WAKALA WA SHETANI MWISHO
#ILIPOISHIA:
Ilikuwa ajabu ya mwaka, kila walivyojitahidi kufungua milango ili waruke nje, iligoma kufunguka huku gari likizidi kuelekea bondeni.
#SASA_ENDELEA...
Wakati huo mvua kubwa ilikuwa ikiendelea kunyesha na kusababisha maporomoko ya maji yaliyotengeneza mto kutokea juu ya mlima. Gari lilizidi kuserereka na kusogea kwenye ukingo wa bonde lile na kumfanya Mr. Brown na watu wake kutahayari. Gari lilikosa kizuizi na kuporomoka hadi bondeni na kuangukia kwenye maji yaliyokuwa yamejaa mtoni na kwenda kwa kasi.
Gari lilianza kuzama kwenye mafuriko ya maji yaliyotokea juu ya mwinuko, ilikuwa ajabu mvua kama ile ilikuwa haijanyesha kwa kipindi kirefu.
Haikuwa na tofauti na ile iliyonyesha wakati Kusekwa alipozaliwa.
Kila walivyojitahidi kujitoa kwenye gari walishindwa, maji yaliwafunika na kujikuta walikosa hewa, wote watano waliokuwa kwenye gari walikuwa wakifa pamoja na mkuu wao Mr. Brown.
Mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha ilimzindua Kusekwa aliyekuwa amekwama kwenye tawi la mti. Alipotaka kujigeuza alijikuta akiporomoka kutoka juu ya mti na kuangukia kwenye maji yaliyokuwa yakitembea kwa kasi.
Alipotua, maji yalianza kumsafirisha, alijikuta akipigania roho yake kwa kurusha mkono wake mmoja. Mungu alimsaidia aliweza kukwama kwenye rundo la majani lililokuwa limejikusanya baada ya kutolewa mbali na mvua.
Kutokana na hofu ya kupoteza maisha kumtawala, alijikuta akipoteza tena fahamu. Alilala kwenye majani mpaka alfajiri aliposhtuliwa tena na sauti za wanakijiji waliomuona.
Walimchukua na kumpeleka kwa mjumbe wa nyumba kumi ili apate hifadhi kabla ya kuhojiwa ili kujua amepatwa na masahibu gani. Kusekwa hakuamini kujiona akiwa bado yupo hai kwa yote yaliyomtokea baada ya kukutana na Mr. Brown. Kila dakika aliona miujiza ya Mungu iliyomtoa kwenye kinywa cha mauti.
Baada ya kupatiwa huduma ya kwanza kwa kupewa kifungua kinywa na kupata muda wa kupumzika walimuuliza kwa utaratibu kujua amepatwa na nini.
Kabla hajatoa maelezo yake zililetwa habari kuwa kuna gari limeangukia bondeni. Waliokwenda kulitazama walirudisha taarifa kuwa ndani ya gari wamekuta kuna maiti tano, ya Mzungu mmoja na Waswahili wanne.
Wanakijiji waliungana tena kwenda kuzichukua zile maiti na kuzileta kijijini, Kusekwa pamoja na ugeni wake naye alikwenda kuziona maiti hizo. Mawazo yake yalimtuma huenda ni Mr. Brown japokuwa kwa akili ya kawaida alijua haiwezekani.
Alipofika naye alijipenyeza kwenye kundi la watu, kingine, kilichomshtua ilikuwa kuwaona watoto maalbino zaidi ya kumi wakicheza bila hofu yoyote. Alipojipenyeza alifanikiwa kuziona sura za wabaya wake. Alipoiona maiti ya Mr. Brown aliangua kilio kilichowashtua watu wote waliokuwepo pale.
Mjumbe alimchukua Kusekwa na kumpeleka nyumbani huku akimbembeleza, lakini haikusaidia kitu aliendelea kulia. Alidhani huenda kuna ndugu yake.
"Kijana kuna ndugu yako katika wale maiti?" Kusekwa alikataa kwa kutikisa kichwa.
"Sasa nini kinakuliza?"
"Hao ndiyo walitaka kuniua."
"Kukuua?" mjumbe alishtuka.
"Ndiyo."
‘Kivipi?"
Kusekwa ilibidi aanze kumhadithia maneno mazito ya tangu kuzaliwa kwake. Mjumbe aliona maneno yale hawezi kuyasikiliza peke yake akawaita wakuu wenzake na kumuweka chini.
Kusekwa alielezea safari yake toka kuzaliwa mpaka siku ile aliyofika pale kijijini. Wote waliomsikiliza walishikwa na mshangao wasiamini alichokuwa akikisema.
"Kumbe hawa ni watu wabaya, kwa vile maiti haina adui wazikwe kaburi moja," mjumbe alisema.
Walikubaliana kuwazika Mr. Brown na vijana wake kaburi moja. Baada ya mazishi kikao cha kijiji kilikaa mara moja kupanga jinsi ya kumsaidia Kusekwa na kupeleka taarifa serikalini ili kukomesha mauaji ya walemavu wa ngozi na kufanya uchunguzi kwa taasisi zote zinazojitolea kuwasaidia wasiojiweza.
