WAKALA WA SHETANI -27

Author

#Wakala_wa_Shetani -27-.......

Alipopapasa vizuri, aligundua ile ni Toyota Pick Up, akiwa anajiuliza pale ni wapi, mara umeme uliwaka. Kusekwa alijiona yupo kwenye maegesho ya magari, kabla hajaamua afanye nini aliwasikia watu wakielekea kwenye gari hilo huku wakizungumza.
“Inabidi tuwahi kuondoka muda huu mzigo umefika tangu saa saba.”
“Itakuwa vizuri, Mr Brown alikuwa hana raha kabisa.”

Sauti zile zilimfanya Kusekwa aingie chini ya gari na kujificha, akaendelea kumuomba Mungu. Kuwaka kwa umeme kulifanya eneo lote ling’ae kama mchana na kumfanya Kusekwa aamini lazima atakamatwa kutokana na kuwaona

askari wakipishana kuhakikisha ulinzi unaimarishwa mgodini.

#SASA_ENDELEA...

Ndani ya chumba cha kukatia viungo vya albino, baada ya umeme kurudi wauaji wale walishtuka kukuta Kusekwa hayupo sehemu waliyokuwa wamemlaza Kusweka.

“Wazee yule mtoto amekwenda wapi?” mmoja alishtuka na kuuliza huku macho yakiwa yamemtoka pima.
“Si alikuwa amelala hapa?” mmoja alionesha kwa kidole alipokuwa amelala Kusekwa.
“Utani huu, au ametoroka?”
“Inawezekana lakini hata akitoroka atafika wapi? Lazima tutamkamata tu.”
“Tatizo si kukamatwa bali kuokoa muda, mtambo bado kidogo ufae, tukimaliza tuanze kumtafuta, kibaya hatujui katokea mlango upi.”
“Mmh! Kazi ipo jamani, kila mtu atoke na mlango wake ili kumtafuta.”

Baada ya kupeana majukumu, waliingia kwenye kazi ya kumtafuta Kusekwa ambaye alikuwa bado yupo chini ya gari akisikiliza mazungumzo ya dereva na mwenzake.

Kila mmoja alikimbia huku akiulizia walinzi kama wamemuona mtoto albino akipita maeneo hayo. Kila aliyeulizwa alisema hajamuona, kila mmoja akapagawa na kujiuliza atakuwa wapi. Wazo la kuwatoroka hawakuwa nalo zaidi ya kufikiria kuchelewa kutekeleza kazi yao kwa muda muafaka.

Waliamini kabisa mtoto huyo lazima angepatikana asubuhi kama hatajitokeza au kumuona sehemu alipojificha. Kusekwa aliiona miguu ya mbaya wake aliyekuwa amesimama karibu yake kabisa akiwauliza wahusika wa lile gari.

“Wazee hamjamuona mtoto albino?”

“Hatujamuona mtu yeyote, tena bahati nzuri tumefika hapa umeme ukiwa umeshawaka lakini eneo hili hatujaona kiumbe chochote, kwani vipi?”

“Kile kitoto kimetoroka, tulikuwa ndiyo tunatengeneza mtambo kwa ajili ya ishu ya bosi.”
“Sasa?”

“Baada ya umeme kuwaka hatukumuona japo tunajua lazima atapatikana.”
“Sasa fanyeni hivi, toeni taarifa kisha endeleeni na kazi ya kuutengeneza mtambo, mnafikiri atafika wapi? Lazima atapatikana tu. Mkianza kumtafuta hamjui mtachukua muda gani na mkimpata ndiyo muanze kazi ya kutengeneza mtambo.
“Hamuoni mtachukua muda mrefu? Lakini mtambo ukitengemaa na akipatikana mtafanya kazi kwa urahisi,” dereva wa gari alishauri.

“Hapo umesema neno, ngoja nitoe taarifa kisha turudi kutengeneza mtambo.”
Maneno yote hayo, Kusekwa aliyasikia na kuendelea kumuomba Mungu japokuwa aliamini kupona ni sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano. Aliomba Mungu wasiliondoe gari haraka kwani lazima angeonekana.

Wale watu baada ya kusema hivyo, waliondoka na kumuacha chini ya lile gari. Baada ya kuondoka Kusekwa alimsikia dereva akisema:
“Acha tuwahi, muda umekwenda.”
Kusekwa alihofia kukanyagwa, alitoka chini ya gari kwa tahadhari kubwa, alipoliangalia lile gari aligundua kuwa nyuma lilikuwa na turubai. Wazo la haraka lilikuwa kuingia nyuma ya gari na kujifunika lile turubai huku akimuomba Mungu atoke salama kwenye mgodi wa kifo.

Mara gari lilianza kuondoka, mapigo ya moyo yalikuwa yakimwenda kwa kasi, kama mtu angekuwa karibu yake angesikia jinsi moyo unavyodunda. Gari lilipofika getini, askari alilisimamisha.
“Jamani simameni tukague gari.”

Kauli ile ilimfanya Kusekwa atokwe na haja ndogo kwa wasiwasi, alimuomba Mungu kwa kujua lazima ataonekana. Gari lilisimama na mlinzi alizunguka nyuma ya gari na kuanza kufunua turubai. Alishangazwa na sehemu moja iliyokuwa na mwinuko.

Bila kusema neno, alisogea hadi kwenye mwinuko na kufunua. Alipofunua turubai alishtuka kumuona mtoto albino akiwa nyuma ya gari, akiwa amejifunika turubai lile. Alipigwa na bumbuwazi na kujiuliza yule mtoto mbona yumo kwenye lile gari tena kajificha,

alishangaa kumuona mtoto akimuomba msamaha kwa kukutanisha mikono yake bila kusema neno huku machozi yakimtoka.
Alikumbuka taarifa ambazo alizipata juujuu kuhusu mauaji ya walemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina katika mgodi wa Mr Brown. Aliamini kabisa mtoto huyo alikuwa akitoroka. Alishindwa aseme nini, alibaki kumtazama kwa huruma.
Dereva baada ya kuona muda unakatika kwa ukaguzi wa dakika mbili, aliuliza:

“Mzee Kondo mbona unauweka usiku? Umekuta nini naona umeganda?”

“Hakuna kitu, mnaweza kwenda,” alisema huku akirudisha turubai na kumuacha yule mtoto albino kwenye gari.

Alimruhusu dereva ambaye aliondoa gari na kutoka nje ya mgodi bila kujua nyuma ya gari kuna mtu. Kusekwa alimshukuru Mungu

gari kutoka salama mgodini. Gari lilikwenda kwa mwendo mrefu bila Kusekwa kuelewa alikuwa akielekea wapi, akaendelea kujificha kwenye turubai kutokana na upepo mkali. Sehemu moja gari lilisimama, akawasikia wale jamaa wakizungumza.

“Bwana eeh, tuchimbe dawa hapa.”
“Siyo mbaya.”

Kusekwa alitulia wakati watu wale wakiteremka kwenda kujisaidia haja ndogo. Wakati wanaingia kwenye gari ili waondoke,

Kusekwa aliteremka haraka na kuliacha gari liende. Sehemu aliyoshuka ilikuwa ngeni kwake. Kulikuwa na vichaka ambavyo hakuwa na uhakika wa usalama wake.

Itaendelea...

0 comments:

Post a Comment