WAKALA WA SHETANI -30

Author

#Wakala_wa_Shetani -30-....

ILIPOISHIA:
Aliamini kabisa Mr Brown hakujua anayemfuata ni Kusekwa, angejua ni yeye asingekuja yeye zaidi ya kuwatuma wapambe wake. Alimuona akitembea kuelekea ofisini kwa mkuu wa kituo kile cha Misheni chenye hospitali kubwa. Moyo ulimlipuka na kujua alichokuwa akikiwaza kilikuwa kimetimia, Mr Brown alikuwa amemfuata kwa kivuli cha wema wa kuwasaidia huku wengi wakijua ni viumbe kama yeye wanapewa upendeleo wa kwenda nje ya nchi kusoma.
Kumbe safari ya kuzimu yenye maumivu makali ya kukatwa viungo bila ganzi, akiwa bado anatafakari, dada mlezi wa kituo kile alimfuata.
"Kusekwa jiandae basi wageni wameshafika, tena una bahati nasikia watu wa aina yenu ndio hupata nafasi ya kwenda nje kusoma."

#SASA_ENDELEA...

Kusekwa hakujibu zaidi ya kutokwa machozi, Sister Anna alimshangaa Kusekwa alikuwa tofauti na Albino mwenzake aliyekuwa na furaha.
"Kusekwa mbona unalia hukufurahia safari hii?"
"Hii dada si safari ya Ulaya bali ya kifo."
"Kusekwa una maana gani?"
"Dada ni hadithi ndefu ya maisha yangu, nimeweza kuruka mkojo nikakanyaga kinyesi."
"Kusekwa una siri gani ya muda mrefu uliyoiweka moyoni mwako?"
"Wee acha, maisha yangu yamezungukwa na shetani wa mauti."
"Ni kweli, sasa hivi mmekuwa akitafutwa sana na watu wabaya kwa ajili ya kuwatoa kafara. Ndio maana tumekuwa makini kuwalinda kwa nguvu zote ndani ya kituo chetu, muda wote mmepewa kipaumbele hata wafadhili wanapokuja ninyi ndio mnaotakiwa kuondoka.
"Huoni wenzako wana miaka miwili hawakupata nafasi hiyo, lakini wewe na mwenzako mmepewa upendeleo. Huyu mfadhili aliyekuja ni mtu tunayemuamini amekuwa akiwachukua watoto wengi hasa wenye hali kama yako na baada ya muda hutuletea taarifa kuwa amewapeleka nje kusoma."
"Dada mpaka sasa mmeshampa watoto wenye hali kama yangu wangapi?" Kusekwa aliuliza.
"Ni wengi hata thelathini wanafika."
"Mungu wangu!" Kusekwa alishika kichwa.
"Kwani vipi mbona unanitisha Kusekwa?" Sister Anna alishtuka.
"Mna dhambi ya kutoa roho ya watu wote hao na kesho kwa Mungu mna la kujibu."
"Kusekwa kwanini unasema hivyo?"
"Wote uliompa Mr Brown sasa hivi ni nyama ya udongo wakiwa na viungo nusu."
"Mungu wangu, unasema kweli! na umemjuaje Mr Brown?"
"Ndio ushangae kumjua Mr Brown, ni kiumbe mbaya kuliko nyoka aliyelaaniwa na Mungu, cheko lake nyuma ameficha madhambi ya damu za watu wasio na hatia. Kama hapa ameua watu zaidi ya thelathini unafikiri vituo vingine wameuawa watu wangapi?"
"Kusekwa unayosema ni kweli?" Sister Anna alizidi kumshangaa.
"Chanzo cha mimi kukatwa mkono kilikuwa yeye, nilikuwa nimepona kwenye kinywa cha mauti na kuangukia kwenye mikono ya viumbe wenye uchu. Nashukuru nimekatwa mkono lakini kwa Mr Brown ningebakia kiwiliwili kisicho na mikono na miguu."
"Wewee!!"
"Dada yangu shangaa ya Musa uyaone ya Firauni."
"Kusekwa, ilikuwaje?"
Kusekwa alimueleza toka alipokuwa katika kituo cha kulelea watoto wenye matatizo, na chanzo cha yeye kuwa pale. Kutokana na historia aliyopewa mama yake alitoroka baada ya kulipa kisasi cha kuua wanakijiji waliomuua baba yake pamoja na kuchukua mali zao kinguvu yakiwemo mashamba na mifugo.
