WAKALA WA SHETANI -16

Author

#Wakala_wa_Shetani -16-.....

“Mungu wangu, kama ni sumu inafanya nini humu ndani?”
“Si sumu kwa maana imetengenezwa kuua watu, ni dawa ya kuuwa wadudu katika mitaro na mashimo ya maji hata wadudu warukao na watambaao.”
“Sasa inakuwaje unasema ni sumu kumbe ni dawa ya kuulia wadudu?”
“Mama Kusekwa, hii ni dawa lakini ukiitia mdomoni inageuka sumu na kukudhuru.”
SASA ENDELEA...

“Mmh, sawa.”
“Tena dawa hii kama utakumbuka kuna mwaka mtu mmoja aliiweka kwenye tanki la maji na kuua familia nzima.”
“Mmh! Sasa inakuwaje mtu aweke kwenye tanki la maji wafe watu wengi, kwani ina nguvu gani isiyopungua katika maji mengi?”
“Hii ni sumu kali sana ndio maana nikashangaa kukuona umeishika kwa mkono. Unatakiwa kunawa vizuri na sabuni mikono yote na kuhakikisha unakuwa msafi kabla ya kumshika mtoto wako.”
“Nashukuru Sister Lucy. Basi ningetoka hapa ningepewa embe mimi ningekula tu bila kujua kama nina sumu mkononi.”
“Basi kuanzia leo unatakiwa kuvaa gloves kabla ya kupanga vitu vya humu ndani.”
“Nitafanya hivyo, hivi kama ukiitia dawa hii kwenye lambo la kijijini si unaweza kuua watu wengi?”
“Tena usiombe kufanya kitu kama hicho, na dawa hizi hupatikana sehemu kama hizi madukani hazipo kwani ni kali sana, zinaua mara moja.”
Baada ya maelezo yale Ng’wana Bupilipili alikwenda kunawa kwa sabuni na kisha aliendelea na kazi yake.

***
Jioni ya siku ile akiwa amejilaza kitandani kwake, wakati huo mwanaye akiwa anaendelea kufaidi ziwa tamu la mama yake, alijikuta akikumbuka maneno aliyokuwa akizungumza na Sister Lucy kuhusu ukali wa ile dawa ya kuulia wadudu kuwa ni sumu kali kama mwanadamu atainywa.
Aliamini kupitia sumu ile itakuwa njia nyepesi ya kulipa kisasi, alijua akienda kuiweka katika chanzo cha maji ambayo hutumiwa na wana kijiji lazima ataua watu wengi.
Alijikuta akiwachukia watu wote wa kijiji cha Nyasha kwa kuamini kila aliyetoka katika dawa ya wauaji nao walitakiwa kuipata hukumu ile kwa kuamini kama wao walifurahia vifo vya watoto wenye ulemavu wa ngozi basi nao watoto hao nao watafurahi kusikia mauti yao.
Alijikuta akiapa lazima alipe kisasi tena kikubwa na kuacha historia ya vifo vya watu wengi. Alipanga siku ya pili akiingia kufanya usafi achukue paketi nne za sumu ambazo zote ataziweka katika vyanzo vya maji ya Kijiji cha Nyasha.

***
Siku ya pili akiwa anafanya usafi stoo alichukua paketi nne za dawa ya kuulia wadudu na kuificha kwenye kanga. Baada ya usafi alitoka nayo na kwenda kuificha chumbani kwake.
Baada ya kuipata ile dawa alipanga siku moja ataondoka kwenye kambi ile saa kumi za usiku kwenda Kijiji cha Nyasha.
Baada ya kujipanga na kuipanga siku ya kwenda kulipa kisasi, alimtaarifu shoga yake wa karibu kuhusu safari yake lakini alimdanganya kuwa anafuata vitu vyake.
Baada ya kukubaliana siku ya pili majira ya saa kumi za usiku Ng’wana Bupilipili aliamka na kwenda kumuamsha shoga yake ambaye alikuwa amelala.
“Vipi, safari imeiva?”
“Eeh, shoga, niangalizie mwanangu,” alimpa mtoto wake aliyekuwa bado na usingizi.
Shoga yake alimchukua na kumuingiza ndani na kumlaza kitandani kisha alitoka ili amuage.
“Basi shoga safari njema.”
“Nashukuru shoga, Mungu akijalia tutaonana.”
Ng’wana Bupilipili kabla ya kuondoka aliingia chumbani kwa shoga yake na kumnyanyua mtoto wake kitandani na kumkumbatia kwa uchungu huku machozi yakimtoka. Hali ile ilimshtua shoga yake na kuhoji kulikoni.
“Vipi mbona unalia?”
“Basi acha tu, nimekumbuka vitu vingi hasa baada ya kukumbuka kifo cha mume wangu na leo narudi hukohuko.”
“Kama ni hivyo kwa nini unakwenda tena?”
“Hapana kuna vitu vyangu vingi na vya muhimu sana lazima niende.”
“Sasa utaingiaje pale kijijini?”
“Hapana siendi nyumbani nitaishia shambani kwetu.”
“Unajuaje kama shamba bado lipo mikononi kwenu?”
“Yote nitayajua huko huko.”
“Basi bwana akutangulie safari yako yote.”
“Amen.”
Alimrudisha mtoto kitandani baada ya kumbusu, alimgeukia shoga yake na kumkumbatia kabla ya kugeuka na kuondoka kuwahi safari yake ambayo aliamini mpaka saa mbili asubuhi atakuwa Kijiji cha Nyasha.
Hakutokea mlango wa mbele, aliruka ukuta kuogopa kuulizwa na mlinzi anakwenda wapi. Baada ya kufanikiwa kutoka salama nje ya kambi alianza safari kuelekea Kijiji cha Nyasha moyoni akiwa na dhamira nzito ya kuwa tayari kupambana na lolote litakalotokea mbele yake.

#Itaendelea

0 comments:

Post a Comment