WAKALA WA SHETANI -32

Author

#Wakala_wa_Shetani 32
 
#Ilipoishia
"Kama ni kweli tuna dhambi kubwa ya damu za watoto hao ambao tulijua wapo Ulaya kumbe kuzimu," Father alisema kwa masikitiko.
"Mkuu hili lisilale, ikiwezekana tukaliripoti leoleo."
"Hapana Anna, tusifanye papara, nitampigia mpelelezi mkuu wa makosa ya jinai ni rafiki yangu mkubwa. Atakuja hapa tutamueleza yote, nina imani atayafanyia kazi."
#SASA_ENDELEA...

"Kama ni hivyo itakuwa heri."
"Sasa Kusekwa atakuwa wapi?"
"Sijui, nina imani akiwaona wameondoka atarudi."
Kusekwa baada ya kutoka eneo la kambi, aliingia porini. Kutokana na hofu ya maisha yake, alikimbia kwa muda wa saa tatu bila kupumzika. Baada ya kukimbia kwa muda mrefu alijikuta akichoka na kuamua kujipumzisha kwenye mti uliokuwa na hewa safi.
Bila kujielewa, usingizi mzito ulimpitia, alishtushwa na sauti za watu waliokuwa wakizungumza. Alipofumbua macho hakuamini kumuona Mr Brown akiwa na vijana wake mbele yake.
"Bosi huyu si Kusekwa?"
"Ni yeye, mbona hana mkono mmoja?"
"Tumuulize."
Kusekwa baada ya kukurupuka alipokuwa amelala, alitaka kukimbia lakini walimuwahi na kumkamata.
"Vipi wewe mbona upo hapa?" Mr Brown alimuuliza.
Kusekwa hakuwajibu, aliangua kilio cha hofu akiamini bado mauti yalikuwa yakimuandama, pamoja na kuyakimbia kila kukicha tangu alipozaliwa. Mr Brown alijifanya msamaria mwema kwa kumbembeleza.
"Kusekwa usilie, nipo hapa kwa ajili ya kukusaidia, umefikaje huku na muda wote ulikuwa unaishi wapi?"
Kusekwa hakujibu kitu, aliendelea kulia akiwa amekaa chini, pembeni ya ile barabara kulikuwa na bonde kubwa. Kusekwa wazo lake kubwa lilikuwa kujitupia bondeni, aliona heri afe kwa kujitupa bondeni kuliko kukatwa viungo na Mr Brown.
Mr Brown aliagiza achukuliwe na kuingizwa kwenye gari, msaidizi wake alimbeba juujuu ili kumuingiza ndani ya gari. Kusekwa, kwa kutumia mkono wake mmoja alimshika jamaa jichoni nusura amtoe jicho, maumivu aliyoyapata yalimfanya amtupe chini.
Alipofika chini alitimua mbio kuelekea kwenye lile bonde, hawakukubali, walianza kumfukuza ili wamshike. Alikimbia kwa nguvu zake zote ili kujiokoa katika mikono ya wauaji. Mr Brown baada ya kuona Kusekwa amewazidi mbio alisema kwa sauti ya juu:
"Kama anawasumbua mpigeni risasi ya mguu."
Kusekwa kusikia hivyo, alijua mauti yapo usoni kwake, bila kuangalia anaangukia wapi alijitupa bondeni. Kilichoendelea hakujua baada ya kujipiga sehemu na kupoteza fahamu.
Mr Brown hakukubali, aliutaka mwili wa Kusekwa akiwa hai au umekufa, shida yake ilikuwa viungo vilivyobakia. Vijana wake waliingia bondeni kumtafuta. Kutokana na bonde kuwa refu kwenda chini na kutokuwa na njia ya karibu, walisogea mbele kutafuta njia ya karibu kisha kurudi eneo alilojitupia Kusekwa.
Msako ulichukua zaidi ya saa mbili bila kuuona mwili wa Kusekwa. Kutokana na kina cha bonde kuwa na miti, waliamini huenda amekwama kwenye mti. Waliamua kupiga risasi ovyo kwenye miti, kwa bahati mbaya walikuwa na risasi chache hivyo walishindwa kuendelea kupiga.
