#Wakala_wa_Shetani -20-....
"Hapana shoga huenda hii ni safari yangu ya mwisho, hivyo siwezi kumuacha mwanangu japokuwa kiza cha nje kinatisha pia hatufahamu tunakwenda wapi. Ila tuombee kwa Mungu atulinde ili tuonane tena."
#SASA_ENDELEA...
"Yaani huwezi amini moyo wangu umekuwa mzito kwa nini usiahirishe kuondoka usiku huu, uondoke asubuhi?"
"Hapana shoga, niamuapo kitu siwezi kukisitisha, niache niondoke nitarudi baada ya siku mbili. Nina imani huenda asubuhi ya kesho wakaingia hapa."
"Mmh sawa, nakuombea safari njema na Mungu akutangulie kwa jambo lolote."
"Amen."
Bupe alimuacha Ng'wana Bupilipili apumzike kwa ajili ya safari yake ya usiku wa manane.
***
Baada ya tukio la kushtukiza la vifo vya askari watatu waliokuwa wakilinda na kutoroka kwa mtuhumiwa, jeshi lilijipanga upya kumsaka mtuhumiwa kwa kuagizwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kumsaka muuaji ambaye alionekana ni mzoefu tena mtu hatari.
Baada ya kupatikana silaha na askari wa kutosha, msako mkali ulipangwa kuanza siku ya pili alfajiri kwa kusaka pori lote na maeneo ya karibu. Kila kitu kilikwenda kama kilivyopangwa watu nao walijipanga kwa kuamini adui yao ni mzoefu wa kutumia silaha za moto.
Msako ulianza saa kumi na moja alfajiri wakiwa wamepishana robo saa na muda aliopanga Ng'wana Bupilipili kutoka kambini. Wao walikuwa nyuma kwa nusu saa Ng'wana Bupilipili aliondoka majira ya saa kumi na nusu.
Ng'wana Bupilipili aliondoka kambini majira ya saa kumi na nusu akiwa amembeba mwanaye mgongoni kwa kumfunga madhubuti na kitenge.
Kwa ujasiri mkubwa, aliingia ndani ya pori lenye kiza kinene. Akiwa amejitolea kwa lolote litakalotokea mbele yake, alianza safari yake kwa kupita kwenye mbuga iliyokuwa ikitisha huku milio ya wanyama na wadudu watembeao usiku ikitawala.
Hali ya hewa ilikuwa ya baridi kali lakini hiyo haikumsumbua. Alitembea huku akimuomba Mungu amfikishe salama na kumlinda na vitu vibaya japokuwa hakujua anakwenda wapi usiku mnene kama ule.
Baada ya mwendo wa robo saa wingu zito lilitanda na kuongeza kuimeza nuru ndogo ya nyota na kuongeza hofu kwa Ng'wana Bupilipili.
Alimuomba Mungu amuokoe na mvua ile kwa vile sehemu aliyokuwa akienda hakukuwa na sehemu ya kujikinga asilowane.
Dua yake haikufua dafu kwani baada ya dakika tano mvua nzito ilishuka.
Alijikuta akipata wazo la kurudi kambini, kwani sehemu aliyokuwa akielekea ilikuwa haionekani vizuri kutokana na kiza kizito.
Hakujua ajifiche wapi, alisimama akiwa amemkumbatia mwanaye aliyemtoa mgongoni na kumweka kifuani. Alijikuta yupo kwenye uamuzi mzito.
Mvua iliendelea kuwanyeshea ikiambatana na upepo mkali. Aliamini kabisa kurudi ni kujitia ndani ya kitanzi, akapiga moyo konde na kuamua kuendelea na safari.
Lakini kwa upande mwingine aliona kama ataendelea na safari itakuwa sawa na kuhatarisha maisha ya mwanaye kwa mvua na baridi kali ya usiku huo.
Hakuwa akijua mvua itakatika saa ngapi, hivyo lazima mwanaye angepata matatizo ya baridi ambayo yangemfanya awe katika wakati mgumu wa kumhudumia mtoto pia kujificha na maadui zake.
Alijikuta akipiga moyo konde na kuamua kuendelea na safari yake kwa kuamini haitanyesha muda wote uliobakia kufika asubuhi. Alitembea huku amemkumbatia mwanaye.
Alitembea bila kupumzika kwa zaidi ya saa moja huku mvua ikipungua na kumfanya aendelee na safari yake kwa kuingia ndani ya vidimbwi vya maji bila kujua kwa vile kiza kilikuwa kizito hasa kutokana na wingu zito lililokuwa limetanda.
Baada ya mwendo mfupi alijikuta akipita kwenye njia ambayo ilikuwa na shimo na kumfanya ateleze na kutumbukia kwenye shimo lililokuwa limejaa maji.
Alipiga kelele za woga na kujikuta akizama mpaka chini na mwanaye, alianza kuhangaika ndani ya maji kuokoa maisha yake na ya mwanaye.
Alibahatika kushika mzizi uliokuwa ndani ya maji, kwa nguvu zake zote aliufuata ule mzizi hadi kufanikiwa kutoa kichwa chake nje na cha mwanaye.
Aliung'ang'ania ule mzizi huku akichezesha miguu na kufanikiwa kukanyaga jiwe lililokuwa pembeni ndani ya maji mle shimoni.
Alijisogeza hadi juu ya jiwe na kusimama juu yake. Mikono yake ikiwa bado imeshikilia ule mzizi ambao ulikuwa kama nguzo yake mle ndani ya maji.
Baada ya kusimama ndani ya maji aliweza kujitoa mpaka sehemu za kifua, sehemu iliyobaki ilibakia ndani ya maji. Bado hakuona nje wala kujua urefu wa shimo lile. Alimuomba Mungu amuokoe mwanaye kama kifo basi kimkute yeye.
Je, nini kitafuata
0 comments:
Post a Comment