nguvu kubwa waiweke katika mchezo wetu kwa kuwa ushindi wa mabao 5-1 tulioupata hapa umewaweka katika wakati mgumu viongozi wao na hata makocha,”alisema Tiboroha.
“Kuna kiongozi wao alinipigia simu wakitaka kujua tunakwenda lini ili watuwekee hoteli nikawaambia watulie kwa kuwa bado tunajipanga, tunataka kuwa makini katika mchezo huu kuepusha kutolewa kwa makosa ambayo tungeweza kuyakwepa, tumejiandaa vyema kiuchumi kukabiliana na wenzetu hawa.” alisema.

0 comments:

Post a Comment