WAKALA WA SHETANI -19

Author

#Wakala_wa_Shetani -19-....

NG'WANA Bupilipili alimueleza yote aliyoyafanya baada ya kufiwa na mume wake na ahadi ya kisasi aliyoiweka ya kukisambaratisha Kijiji cha Nyasha.
Siku ile jinsi alivyokamatwa na askari na kufanikiwa kumtoroka. Shoga yake Bupe hakuamini alichoelezwa na Ng'wana Bupilipili na ujasiri aliouonesha wa kutimiza dhamira yake.
#SASA_ENDELEA...

"Mmh, nimekusikia, nakupa hongera, wewe ni mwanamke wa shoka kwa yote uliyofanya. Huna kosa shoga kwani ulichokifanya ni sawasawa, kuwatia adabu mashetani wale.
"Sijui kwa nini hukuniambia na mimi nikusindikize, hata mimi nina kisa changu kizito sikuwahi kukueleza na sababu ya mimi kufika hapa."
"Kisa gani hicho shoga?"
"Kwa vile wewe umeniamini na kunipa siri yako nzito, nami sina budi kujiweka wazi kwako. Mimi nilikuwa nimeolewa katika Kijiji cha Ng'wana Nsimba, Shinyanga vijijini na mume aliyekuwa na mali ya wastani.
"Kwa bahati mbaya mume wangu alifariki, ndugu walinidhulumu mali zote na kuonekana sina thamani mbele ya watu. Kwa kweli roho iliniuma kwa vile tangu nilipoolewa nilikuta ng'ombe ishirini tu, kwa vile sikutaka mume wangu apate shida, katika ng'ombe zangu sabini za mahari nilichukua 40 na kuzichanganya na za mume wangu.
"Kwa miaka minane zizi lilikuwa na ngombe mia nne ishirini. Kwa bahati mbaya mume wangu alifariki, ndugu wakanifukuza kama mbwa, hata nilipoomba ng'ombe zangu 40 walininyima. Sikutaka kubishana nao, niliondoka na kurudi nyumbani na wanangu wawili.
"Nikaapa kuwashikisha adabu japokuwa walinidhihaki na kuniona siwezi kufanya kitu chochote kwa vile waliamini wanawake ni viumbe dhaifu.
"Moyoni nilipanga pigo zito, ndipo siku moja niliwavizia wamelala na kutia moto nyumba zao za nyasi kwa kuanzia milangoni. Kwa vile nyumba nyingi za vijijini za nyasi madirisha yake ni madogo, walikosa pa kutokea, nikaiteketeza familia yote ya marehemu mume wangu.
"Siku ya pili taarifa zilizagaa juu ya vifo vya familia ya mume wangu, sikutaka kuitwa kutoa ushahidi kutokana na kutoa maneno makali siku waliyonidhulumu mali zangu.
"Niliamini mtu wa kwanza nitakuwa mimi, basi nilitoroka bila mtu yeyote kujua na kutembea kwa miguu kwa muda wa siku tatu, usiku nililala na asubuhi niliendelea na safari zangu.
"Ndipo siku moja nilipotokea mbele ya kambi hii nikiwa nimevimba miguu kwa kutembea. Kwa kweli watu wa hapa kwa ukarimu waliniokota na kunitibu kisha walinitunza mpaka leo hii.
"Najua walinitafuta nami nilijificha huku, sijui nitatoka lini kwa vile najua nikionekana kijijini kwetu nina kesi ya mauaji. Basi mdogo wangu matatizo yetu yanafanana na kisasi chetu kinafanana japo wewe ulidhamiria kufyeka kijiji kizima na mimi nilitimiza nadhiri yangu ya kuipoteza familia yote.
"Japo ni dhambi lakini namshukuru Mungu kuniwezesha kulipa kisasi, hata leo nikifa nitakuwa nimekufa bila kinyongo. Kwa kweli sikushangai kwa hatua uliyochukua, kisasi ni hapahapa dunia kwa Mungu hesabu, naamini hata uliowaua umelipa kisasi kwa kiasi kikubwa," Bupe alisema kwa hisia kali zilizomkumbusha donda na maumivu ya moyo.
"Mmh! Umeona dada watu walivyo na roho za kikatili kuliko wanyama? Ni kweli kabisa kisasi duniani kwa Mungu hesabu."
"Umeona eeh!"
"Ila shoga kuna kitu kinanichanganya sana akili yangu."
"Kitu gani tena?"
"Wasiwasi wangu huenda wale askari wakaendesha msako mkali, wakinikosa porini lazima watafika huku. Heri ningekuwa nimewaua wanakijiji tu msako wake usingekuwa mkali lakini nimewaua baadhi ya askari waliopiga mswaki asubuhi kwenye mto ule.
"Hawawezi kukubali kirahisi, lazima watanisaka kwa udi na uvumba, wakinikosa porini watakuja kunitafuta hapa na lazima watanikamata."
"Sasa ulikuwa na wazo gani?"
"Nitoroke."
"Uende wapi?"
"Nitokemee zangu mbele kwa mbele huku nikimlinda mwanangu na wanyama wakali."
"Kwa nini usibakie ili siku wakija ujifiche usijitokeze?"
"Mmh, hiyo itakuwa yamkini, hujui wana ujuzi gani katika kusaka wahalifu, wanaweza kunikamata kama kuku wa mdondo, shoga niache nitokomee zangu Mungu anajua majaliwa yangu na mwanangu."
"Sema tu wasiwasi wako, basi wakipita hao watu urudi sidhani kama watarudi mara mbili."
"Sawa shoga."
"Sasa kwa nini usimuache Kusekwa ili uende peke yako? Si unajua jinsi pori linavyotisha hasa usiku huu."
"Hapana shoga huenda hii ni safari yangu ya mwisho, hivyo siwezi kumuacha mwanangu japokuwa kiza cha nje kinatisha pia hatufahamu tunakwenda wapi. Ila tuombee kwa Mungu atulinde ili tuonane tena."
Je, nini kitafuatia?

0 comments:

Post a Comment