#Wakala_wa_Shetani - 15.............
Baada ya kusema vile, msaidizi alitoka kumfuata mtoto na kubakia daktari Mzungu ambaye aliendelea kumdodosa mgonjwa.
“Eti mama umetokea sehemu gani?”
“Kabla sijakujibu naomba unieleze hapa ni wapi na nimefikaje?”
SASA ENDELEA...
“Ooh vizuri mama, hapa ni kituo cha watumishi wa kiroho, tupo kwa ajili ya kutoa misaada kwa watu wa maeneo ya karibu kielimu na kiafya. Taarifa zako tumezipata kutoka kwa wasamaria wema waliokuwa wakipita porini na kukuta ukiwa umepoteza fahamu, ilibidi tuwatume vijana wetu ambao walikuchukua na kukuleta hapa.
Baada ya kukufanyia uchunguzi haukuwa na tatizo kubwa zaidi ya njaa na uchovu wa kuonekana umetembea kwa muda mrefu bila kupumzika na pia ulikuwa hajapata chakula cha kutosha, kitu kilichofanya mwili ukose nguvu na kukufanya upoteze fahamu.
Nina imani umenielewa vizuri, una swali lingine?” daktari alimuuliza kwa sauti ya faraja.
“Ooh, asanteni sana Mungu aendelee kuwabariki.”
“Amen, mh! Nini kimekusibu mpaka kuwa katika hali hii?”
Ngw’ana Bupilipili kabla ya kujibu alivuta kumbukumbu jinsi alivyonyanyasika kwa ajili ya kujifungua mtoto albino na kifo cha mumewe huku akishangaa jinsi mwanaye alivyopewa huduma nzuri bila kubaguliwa kwa jinsia au rangi yake.
Bila kutegemea machozi yalianza kumtoka, mdomo ulikuwa mzito kutoa matamshi. Daktari alishtushwa na hali ile na kumfanya aamini lazima yule mama atakuwa na tatizo zito. Kabla hajanyanyua mdomo wake kutamka kitu. Mara mlango ulifunguliwa, akaingia yule msaidizi akiwa amempakatia mtoto.
Ngw’ana Bupilipili alitaka kunyanyuka kitandani baada ya kumuona mwanaye akiwa hai. Baada ya kupewa mwanaye alijikuta akimtazama mara mbilimbili huku akimgeuza kwa kumuangalia kama yupo sawa.
Baada ya kupata uhakika yupo sawa alimnyonyesha, mtoto akalidaka ziwa la mama yake na kunyonya kwa fujo kutokana na njaa kali.
Daktari na msaidizi wake walitabasamu kwa pamoja huku wakifurahia mtoto alivyofurahia ziwa la mama yake. Daktari hakutaka kumsumbua sana, alimwacha amnyonyeshe mtoto na kumuachia maagizo msaidizi wake.
“Pamela, baada ya kumaliza kunyonyesha mgonjwa apewe chakula, apate maji ya kuoga kisha apumzike, jioni nitakuwa na mazungumzo naye, anaonekana ana kitu kizito moyoni mwake.”
“Sawa dokta.”
Daktari alitoka na kumuacha msaidizi wake ameketi kwenye kiti kusubiri amalize kunyonyesha mtoto na kumpa huduma alizopangiwa.
***
Ngw’ana Bupilipili aliishi pale kwenye kituo cha kiroho na mtoto wake ambaye alikutana na watoto wengine wenye ulemavu wa ngozi. Hali ile ilimpa faraja kubwa na kuamini kijijini kwao imani za ushirikina ndizo zilizotawala na kuwafanya kila kukicha wamkosee Mungu.
Pamoja na kukaa pale kwa amani, moyo wake ulikuwa ukiumia kila alivyofikiria kifo cha mumewe na mali walizoziacha kijijini. Alijikuta akiapa lazima alipe kisasi cha kifo cha mumewe na mtoto wao wa kwanza albino aliyeuawa kwa imani za kishirikina.
Kila kukicha alikuwa akibuni njia ya kulipa kisasi kwa wanakijiji waliosababisha yote yale. Siku moja akiwa anafanya usafi kwenye stoo aliona pakiti ndogo iliyokuwa imeanguka chini na kumwaga unga mweupe chini.
Aliiokota na kutafuta sehemu ya kuiweka, wakati huo Sister Lucy alikuwa akiingia stoo na kushtuka kumuona Ngw’ana Bupilipili ameshika pakiti ile tena bila ‘gloves’ mkononi. Alionekana kushtuka sana.
“Mama Kusekwa kwa nini unashika dawa hiyo bila gloves?”
“Nimeikuta hapa chini ndio nilikuwa natafuta sehemu ya kuiweka.”
“Hii ni sumu, ukiiweka mdomoni utakufa dada yangu.”
“Sumu?”
“Eeh.”
“Mungu wangu, kama ni sumu inafanya nini humu ndani?”
“Si sumu kwa maana imetengenezwa kuua watu, ni dawa ya kuua wadudu katika mitaro, mashimo ya maji hata wadudu warukao na watambaao.”
“Sasa inakuwaje unasema sumu kumbe dawa ya kuulia wadudu?”
“Mama Kusekwa, hii ni dawa lakini ukiitia mdomoni inageuka sumu na kukudhuru.”
#Itaendelea
0 comments:
Post a Comment