#Wakala_wa_Shetani -29-......
ILIPOISHIA:
Ilibidi ufanyike msako wa siri kutaka kubaini Malimi yupo wapi, lakini hakukuwa na taarifa zozote. Mr Harison alikumbuka kauli za wanawake walipokuwa kwenye mafunzo kwamba baada ya kusoma lile gazeti alitoka darasani. Aliamini kabisa ni mwenyewe ambaye baada ya kuiona picha yake ameamua kukimbia.
#SASA_ENDELEA...
Waliongeza msako kila kona lakini waliambulia patupu. Ng'wana Bupilipili alikuwa ameshapotea eneo lile. Taarifa zile alizirudisha kwa wenzake ambao walipigwa butwaa wasiamini tuhuma zile kuwa zake kutokana na tabia yake ya upole tena yenye huruma na mapenzi kwa watu wote.
Hakuwa mbaguzi, alikuwa akijitoa yeye kwa wenzake ili kutatua matatizo yao, hata kutoa sehemu ya posho yake kuwasaidia wenzake. Japokuwa picha ilifanana kwa asilimia mia, bado shoga zake walisema siyo yeye. Lakini kizungumkuti kikabakia kama siyo, yeye yupo wapi?
Lilibakia fumbo zito vichwani mwao, wasijue Malimi kipenzi chao amekwenda wapi.
***
Kusekwa aliposhtuka alijikuta amelala kwenye kitanda cha kamba, alipozungusha macho alijikuta yupo kwenye chumba cha nyumba ya udongo. Alijiuliza pale ni wapi na amefikaje. Alisikia sauti za watu wakizungumza nje ya chumba.
"Dogo lazima atakuwa ameamka."
"Ngoja nikamcheki."
Kusekwa aliangalia mlangoni na kumuona mtu mmoja akiingia, walipokutanisha macho alisema kwa sauti:
"Ameamka."
"Poa, njoo naye apate uji na viazi inaonekana hajala tangu jana," sauti kutoka nje ilisema.
"Hakuna tatizo, dogo amka," jamaa alisema na kumfanya Kusekwa anyanyuke kitandani.
Alitoka nje ya chumba na kukuta sebuleni kuna watu wengine wawili.
"Hujambo dogo?" walimsalimia.
"Sijambo, shikamooni."
"Marahaba."
Walimpatia uji na viazi vya kuchemsha, baada ya kula, walimuuliza sehemu waliyomuokota amefikaje na alikuwa anatoka wapi. Kusekwa aliwaeleza yote yaliyomkuta baada ya kuamini wale ni watu wema kutokana na walivyomuokoa na kumtunza kama mdogo wao.
Jamaa alishtuka na kumpa pole huku wakimhakikishia kuishi naye maisha mazuri pale na kumtafutia shule yenye usalama. Aliwashukuru kwa kumuokoa na kuwa tayari kumlea. Siku ilipita wakimlea kama mtoto wao kwa kumuonesha upendo wa hali ya juu.
Usiku ulipofika walikwenda kulala na Kusekwa alipewa chumba chake, majira ya usiku wa manane Kusekwa alishtuka usingizi baada ya kuvamiwa na kuzibwa mdomo. Ghafla alisikia maumivu makali mkono wake wa kushoto. Alitaka kupiga kelele lakini mdomo ulikuwa umezibwa.
Alihisi maumivu makali na kupoteza damu nyingi, aliteseka bila msaada wowote huku akijiuliza wenyeji wake wapo wapi mpaka watu wale wabaya wameingia na kumkata mkono. Baada ya kutoka damu nyingi alipoteza fahamu.
Aliposhtuka alijikuta yupo hospitali lakini hakuwa na mkono mmoja, aliangua kilio kitu kilichofanya wauguzi wafike na kumbembeleza. Baada ya kutulia alielezea yote tangu kuchukuliwa na Mr Brown na kukosa kukatwa viungo na siku aliyovamiwa na watu wabaya na kumkata mkono wake wa kushoto.
Kwa vile ilikuwa hospitali ya dini walimpa malezi mazuri ya kumfajiri, aliendelea kuuguza jeraha la mkono. Baada ya siku mbili zilipatikana taarifa kuna watu wamekamatwa na mkono wa albino. Kwa vile Kusekwa alikuwa amekatwa mkono siku chache. Alichukuliwa kwenda kuwatambua watu wale japokuwa aliamini kwa usiku alivyovamiwa asingeweza kuwajua.
