WAKALA WA SHETANO -28

Author

#Wakala_wa_Shetani -28-...

"Bwana eeeh tuchimbe dawa hapa."
"Sawa."
Kusekwa alitulia akijua jamaa wameteremka kwenda kujisaidia haja ndogo, wakati wanaingia kwenye gari ili waondoke, aliteremka haraka na kuliacha gari liende. Sehemu aliyoshuka ilikuwa ngeni kwake. Kulikuwa na vichaka ambavyo hakuwa na uhakika wa usalama wake.

Story hii inapostiwa chini ya #Udhamini wa #SOKON_2_YOUTH_GROUP #MAMBO_BAND NA #KM_MUSIC_REC

#SASA ENDELEA...

baada ya kutoka ndani ya kinywa cha mauti aliamini alikuwa salama, wakati akitafakari afanye nini mara kwa mbali aliona gari likija na kuwasha taa. Kwa woga alikimbia na kujificha nyuma ya kichaka ili wenye gari wasimuone. Gari lilipita bila wale watu kumuona na kumfanya abaki anajiuliza nini cha kufanya.
Baridi ya alfajiri ilikuwa kali lakini kwa Kusekwa haikuwa shida kwa vile furaha ya kubakia hai ilikuwa zaidi ya baridi ile. Kutokana na kiza cha alfajiri ile aliamua kujilaza pembeni ya kichaka ambacho hakujua usalama wake upo kiasi gani.
Pamoja na kutetemeka, alimuomba Mungu kupambazuke ili ajue yupo wapi na afanye nini. Pamoja na kuwaogopa wanadamu lakini aliamini wapo wenye roho nzuri kama Father Joe ambaye alionesha upendo wa hali ya juu. Aliwachukia binadamu kama Mr Brown ambao hujionesha wana roho nzuri usoni lakini moyoni wana roho mbaya zaidi ya nyoka.
Na pia aliamini kabisa Father Joe hajui chochote toka kwa rafiki yake mkubwa, Mr Brown kuwa anawachukua watoto wenye ulemavu wa ngozi na kwenda kuwakata viungo huku akidanganya kawapeleka Ulaya na kumbe Ulaya yenyewe ni kuzimu.
Kutokana na akili yake kufanya kazi na kujua haki ya mwanadamu inapatikana wapi, alipanga kama atapona katika kile kifo basi atakwenda kwenye vyombo vya sheria. Alikumbuka siku moja aliyoelezwa na Father Joe kuwa kila kitu kinaongozwa na sheria na chombo kinacholinda raia ni jeshi la polisi.
Alimuomba Mungu aweze kufika polisi kufichua uovu ule wa Mr Brown, kila alipojaribu kufumba macho, jinamizi la kutaka kukatwa viungo lilimjia na kumfanya akae macho mpaka kunapambazuka.
Kutokana na baridi kuwa kali, ilibidi Kusekwa ajiingize katikati ya kichaka ili kupunguza ukali wa baridi lile. Kwa bahati mbaya, sehemu aliyoingia kulikuwa na nyoka amelala ambaye alimkanyaga. Naye nyoka katika kujitetea alimgonga mguuni.
Kusekwa alishtuka na kupiga kelele za maumivu, wakati huo nyoka alikuwa akikimbia eneo lile kwa kutoa mlio wa kutambaa. Kusekwa alitoka kichakani mbio huku akishikilia mguu na kusogea barabarani.
Baada ya kwenda mwendo mfupi kuondoka eneo la tukio akiogopa kushambuliwa tena na nyoka, alianza kusikia kizunguzungu ambacho kiliongezwa na mwanga mkali wa gari uliompiga usoni na kumfanya aanguke chini, hakujua kilichoendelea.
#MIAKA_SABA_BAADAYE
Ng'wana Bupilipili alikuwa katika Kijiji cha Sangema kwenye kituo cha kuwatunza watu wenye maisha magumu, baada ya kupata hifadhi. Kituoni hapo hapakuwa tofauti na kituo alichokimbia. Shughuli zilikuwa zilezile za kazi za mikono. Kutokana na uzoefu alioupata, alijikuta akipewa kipaumbele na mkuu wa kituo, Mr Harrison kuwa kiongozi na mwalimu msaidizi.