Mzee mmoja alijitolea kumlea Kusekwa na kumsomesha mpaka mwisho wa elimu yake.
Wakati huo Ng'wana Bupilipili baada ya kukimbia kwenye ile kambi alijikuta akifikia kwenye Kijiji cha Busesa alichopokelewa mwanaye Kusekwa.
Baada ya kufika alipokelewa na mzee mmoja aliyekuwa mjane na kumchukua kama mkewe.
Mpaka mwanaye Kusekwa anafika katika kijiji kile alikuwa na mtoto wa miaka mitatu na mimba juu, mmoja wa watoto wake watatu alikuwa albino.
Siku moja alisikia taarifa za kuokotwa kwa mtoto albino mwenye mkono mmoja. Jina lake na taarifa zake zilimshtua, alipatwa na shauku ya kumjua huyo mtoto.
Alikwenda hadi katika nyumba aliyokuwepo Kusekwa, akiwa na hamu ya kumuona huyo mtoto. Alipofika alimuona mtoto mwenye ulemavu wa ngozi akiwa amekaa akicheza na wenzake.
Alipomuangalia sana mwili ulimsisimka na kuamini kuwa ndiye mwanaye wa kuzaa ambaye wakati huo alikuwa na mkono mmoja.
Alijikuta akitamka kwa sauti.
"Kusekwa."
Kusekwa alishtuka na kugeuka bila kuitikia alimtazama aliyemwita, Ng'wana Bupilipili huku machozi yakimtoka alimwita huku akimfuata.
"Kusekwa mwanangu."
Kusekwa naye bila kujielewa alijikuta akinyanyuka na kwenda kumkumbatia mama yake. Ng'wana Bupilipili alijikuta akilia kwa uchungu hasa baada ya kumuona mwanaye akiwa na mkono mmoja. Watu hawakuamini historia iliyojirudia kwa watu waliopotezana kukutana tena.
Baada ya Ng'wana Bupilipili kumpata mwanaye ambaye hakuwaza hata siku moja kama kuna siku wangeweza kuonana tena, alipiga magoti na kumshukuru Mungu.
"Asante Mungu, umedhihirisha tena kuwa wewe unaweza kufanya kisichowezekana katika akili za kibinadamu. Huu muujiza ulionifanyia mbele yangu ni zaidi ya kumfufua aliyekufa, ni zaidi ya ngamia kupita kwenye tundu la sindano. Asante Mungu, asante baba, asante kwa kudhihirisha kuwa wewe ni mwanzo na mwisho."
Baada ya kushukuru alimkumbatia mwanaye na kuwafanya watu wote waone muujiza ambao Mungu ameufanya kwa yeyote anayemuamini. Alimchukua na kurudi naye nyumbani kwake.
***
Taarifa za kuwepo na migodi inayotumia nguvu za kishirikina kuua albino ili wapate mali nyingi zilipelekwa kwenye vyombo vya dola na kufuatia taarifa zile ambazo hata mkuu wa kambi aliyotoroka Kusekwa alikwisha peleka taarifa kwenye vyombo vya usalama.
Msako mkali ulifanyika katika migodi mingi na watu wote wanaoishi pembezoni mwa machimbo. Wengi walikamatwa na viungo vya albino vilivyokuwa vipo tayari kuuzwa kwa wamiliki wa migodi wenye kuabudu nguvu za giza.
Mgodi wa Mr. Brown ulitaifishwa na serikali na wote waliobakia katika mgodi huo walikamatwa na kufunguliwa kesi za mauaji. Baada ya operesheni iliyovumbua vitu vingi, serikali ilitoa tamko kwa watu wote kuwa makini na wageni wanaotumia njia za dini au uwezo wa fedha zao kuwasaidia watu huku wakifanya hujuma ya kuliteketeza taifa.
Kuanzia siku ile ulinzi uliimarika kwa albino wote. Wageni wote waliwekwa chini ya uangalizi mkali na serikali.
Kusekwa alifanikiwa kusoma akiwa na mkono mmoja na kujiunga cha chombo cha sheria cha kutetea watu wenye matatizo.
Serikali ilimuongezea elimu, sasa hivi ndiye mkuu wa kitengo cha sheria na anapata mshahara mzuri unaomuwezesha kumlea mama yake na kuwasomesha
wadogo zake.
Huu ndiyo mwisho wa riwaya yetu ila lazima tuamini kila mwanadamu ana haki ya kuishi hakuna mtu aliyeumbwa kwa ajili ya kumpatia mwenzake utajiri kupitia damu yake. Imani potofu imesababisha maisha ya wenzetu wenye matatizo ya ngozi kuwa ya wasiwasi na wengine kuongezewa vilema vya maisha au kuuawa.
Uhai wao unaonekana na waovu na kunukia kwa kila mpenda pesa. Kila apataye fedha kwa damu ya mtu huwa wakala wa Shetani ambaye ameamua kuwa mfuasi wakek wa kutenda dhambi kila siku.
Tusifanye hivyo, kila mtu ana haki ya kuishi na kufurahia maisha, siri ya utajiri si kutoa damu ya mtu bali ni kufanya kazi kwa bidii.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment