#Wakala_wa_Shetani -25-......
“Kwa usemi huo ni kweli kabisa, mmh! Mwanamke yule basi ni mzoefu, kama ameweza kukaa hapa na kufanya mauaji bila mtu yeyote hapa kambini kujua ni mzoefu wa hali ya juu,” Sister Mary alisema kwa maskitiko makubwa.
“Sasa atakuwa wapi?” Father Joe aliwauliza wale askari.
“Kwa kweli mpaka sasa hatufahamu amekimbilia wapi, kwa sababu mazingira ya kututoroka yana
utata wa hali ya juu. Inawezekana alishapitia mafunzo fulani ya jeshi, si rahisi mtu wa kawaida akawa na uwezo wa kufanya vile hata kuweza kutembea porini peke yake na kukimbia kwa umbali mrefu.”
“Sasa mtafanya nini?”
“Tutaondoka na picha hii ambayo tutaiweka katika vyombo vya habari, lazima atakamatwa tu.”
“Lakini nina imani kama ni tabia yake ya kurudi kambini basi lazima atarudi na sisi tutawajulisha mara moja,” Father Joe alitoa wazo.
“Mtakuwa mmetusaidia sana.”
Walikubaliana wamuache mtoto Kusekwa ambaye ni mlemavu wa ngozi na kuamua kuendelea kumsaka Ng’wana Bupilipili.
#SASA_ENDELEA...
Ng’wana Bupilipili aliposhtuka, alijikuta amelala kwenye kitanda kilichoashiria kuwa pale ni hospitali. Alijiuliza amefikaje mahali pale, akajikuta akichanganyikiwa. Alipotaka kuamka, mwili wake haukuwa na nguvu na kumfanya arudi kulala kitandani.
Akiwa bado amejilaza na maswali lukuki yakiendelea kupita kichwani kwake, ghafla mlango ulifunguliwa, Ng’wana Bupilipili alifumba macho kwa haraka na kutulia tuli kitandani kusikilizia aliyeingia ni nani.
“Itakuwa amepata nafuu,” ilikuwa ni sauti ya kiume.
“Ni kweli, ilionesha alitumia nguvu nyingi sana pia mwili umepungukiwa maji.”
“Atakuwa anatoka wapi?”
“Hilo swali tumsubiri aamke mwenyewe.”
“Kwa hiyo tumuache alale?”
“Hapana mshitue aamke ili apewe uji wa maziwa na baadaye chakula aweze kupata nguvu, zaidi ya hayo hana tatizo kubwa.”
Baada ya muda, Ng’wana Bupilipili alisikia akitingishwa taratibu huku akiitwa.
“Mama mdogo... mama mdogo.”
“Mmh,” Ng’wana Bupilipili aliitikia kama yupo usingizini.
“Dokta anaamka.”
“Muamshe kabisa kisha fanya nilivyokueleza, mimi nipo ofisini taarifa zingine utaniletea.”
“Sawa dokta.”
Yote Ng’wana Bupilipili aliyasikia na kuamini sehemu aliyokuwepo ni salama kwake. Alipoitwa mara ya pili aliitikia huku akifumbua macho, akakutana na muuguzi mbele yake.
“Pole,” muuguzi alisema kwa sauti ya upole.
“Asante.”
“Unajisikiaje?”
“Mwili hauna nguvu.”
“Basi amka upate uji kisha ule chakula utajisikia vizuri.”
Ngw’ana Bupilipili aliamka kitandani kwa msaada wa muuguzi na kukaa kitako, muuguzi alitembea naye akiwa amempa msaada wa kumshika mkono hadi chumba cha chakula. Alimketisha kwenye kiti na kumletea uji wa maziwa ambao aliunywa wote.
Baada ya kunywa uji, alijikuta akitokwa na jasho jingi, muuguzi aliyejitambulisha kuwa anaitwa Sabina alimuonesha bafuni ambako alienda kujimwagia maji na kupata nguvu. Alirudi naye chumba cha chakula na kumpatia chakula ambacho nacho alikila chote kuonesha alikuwa na njaa kali.
Baada ya kula alirudishwa wodini ili apumzike kabla ya kuonana na mganga mkuu. Baada ya nusu saa, alifuatwa na muuguzi kupelekwa kwa mganga mkuu. Ng’wana Bupilipili aliongozana na yule muuguzi akijua lazima kuna maswali ya kuulizwa juu ya kuwepo pale na mahali alikotokea.
Aliingizwa katika ofisi ambayo haikutofautiana na ya Father Joe, pia mganga mkuu alikuwa Mzungu. Alipowaona wanaingia, aliacha kazi zake na kuwakaribisha.
“Ooh, karibuni.”
“Asante,” alijibu Ng’wana Bupilipili.
“Pole na matatizo.”
“Asante.”
“Unaitwa nani?”
“Malimi,” Ng’wana Bupilipili alidanganya.
“Unatokea wapi?”
“Kijiji cha Sanza.”
“Kijiji cha Sanza mpaka huku umefikaje?”
“Kulitokea vita ya familia ambayo ilifanya wanakijiji tutawanyike na kukimbia kusikojulikana kuokoa maisha yetu.”
“Umetumia muda gani kufika barabara kuu?”
“Siku tatu.”
“Mmh, pole sana.”
“Asante.”
“Una mpango gani?”
“Kwa kweli mpaka sasa sijajua niende wapi hata hapa nimefika sijui ni wapi?”
“Hapa ni Sangema, je, upo tayari kurudi kijijini kwako?”
“Bora nife lakini sipo tayari kurudi huko.”
“Una familia?”
“Yote imeteketea vitani.”
“Pole sana.”
“Asante.”
“Basi mama, sijui unaitwa nani?”
“Baba si nimekueleza naitwa Malimi.”
“Ooh samahani, sasa mama Malimi utaishi hapa kwa vile kituo hiki kinatunza watu wenye shida.”
“Nashukuru baba yangu, asanteni kwa moyo wenu wa kujitolea Mungu awazidishie.”
“Amen.”
“Sabina kamuoneshe chumba apumzike mambo mengine atapangiwa kesho.”
Sabina alimchukua Ng’wana Bupilipili na kwenda kumuonesha chumba cha kupumzika.
#MIAKA_SABA_BAADAYE
Kusekwa aliendelea kukua vizuri akiwa katika kambi aliyoachwa huku akiendelea na masomo ya awali ya chekechea wakati akiandaliwa kwenda shule ya msingi. Kabla hajaanza shule ya msingi, alitokea Mzungu mmoja aliyekuwa akimiliki machimbo ya dhahabu.
Mzungu huyo aliyejulikana kwa jina la John Brown ‘Mr Brown’ alikuwa na mgodi mkubwa uliokuwa na wachimbaji wengi sana. Kutokana na uwezo wake wa kifedha aliweza kuwasaidia wanakijiji waliokuwa jirani na machimbo yale. Alijenga zahanati na
miradi ya maji na umeme ambayo ilikuwa msaada tosha kwa wanakijiji ambao walifaidika na machimbo yake.
Mr Brown ndani ya eneo lake la machimbo alijenga shule kwa ajili ya watoto kuanzia miaka miwili na kuendelea. Sifa zake zilizagaa kila kona ya nchi na kuifanya serikali impunguzie kodi pamoja na kumpa misamaha katika vitu alivyokuwa akiingiza nchini.
Itaendelea...
0 comments:
Post a Comment