Sister Anna alibakia mdomo wazi huku muda ukiwa umekwenda.
"Lazima nikiri kuwa Mungu mkubwa ndiye aliyeniokoa na mauti yale, nilikuwa nimeshafungwa kwenye mashine tayari kukatwa viungo bila ganzi. Tena kibaya wanaofanya hivyo ni miongoni mwa ndugu zetu tunaoishi nao sehemu moja kutokana na tamaa ya pesa wanakosa utu ndani ya mioyo yao na kututoa uhai wetu ambao hatukupewa kimakosa na Mungu."
Maneno mazito yaliyochanganyikana na kilio yalimfanya sister Anna kutokwa ma machozi bila kujijua, akiwa hajapata cha kumwambia Kusekwa, walishtuliwa na mkuu wa kituo aliyewafuata baada ya kuona wanachelewa.
"Anna unafanya nini, mtoto mmoja tayari huyo unafanya naye nini muda wote niliokutuma?" mkuu wa kituo aliuliza kwa ukali.
"Samahani mkuu, anakwenda kuoga sasa hivi," alimjibu bila kugeuka.
"Kwa vile hajachafuka kambadilishe nguo tu umlete haraka."
"Sawa."
"Haya fanyeni haraka," baada ya kusema vile aligeuka na kuondoka akimuacha Sister Anna akitazamana na Kusekwa. Kama mkuu wa kituo angemuangalia vizuri Anna usoni angegundua kitu, lakini haraka yake ilimfanya afikishe ujumbe kuliko kuwaangalia wahusika.
Sister Anna alikuwa akitokwa na machozi kwa maneno mazito ya Kusekwa juu ya vijana maalbino wengi waliopoteza maisha yao bila hatia kwa kisingizio cha kupelekwa nje ya nchi kusoma. Alimtazama Kusekwa na kukosa cha kumwambia kwani aliamini kabisa hatakubali kuondoka na Mr Brown baada ya kunusurika kwenye kinywa cha mauti.
"Sasa Kusekwa tufanye nini?" Sister Anna alimuuliza Kusemwa.
"Dada Anna mimi huko siendi labda mauti yangu, siwezi kurudi ndani ya kinywa cha mauti."
"Sawa, sasa tutafanyeje na muda unakwenda?"
"Mimi natoroka siendi huko."
"Hata mimi sikushauri uyafuate mauti tena uliyakimbia kwa muujiza wa Mungu , lakini nitamueleza nini mkuu anielewe?"
"Mweleze ukweli wala usimfiche, acha niondoke eneo hili kabla hajaja tena."
Kusekwa alikwenda chumbani kwake na kuvaa nguo nzito na viatu na kuondoka eneo la kambi aliyokuwa karibu msitu wa miti ya asili, iliyopandwa kwa ajili ya kulinda mazingira na kutengeneza vyanzo vya maji.
Kusekwa akiwa amevaa nguo zake za baridi aliingia porini na kuanza kukimbia katikati ya msitu akiwa na mkono wake mmoja lakini alikuwa ameshauzoea.
***
Baada ya Kusekwa kukimbia na kuondoka eneo la kambi ile, Sister Anna alijikuta akitafuta cha kumwambia mkuu wake. Alikwenda taratibu hadi ofisini ambapo mtoto mwingine albino alikuwa tayari ameandaliwa kwa ajili ya kuondoka na Mr Brown.
Mkuu wake alishangaa kumuona Anna peke yake bila Kusekwa.
"Vipi mbona unakuja peke yako?"
"M..mm...," Sister Anna alikosa jibu.
"Vipi! Mbona sikuelewi yupo wapi muda unakwenda si unajua wanakaa mbali?"
Anna alishindwa kujibu na kubakia akitoa macho kama kameza mfupa, kitu kilichomfanya mkuu wake anyanyuke kwa kuwaomba samahani wageni.
"Jamani samahanini, nakuja?"
"Bila samahani," walijibu kwa pamoja.
Alimfuata Anna na kutoka naye nje baada ya kugundua alikuwa na kitu kilichokuwa kikimtatiza kwani haikuwa kawaida yake kuwa vile. Baada ya kutoka naye nje alimuuliza kwa sauti ya upole.
"Vipi mbona hivyo, Kusekwa yupo wapi?"
"Kuna tatizo father!"
Itaendelea wiki ijayo.

Je, nini kitaendelea? Usikose..

0 comments:

Post a Comment