Lakini alipofika polisi ilikuwa tofauti na alivyofikiria, watu waliomuokota na kumuahidi kumtunza ndiyo waliokamatwa na mkono wake. Roho ilimuuma na kuona hakuna kiumbe wa kuaminiwa diniani, kama waliomuokota ndiyo waliomtenda.
Alirudishwa hospitali na watu wale walifunguliwa mashitaka ya kukutwa na mkono wa mtu. Kusekwa naye aliendelea vizuri na jeraha lake ambalo kila siku lilionesha maendeleo vizuri. Baada ya kupata nafuu alihamishwa kutoka wodini na kupelekwa kwenye kituo kidogo cha kulelea watoto yatima ambao huchukuliwa na wafadhili mbalimbali.
Alikaa pale kwa mwezi mmoja akitunzwa na kupata mafunzo ya awali ambayo alianza kuyapata kwenye mgodi wa Mr Brown. Siku zote alijenga chuki kwa watu, kiumbe aliyemwamini alikuwa mwanamke peke yake. Lakini wanaume wote aliwaogopa kwa kuwaona wana sura za furaha lakini mioyo yao ilikuwa na nia mbaya kwao.
Alizidi kuwachukia baada ya kuwasikia mganga mkuu na msaidizi wake wakizungumza juu ya wao maalbino kutolewa kafara kwa ajili ya utajiri wa watu. Hakuamini kama kweli Mungu aliwaumba wawe dawa ya utajiri bali viumbe wenye haki ya kuishi kama wengine.
Alijiuliza haki yake itapatikana wapi kwa vile wale wanaoonekana wema mbele ya watu ndiyo haohao walio mstari wa mbele kusaka roho zao kwa udi na uvumba.
Baada ya mwezi kupita huku afya yake ya jeraha ikizidi kuimarika, alipewa taarifa ambazo kwa wengine waliamini ni njema lakini kwake haikuwa hivyo. Walielezwa mfadhili atakuja kuwachukua watoto wawili, mmoja akiwa yeye Kusekwa.
Kilichomshangaza ni kuchaguliwa yeye na mwenzake ambaye alikuwa albino aliyekuwa na umri mdogo kuliko yeye. Alikumbuka jinsi alivyochukuliwa kwenye kambi ya Father Joe na Mr Brown kuwa anakwenda kumtunza kumbe kumtoa roho.
Alitaka kukataa kwenda popote lakini bado hakutakiwa kuonesha kiburi kwa vile kuna watu wenye roho nzuri kama Father Joe. Hakuwa na uwezo wa kukataa kwenda kwa huyo mfadhili. Alikubali kwa shingo upande huku uhai wake akimkabidhi Mwenyezi Mungu.
Siku ya kuja kuchukuliwa ilipofika alikutwa akiwa amejipumzisha kwa vile haikuwa siku ya masomo. Aliliona gari likija, halikuwa geni machoni mwake, baada ya wageni kushuka, jicho lake lilitua kwa hasimu wake mkubwa Mr Brown. Akiteremka kwenye gari akiwa na wapambe wake walewale aliokuja nao kumchukua kwa Father Joe.
Aliamini kabisa Mr Brown hakujua anayemfuata ni Kusekwa, angejua ni yeye asingekuja zaidi ya kuwatuma wapambe wake. Alimuona akitembea kuelekea ofisini kwa mkuu wa kituo kile cha Misheni chenye hospitali kubwa. Moyo ulimlipuka na kujua alichokuwa akikiwaza kilikuwa kimetimia. Mr Brown alikuwa amemfuata kwa kivuli cha wema wa kuwasaidi huku wengi wakijua ni viumbe kama yeye wanapewa upendeleo wa kwenda nje ya nchi kusoma.
Kumbe ilikuwa safari ya kuzimu yenye maumivu makali ya kukatwa viungo bila ganzi, akiwa bado anatafakari, dada mlezi wa kituo kile alimfuata.
"Kusekwa jiandae basi wageni wameshafika, tena una bahati nasikia watu wa aina yenu ndiyo hupata nafasi ya kwenda nje kusoma."
Je, Kusekwa atafanya nini? Usikose...
0 comments:
Post a Comment