#Wakala_wa_Shetani -26-.........
#MIAKA SABA BAADAYE
Kusekwa aliendelea kukua, akafikia hatua ya kwenda shule iliyokuwa katika kambi hiyo, akaanza chekechea na kuandaliwa kwenda shule ya msingi. Lakini kabla hajaanza
shule ya msingi alitokea Mzungu mmoja aliyekuwa akimiliki machimbo ya dhahabu.
Mzungu huyo aliyejulikana kwa jina la John Brown ‘Mr Brown’ alikuwa na mgodi
mkubwa uliokuwa na wachimbaji wengi sana. Kutokana na uwezo wake wa kifedha aliweza kuwasaidia wanakijiji waliokuwa jirani na machimbo hayo. Alijenga zahanati na
miradi ya maji na umeme ambayo ilikuwa msaada tosha kwa wanakijiji ambao walifaidika na machimbo yake.
Ndani ya eneo lake la machimbo, Mr Brown alijenga shule kwa ajili ya watoto kuanzia miaka miwili na kuendelea. Sifa zake zilizagaa kila kona ya nchi na kuifanya serikali
impunguzie kodi pamoja na kumpa misamaha katika vitu alivyokuwa akiingiza nchini.
Kingine ambacho kiliungwa mkono na wengi ilikuwa ni kuwachukua walemavu wa ngozi (albino) ambao walianza kusoma pale na baadaye kuwapeleka nje ya nchi kwa masomo zaidi.
#SASA_ENDELEA...
Kusekwa naye alichukuliwa na Mr Brown na kuanza masomo yake ya darasa la kwanza.
Baada ya miezi miwili, Kusekwa alipata nafasi ya kusafiri kwenda Ulaya kimasomo. Aliandaliwa sherehe kama wenzake waliotangulia na safari yake ilikuwa siku ya pili alfajiri.
Kama kawaida, Kusekwa alikwenda kulala kusubiri asubuhi asafiri. Siku hiyo alilala sehemu tofauti na anapolala siku zote. Majira ya saa nane za usiku, alishtushwa na watu walioingia chumbani kwake wakiwa wameziba nyuso zao, kabla hajajua nini kinaendelea alivamiwa na kuzibwa mdomo kisha alibebwa juujuu na kupelekwa asikokujua.
Kusekwa alibakia na mawazo wale ni akina nani na mbona wamembeba vile au ndiyo mtindo wa wote wanaosafiri kwenda Ulaya? Alijifikiria kama wangekuwa ni majambazi au watu wabaya wamepitia wapi mpaka kuingia kule chumbani kwenye kambi yenye ulinzi mkali?
Alijikuta akiwa njia panda huku wale watu wakimpeleka kimyakimya bila kuongea chochote. Baada ya muda, aliingizwa kwenye chumba kimoja ambacho kilikuwa na kiti na kukalishwa pale. Baada ya kukalishwa, mtu mmoja aliwasha swichi, mikono na miguu ya Kusekwa ilishikiliwa na vyuma.
Kusekwa alizidi kushangaa watu wale kumfanya vile walikuwa na shida gani tena walionesha siyo wema kwake. Baada ya kubanwa na vyuma, mashine iliwashwa ili kumkata viungo. Lakini ilikuwa ajabu mashine iligoma kuwaka, kitu kilichowachanganya wale watu na kujaribu mara ya pili lakini iligoma.
“Sasa itakuwaje?” Mmoja aliuliza jasho likimtoka baada ya mtambo kugoma.
“Tatizo hili lilitokea hata mwezi uliopita tulipotaka kumkata viungo yule albino lakini baadaye ilikubali na kufanya kazi yake.”
Kauli ile ilimshtua sana Kusekwa na kuona kumbe safari ya Ulaya ni kifo, alianza kulia kwa sauti kuomba msaada lakini aliambulia makofi yaliyomfanya anyamaze kusubiri hatima yake. Alimuomba Mungu kwa kila lugha aliyoifahamu. Aliiomba mizimu ya baba na mama yote imtangulie kumponya katika kinywa kile cha mauti.
