WAKALA WA SHETANI-18

Author

#Wakala_wa_Shetani -18-

Daktari Father Joe alipoingia ndani alimkuta Ng’wana Bupilipili akiwa amejilaza kitandani. Lakini aliamini kabisa mlalo ule si wa mtu kupoteza fahamu bali wa usingizi wa kawaida. Akiwa bado hajapata jibu juu ya kuwa katika hali ile alimgeukia msaidizi wake Sister Marry.
SASA ENDELEA...

“Eti sister nini kilichomtisha na kumfanya akimbie na kuanguka kisha kupoteza fahamu?”
“Kwa kweli mpaka sasa hatujajua ila niliambiwa alitoka mara moja.”
“Alikuwa amekwenda wapi?”
“Mmh, hapo sijui ngoja tutamuuliza mwenyewe akipata fahamu.”
Ng’wana Bupilipili alizifahamu vizuri sauti za Father Joe na Sister Marry hali iliyomfanya ashushe pumzi kwa kuamini yupo sehemu salama. Alijifanya kujigeuza kitu kilichowafanya wasogee kitandani. Sister Marry akamwita:
“Mama Kusekwa... Mama Kusekwa.”
“Abee,” aliitika na kujinyoosha.
“Vipi unajisikiaje?” Sister Marry alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Mmh, sijambo kiasi,” alijibu huku akifumbua macho.
“Eti tatizo nini?”
“Nilikuwa natoka kutafuta baadhi ya vitu vyangu nilivyoviacha porini wakati nakuja, ndipo nilipokutana na mnyama mkali aliyeanza kunifukuza, kwa kweli nilikimbia kwa nguvu zangu zote.
“Sikumbuki kilichoendelea na kujikuta nipo hapa,” Ng’wana Bupilipili alitengeneza uongo unaofanana na ukweli.
“Ooh, pole sana.”
“Asante.”
“Hakukujeruhi?” Father Joe aliuliza.
“Sidhani najiona nipo salama ni maumivu madogomadogo ambayo sijui ni ya nini.”
“Unaweza kwenda chumbani kwako, kama utasikia tatizo lolote mwilini mwako utatujulisha.”
Ng’wana Bupilipili alinyanyuka kitandani na kutembea kwa kuchechemea kwa muda kisha alitembea kawaida. Alikwenda hadi chumbani kwake na kujilaza bila kumfuata mtoto kwani hakuwa na mawazo ya mwanaye zaidi ya kujifikiria jinsi alivyookoka katika mikono ya askari waliokuwa wakilinda chanzo cha maji.
Wasiwasi wake mkubwa ulikuwa huenda wakafanya msako na kwa vile askari yule ameshaiona sura yake, lazima angemtafuta na kumpata. Aliamini katika msako wao lazima wangefika kwenye ile kambi na lazima angemtambua na kumkamata.
Ng’wana Bupilipili aliamini kabisa kwa upande wake muda ule kwake kuwepo pale kambini hakufai, kwa kuamini wakimkosa porini lazima watamtafuta kwenye kambi ile.
Wazo lake kubwa lilikuwa ikifika usiku atoroke na mwanaye na kutimkia sehemu asiyoijua japokuwa alijua ni hatari, lakini aliamini bora akafie mbele kuliko kukamatwa na kuhukumiwa kifo.
Hata shoga yake alipoingia hakumuona kwa vile alikuwa amezama kwenye dimbwi la mawazo.
“Shoga nakuona upo mbali vipi umeumia sana?”
“Walaa, kawaida tu.”
“Mh! Za huko?”
“Shoga mbona yamenikuta leo makubwa.”
“Yapi hayo?”
“Kidogo leo nishikwe na askari waliokuwa wakilinda vyanzo vya maji.”
“Vyanzo vya maji?”
“Eeh, japokuwa nilikuwa sijakueleza ukweli wa safari yangu, kwa vile wewe umekuwa mtu wangu wa karibu na muhimu sana lazima nikueleze ukweli hata nikishikwa ujue tatizo langu.”
“Ushikwe kwa kosa gani tena?” shoga yake alishtuka.
“Tulia basi nikueleze usiwe na pupa na nitakachokueleza naomba ibakie siri yako.”
“Hakuna tatizo shoga.”
Ng’wana Bupilipili alimueleza yote aliyoyafanya baada ya kufiwa na mume wake na ahadi ya kisasi aliyoiweka ya kukisambaratisha Kijiji cha Nyasha, siku ile jinsi alivyokamatwa na askari na kufanikiwa kumtoroka. Shoga yake Bupe hakuamini alichoelezwa na Ng’wana Bupilipili na ujasiri aliouonesha wa kutimiza dhamira yake.

#Itaendelea

0 comments:

Post a Comment