WAKALI WA SHETANI -17

Author

#Wakala_wa_Shetani - 17-

Katika kijiji cha Nyasha ilikuwa siku ambayo iliwachanganya watu wengi baada ya kila nyumba kulalamikia tatizo la tumbo. Hospitali zilijaa wagonjwa ambapo wengi walipoteza maisha. Ilibidi taarifa zifike haraka mkoani na kutumwa timu ya wataalamu kuja kufanya uchunguzi.

Ilionesha watu wa kijiji kile wamekunywa sumu iliyokuwa kwenye maji, mifugo yote ilikufa na kufanya kijiji kiwe katika janga zito la maafa ya watu na mifugo. Ilibidi wagonjwa wote wahamishiwe mjini lakini wengi walifia njiani.

*Sasa Endelea*

KaYA nyingine zilipoteza familia nzima na nyingine zilipoteza zaidi ya watu watatu.
Mara moja watu wa Kijiji cha Nyasha walipigwa marufuku kunywa maji yote, uchunguzi ukaanza kufanywa ambapo ilibainika kuwa vyanzo vyote vya maji vilikuwa na sumu.
Ilibidi iletwe dawa na kuondoa sumu katika sehemu zote zenye vyanzo vya maji lakini wakati huo Kijiji cha Nyasha kilikuwa na msiba mzito wa kupoteza nusu ya wanakijiji.
Taarifa za msiba mzito uliowakuta wanakijiji wa Nyasha zilimfikia Ngw’ana Bupilipili ambaye alijawa na furaha kuamini mpango wake umefanikiwa. Pamoja na kufanikiwa kuua watu wengi, bado dhamira yake ilikuwa haijatimia. Alipanga kukifanya kijiji kile kiwe cha historia kwa kuwamaliza wanakijiji wote na kubakiza magofu.

***
Baada ya kufanikisha zoezi la awali la kukiteketeza Kijiji cha Nyasha, Ngw’ana Bupilipili aliendelea na mchezo wake ule, kila hali ilipotulia alikwenda kuweka sumu kwenye maji. Hali ile ilikiweka Kijiji cha Nyasha kwenye mashaka na kuamua kufanya uchunguzi wa kina juu ya nani anayefanya mchezo huo.
Makachero toka serikalini walianza uchunguzi wa siri bila mtu yeyote kujua. Walilinda kwa saa 24 vyanzo vyote vya maji kwa kubadilishana kufuatilia mtu aliyekuwa akisababisha mauaji ya wanakijiji cha Nyasha.
Ngw’ana Bupilipili kama kawaida yake baada ya mambo kutulia alirudi tena kwenye Kijiji cha Nyasha kuendeleza hukumu yake ya kuhakikisha anakisafisha kijiji chote.
Kurudi kijiji pale ilikuwa mara ya nne, kama kawaida alimuaga shoga yake na kumuachia mwanaye Kusekwa aliyekuwa ametimiza miaka miwili.
Alitembea katika mbuga kama ilivyo kawaida yake, kwa vile alikuwa ameshakuwa mzoefu, hakuwa na hofu tena ya kutembea mbugani peke yake. Kutokana na uzoefu alikuwa akitoka usiku zaidi ili alfajiri imkute ameshamaliza kazi yake.
Baada ya mwendo wa saa tatu bila kupumzika, aliingia Kijiji cha Nyasha kukiwa bado na giza, hakukuwa na mtu yeyote. Alijisifu kuondoka mapema kwa kuamini atamaliza kazi zake bila mtu yeyote kumuona.
Baada ya kuangalia usalama wa eneo lile na kuona hakuna tatizo, aliifungua ile sumu na kuitia kwenye chanzo cha maji kisha aliifunga na kuelekea kwenye kisima cha akina mama. Wakati akifanya vile walinzi wa eneo lile walikuwa bado hawajamuona.
Wakati anataka kuondoka eneo lile askari mmoja alishangaa kumuona mwanamke akitokea kwenye chanzo cha maji.
“Hey, wee mama unafanya nini alfajiri hii?”
“Nakwenda shamba,” Ngw’ana Bupilipili japo alikuwa katika mshtuko mkubwa lakini alijitahidi kujibu kwa kujiamini.
“Shamba, mbona majibu yako yana utata, unakwenda shamba gani ikiwa mashamba hayapo eneo hili?”
“Achana naye bwana, si unajua tumemaliza lindo salama,” alisema mlinzi mwingine.
“Haya potea hapa.”
Ngw’na Bupilipili alimshukuru Mungu kumuepusha na watu wale, ndipo alipofumbuka macho kuwa sehemu ile ina ulinzi. Aliteremka kuelekea bondeni kwa kuhofia kugeuza lazima wangemtilia wasiwasi.
Aliamua kutafuta njia nyingine ya kumuokoa kwa kuondoka eneo lile ambalo aliamini limezungukwa na ulinzi mzito. Alitembea kwa tahadhari akipita pembeni kutafuta njia ya kutokea nje ya Kijiji cha Nyasha.
Askari mmoja alimuona Ngw’ana Bupilipili akitembea kwa mashaka na kuamua kumfuatilia taratibu. Baada ya mwendo mfupi alikutana na sehemu kubwa iliyokuwa imetengeneza kama bwawa.
Alipoiangalia sehemu ile ilimuonesha kabisa watu huchota maji. Akili yake ilimtuma sehemu ile vilevile inatakiwa kuwekwa sumu. Kwa tahadhari kubwa alitoa paketi ya dawa ya kuulia wadudu na kuanza kuinyunyizia kwenye maji yake.
Askari aliyekuwa akimfuatilia alimshangaa na kujiuliza yule mwanamke ananyunyiza nini kwenye yale maji.
Hakutaka kumshtua alimsogelea taratibu mpaka alipokuwa na kusimama nyuma yake bila Ngw’ana Bupilipili kumuona. Baada ya kuimiminia ile dawa iliyobaki aliirudisha kwenye paketi yake kisha aliifunga kwenye mfuko wa plastiki na kuiweka katika mfuko wa kaptura aliyokuwa amevaa.
Wakati anavua gloves ndipo yule askari alipomshtua.
“Unafanya nini?”
Ngw’ana Bupilipili alishtuka na kuanza kutimua mbio, lakini hakufika mbali alikamatwa.

*Itaendelea*

0 comments:

Post a Comment