Walikubaliana kumfungua ili kurekebisha ule mtambo ambao uligoma kukata viungo vya albino. Walimfungua Kusekwa ambaye alikuwa amepoteza fahamu kwa woga wa kupoteza maisha. Walimlaza chini na kuanza kuufanyia matengenezo mtambo ili uweze kufanya kazi yake vizuri.
Walijitahidi kufanya kazi kwa haraka ili waifanye kazi kwa wakati na kurudisha salamu kwa Mr Brown. Wakiwa katika hali ya kutengeneza mtambo, walimuacha Kusekwa amelala chini kwenye sakafu akiwa kifua wazi. Kutokana na ubaridi wa kwenye sakafu uliosababishwa na kiyoyozi, Kusekwa alizinduka.
Alipofumbua macho taratibu, aliwaona wabaya wake wakihangaika kutengeneza mtambo wa kukatia viungo vya albino. Alitembeza macho taratibu na kuangalia mandhari ya mle ndani na kugundua kuna mitambo mingine miwili na milango minne, kati ya hiyo mitatu ilikuwa wazi.
Ndani ya kile chumba kilichokuwa na mtambo mmoja wa kukatia viungo na mitambo mingine ambayo hakuifahamu, pia kulikuwa na majokufu yaliyoonekana yana kazi ya kuhifadhi viungo vya albino.
Watu wale walikuwa wamemsahau na akili zao zote zilikuwa katika mashine. Akiwa bado amejilaza chini bila kujitikisa kwa kuogopa kumuona na kuhamishia mawazo yao kwake, Kusekwa alipata wazo la kutoroka kwa kunyata huku akimuomba Mungu aweze kutoka salama.
Kabla hajachukua uamuzi huo ambao kwake ilikuwa ni kama kucheza mchezo wa pata potea. Umeme ulikata ghafla na wote waliokuwa katika kile chumba walishtuka, alimsikia mmoja akisema.
“Huu mkosi gani? Mashine ilibakia kidogo kieleweke, kukatika kwa umeme kumeturudisha nyuma kabisa.”
“Unajua kazi hii tunaidharau lakini inaweza kututoa jasho,” mwingine aliongeza.
“Wasiwasi wenu tu, umeme unawaka na kazi inaendelea, tatizo tumeshalijua hatutachukua muda mrefu kulitatua,” wa tatu naye alisema.
Kusekwa aliwashangaa wale watu ambao hawakuwa na chembe ya huruma kwa kutengeneza mtambo ule haraka ili wamgawanye viungo vyake bila huruma. Akiwa bado amejilaza chini, aliwashangaa watu wale pamoja na umeme kukatika hawakumgusia yeye zaidi ya mtambo uwahi kupona na kumtenganisha viungo vyake.
Aliamini muda ule wakati wauaji wasio na huruma wakisubiri umeme uwake naye angejaribu bahati yake ya kutoroka. Alinyanyuka taratibu pale chini alipolazwa na kuanza kutembea kwa mwendo wa kunyata. Aliutafuta mlango, akafanikiwa kuupata na kutoka kwa kunyata bila kujua anaelekea wapi.
Aliendelea kutembea kuelekea nje katika giza nene huku akimuomba Mungu amuepushe na kikombe kile. Baada ya kutembea kwa muda huku akipapasa na kuomba Mungu umeme usiwake upesi, alijikuta akijigonga kwenye kitu, alipopapasa aligundua ni gari.
Alipopapasa vizuri aligundua ile ni Toyota Pick Up, akiwa anajiuliza pale ni wapi, mara umeme uliwaka. Kusekwa alijiona yupo kwenye maegesho ya magari ambayo yalikuwa na magari mengi, kabla hajaamua afanye nini aliwasikia watu wakielekea kwenye ile gari wakizungumza.
“Inabidi tuwahi kuondoka muda huu mzigo umefika tangu saa saba.”
“Itakuwa vizuri, Mr Brown alikuwa hana raha kabisa.”
Sauti zile zilimfanya Kusekwa aingie chini ya gari ile na kujificha, akiendelea kumuomba Mungu. Kuwaka kwa umeme kulifanya eneo lote ling’ae kama mchana na kumfanya aamini lazima atakamatwa kutokana na kuwaona askari wakipishana kuhakikisha ulinzi wa mule mgodini.
Itaendelea....
0 comments:
Post a Comment