Kingine kilichowachanganya ni giza lililoanza kuingia, waliamua kuondoka huku wakijipanga kwenda kuwaita vijana walinde eneo lile mpaka aonekane. Walielekea katika gari lao ili waondoke huku Mr Brown akimlaumu kijana wake kuonesha uzembe wa hali ya juu kwa kushindwa kuvumilia maumivu ya makucha ya jicho aliyopigwa na Kusekwa.
"John leo umeniangusha sana."
"Bosi ningechelewa kidogo angenitoa jicho, aliingiza kucha kwenye mboni ya jicho."
"Basi ungempigiza chini ili asikimbie kuliko kumuacha vile na kutufanya tuonekane wazembe kila siku kwa mtu mmoja. Mnaona alitoroka na mikono miwili lakini leo tumekutana naye akiwa na mkono mmoja? Tukimpoteza leo tutakutana na mzoga wake ukiwa umemalizwa viungo vyote, siyo sisi tu tunaotafuta viungo vyao, si mnajua kuna migodi mingapi?"
"Bora iwe hivyo lakini kama ataokotwa na msamaria mwema lazima atatoa siri yetu, mnafikiri kutakuwa na usalama tena kwetu? Lazima serikali itataka kufanya uchunguzi juu ya maalbino wote tuliowachukua kwa kisingizio cha kuwapeleka Ulaya."
"Usemacho ni kweli, lazima tufanye msako wa kufa mtu ili tuhakikishe tunamtia mikononi huyu mtoto la sivyo tutaumbuka," Mr Brown alizungumza akiwa amekunja uso kwa hasira.
"Ni kweli mkuu, kwa nini usipige simu mgodini ili kuleta jeshi litakalolinda eneo hili kuhakikisha huyu mtoto hatoki na kuangukia mikononi mwetu?"
"Ni kweli lakini sehemu hii haina mawasiliano kabisa, mbona ingekuwa hivyo ingekuwa rahisi kwetu?"
"Sasa tutafanyeje na usiku ndiyo unaingia?"
"La muhimu tuwahi kambini tuchukue baadhi ya watu waje hapa. Nimepata wazo jingine, bora niwaache ninyi hapa ili mlinde eneo hili mimi nitaondoka kwenda kuleta vijana wa kulinda, ambao watawapokeeni au mnasemaje?"
"Mkuu wazo zuri sana, hata mimi nilikuwa na wazo kama hilo."
"Okay, mimi niwaache ili niwahi mgodini."
Kabla hajaingia kwenye gari ili aondoke, lilitanda wingu zito lililoashiria kuteremka mvua kubwa. Mara mvua kubwa ilianza kunyesha, wote walikimbilia kwenye gari na kupandisha vioo juu. Mvua iliendelea kunyesha na kulifanya gari lao kuanza kuserereka kutokana na kulisimamisha pembeni ya bonde lile lenye udongo wa mfinyanzi.
Dereva alipoona vile, aliliwasha harakaharaka na kuweka ‘four wheel drive' kuliondoa lakini alikuwa kama ndiyo analiongeza kulitelezesha kwenda bondeni. Ilikuwa ajabu ya mwaka, kila walivyojitahidi kufungua milango ili waruke nje, iligoma kufunguka huku gari likizidi kuelekea bondeni.
Wakati huo, mvua kubwa ilikuwa ikiendelea na kusababisha maporomoko ya maji yaliyotengeneza mto kutoka juu ya mlima. Gari lilizidi kuserereka kusogea kwenye ukingo wa bonde hilo na kumfanya Mr Brown na watu wake waanze kuhaha. Gari lilikosa kizuizi na kuporomoka hadi bondeni, likaangukia kwenye maji yaliyokuwa yamejaa na kwenda kwa kasi.

Je, nini kitafuatia? Usikose...

0 comments:

Post a Comment