WAKALA WA SHETANI -31

Author

#Wakala_wa_Shetani -31-......

Anna alishindwa kujibu na kubakia akikapua macho kama kameza mfupa, kitu kilichomfanya mkuu wake anyanyuke kwa kuwaomba msamaha wageni.
"Jamani samahani, nakuja."
"Bila samahani," walijibu kwa pamoja.
Alimfuata Anna na kutoka naye nje baada kugundua alikuwa na kitu kilichokuwa kikimtatiza, haikuwa kawaida yake kuwa vile. Baada ya kutoka naye nje alimuuliza kwa sauti ya upole.
"Vipi mbona hivyo, Kusekwa yupo wapi?"
"Kuna tatizo father!"

#SASA_ENDELEA...

"Tatizo! Kusekwa kafanya nini?" Father alishtuka.
"Father kuna makosa makubwa tutakuwa tumefanya bila kujua."
"Makosa gani?"
"Kama ni kweli tutakuwa tumepata dhambi kubwa kwa kutoa roho za albino wasio na hatia."
"Una maana gani kusema hivyo?"
Anna alimueleza yote aliyoelezwa na Kusekwa na uamuzi aliochukua wa kukimbia.
"Anna unasema kweli!?" Father alishtuka sana kusikia vile.
"Ni kweli, Kusekwa amejuaje kama yule Mzungu anaitwa Mr Brown?"
"Hapo si ndiyo nashangaa kusikia hivyo!"
"Inaonekana kumbe maalbino wote tuliokuwa tukimpa na kusema anawapeleka nje kusoma kumbe alikuwa akiwakata viungo kwa imani za kishirikina kwa ajili ya mgodi wake."
"Lakini watakuwa wanamsingizia, mbona hafanani na tuhuma hizo?"
"Kusekwa aliyosema mwanzo si alitueleza kuwa alitoroka katika mgodi, Mr Brown hana mgodi?"
"Anao."
"Na jina siyo lake?"
"Ni lake."
"Basi Father umiza kichwa, la sivyo tutaendelea kuwatoa kafara watoto maalbino huku tukijua kinachoendelea, tutakuwa wauaji."
"Mmh! Hii mpya, sasa tutafanya nini maana jamaa anajua anaondoka na albino wawili?"
"Hakuna cha kujiuliza, mueleze tumesitisha kuwatoa watoto maalbino."
"Atanielewa kweli, mtu nilishamkubalia na mtoto tumeshamuandaa na amemuona?"
"Mimi nafikiri suala la uhai wa mtu si la kufumbiwa macho, kama wewe huwezi niachie mimi nitamueleza. Huoni tuna dhambi ya watoto wote ambao tuliambiwa wamekwenda Ulaya kusoma kumbe ni Ulaya ya kuzimu?"
"Mmh! Ipo kazi."
"Father kama huwezi niachie niwaeleze, roho inaniuma sana kuona watoto wote tuliompa Mr Brown amewaua kikatili kwa kuwakata viungo," Sister Anna alisema kwa uchungu.
"Okay, nimekuelewa niache nikawaeleze kwamba Filipo haondoki."
Baada ya mazungumzo ya siri waliongozana hadi kwa wageni, mkuu wa kituo baada ya kukohoa akasema:
"Samahani kwa kuwaweka kwa muda mrefu."
"Bila samahani," walijibu wote.
"Kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu, hatutakupa watoto kwa vile nilipitiwa kuwaeleza kuwa watoto kabla ya kuondoka walitakiwa kuonana na wazazi wao."
"Mkuu mbona unaharibu mambo, si unajua kampuni yangu inahusika kuwapeleka nje watoto wenye ulemavu wa ngozi?" Mr Brown alilalamika.
"Ni kweli, lakini hata watoto wasio na ulemavu wa ngozi nao wanahitaji kwenda nje," Father alisema.
"Ni kweli, lakini wenye ulemavu wa ngozi ndiyo waliopewa kipaumbele kutokana na kusakwa na watu na kuwakata viungo. Hivyo tumewapa kipaumbele wao ili kuwaweka sehemu salama," Mr Brown alitetea hoja yake.
"Sina hakika kama walemavu wanaoonewa huruma ni wa ngozi tu, mbona wapo wengi?" Sister Anna alihoji.
"Huo ni mpango uliopangwa mwakani kuwachukua watoto mchanganyiko."
"Sawa lakini kama nilivyokueleza hawawezi kuondoka bila kuonana na wazazi wao," Father alikataa kuwatoa watoto.
"Wanakuja lini?"
"Hawakusema ila walituma ujumbe lazima waonane na watoto wao."
"Lakini nina siku moja tu, kama vijana hawa ningeondoka nao leo wangeungana na wengine wanane kuondoka keshokutwa, tena wana bahati ya mtende," Mr Brown alizidi kuwatia tamaa.
"Ni kweli, lakini hatuwezi kukiuka kauli ya wazazi wao kwa vile sisi ni walezi lakini wenye haki ni wazazi wao."
"Sasa mkuu, mimi nitakuachia hapa kiasi cha pesa wakija wape ili wasikusumbue."
"Kama pesa hata mimi ningewapa, lakini naheshimu kauli zao kwa vile wao ni wazazi sisi ni walezi tu, hatuna mamlaka ya kwenda kinyume na makubaliano tuliyokubaliana. Mbona waliotangulia tulikupa bila kipingamizi tena wengi kuliko hawa wawili?"
"Kwa hiyo nisubiri mpaka lini?"
"Wakija leo nitakujulisha uje kesho, wakija kesho vilevile nitakujulisha, usife moyo."
"Okay, hatuna jinsi."
Mr Brown aliondoka akiwa amenyongea baada ya kuwakosa wale maalbino wawili, waliingia kwenye gari lao na kuondoka kurudi mgodini. Baada ya kuondoka walibakia mkuu wa kituo na Sister Anna wakijadiliana.
"Father umeona?" Sister Anna aliuliza.
"Nimeona."
"Anataka kutoa pesa ili awanunue watoto, huoni kama ana maslahi nao?"
"Ni kweli."
"Sasa hizi taarifa zifike kwenye vyombo vya dola ili wachunguzwe na wakigundulika wachukuliwe hatua kali."
"Kuna muhimu wa kufanya hivyo, bado siamini kama kweli watoto wote aliowachukua amewaua kwa kuwakata viungo. Kama ni kweli tuna dhambi kubwa ya damu za watoto wale ambao tulijua wapo Ulaya kumbe kuzimu," Father alisema kwa masikitiko.
"Mkuu hili lisilale, ikiwezekana tukaliripoti leoleo."
"Hapana Anna tusifanye papara, nitampigia mkuu wa makosa ya jinai, ni rafiki yangu mkubwa. Atakuja hapa na tutamueleza, yote nina imani atayafanyia kazi."

Je, nini kitaendelea? Usikose...

0 comments:

Post a Comment