Kutokana na kupewa uongozi alijikuta akipata posho ndogondogo tofauti na kituo cha awali ambacho malipo yake yalikuwa kula na kulala. Alijikuta akifurahia maisha kule, kila siku dua zake zote alizielekeza kwa mwanaye Kusekwa ili Mungu amtangulie na kumkinga na roho mbaya za watu na kumpa maisha marefu.
Aliendelea kuwa mwalimu mwanafunzi pale kituoni, akawa anajifunza asichokijua na kuwafundisha wenzake anachokijua. Kwa kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele ndivyo alivyokuwa akiongeza ujuzi wa kazi yake. Siku moja akiwa darasani, juu ya meza ya mwalimu wao kulikuwa na gazeti.
Ng'wana Bupilipili alilichukua lile gazeti na kuanza kulisoma, ndani yake alikutana na picha yake iliyokuwa robo ukurasa, ikiwa na maandishi makubwa; #ANATAFUTWA. Chini ya picha kulikuwa na maneno yaliyosomeka: Mtuhumiwa hapo juu anayetambulika kwa jina la Rozalia Bupilipili au maarufu kwa jina la Ng'wana Bupilipili anatafutwa na jeshi la polisi kwa mauaji ya wanakijiji cha Nyasha pamoja na askari wawili. Ni mwanamke hatari sana mwenye mafunzo ya kigaidi. Yeyote atakayemuona atoe taarifa kituo chochote cha polisi. Zawadi nono itatolewa.
Ng'wana Bupilipili alishtuka kuona picha yake kwenye gazeti huku akituhumiwa kufanya mauaji ya kutisha ya wanakijiji wa Nyasha pamoja na askari wawili. Aliamini usalama wake upo mashakani, kwani kwa yeyote atakayebahatika kuiona ndani ya kituo kile lazima atamuogopa na kisha kuripoti polisi na kusababisha akamatwe.
Kwa jinsi ilivyoonesha, gazeti lile lilikuwa la siku ile, hata mkuu wa kituo kile, Mr Harrison alikuwa bado hajaliperuzi. Alipata wazo la kulichana lakini wasiwasi wake ulikuwa mtu yeyote atakayebahatika kuliona gazeti hilo lazima angemtambua. Kwa ajili ya kuhofia maisha yake, alipata wazo la kutoroka eneo lile ili kujiokoa.
Alitoka darasani taratibu na kuelekea chumbani kwake, akachukua vitu muhimu tu na kuondoka eneo la kituo bila mtu yeyote kujua. Alijitanda khanga na kuuficha uso wake kwa sehemu kubwa kisha alikwenda hadi kituo cha basi ambako alipanda gari kuelekea asikokujua, akawa anatafuta sehemu za kijijini zaidi ambazo magazeti hayafiki.
Mr Harrison baada ya kumaliza shughuli zake ndogondogo, alirudi darasani kuulizia wamefikia wapi. Lakini alishangaa kutomkuta mwalimu, ilibidi amuulize kwa wenzake
"Mwalimu wenu yupo wapi?"
"Mmh! Alikuwa anasoma gazeti hapo kisha alitoka nje, huenda amekwenda msalani."
Mr Harison alichukua gazeti lake na kuanza kulisoma taratibu, alipofika kwenye ukurasa uliokuwa na picha ya Ng'wana Bupilipili alishtuka. Aliiangalia ile picha kwa muda kisha akasoma maelezo yake ambayo yalimshtua sana, habari hiyo ilionesha kuwa mwanamke huyo ni hatari sana.
Ili kutaka ukweli, alitoka na lile gazeti hadi kwa wenzake ambao aliwaonesha ile picha, kila mmoja alimtambua Ng'wana Bupilipili. Kwa vile walijua amekwenda msalani, walimsubiri ili wambane na kumuuliza kuhusu uhusiano na ile picha lakini ajabu muda ulizidi kukatika bila kuonekana.
Ilibidi ufanyike msako wa siri kutaka kubaini yupo wapi, lakini hakukuwa na taarifa zozote. Mr Harrison alikumbuka kauli za wanawake waliokuwa kwenye mafunzo kwamba baada ya kusoma lile gazeti alitoka darasani. Aliamini kabisa ni mwenyewe na ameamua kukimbia.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia...

0 comments:

Post a Comment