WAKALA WA SHETANI -14

Author

#Wakala_wa_Shetani -14-.....

Ngw'ana Bupilipili aliposhtuka alijikuta amelala kwenye kitanda cha chuma kilichokuwa kimetandikwa vizuri. Mkononi kulikuwa na mrija wa kuingizia maji mwilini mwake. Alitulia na kutafakari kwa muda huku akipepesa macho. Baada ya akili yake kutulia, aligundua pale ni hospitalini.
#SASA_ENDELEA...

Alishtuka na kuamini mtoto wake anaweza kuwa ameuawa na yeye yupo pale anasubiri kupona ili wanakijiji wakamfungulie mashitaka ya mauaji ya wanakijiji ambao waliuawa na marehemu mumewe.
Aliamini hata kama atajitetea vipi kuwa hakuhusika na mauaji ya wale wanakijiji waliomuua mume wake, bado wasingemwelewa kwa kuamini alishirikiana na mumewe kufanya mauaji.
Alitamani kunyanyuka, ikiwezekana atoroke japo hakujua pale yupo wapi. Alijaribu kujinyanyua alipokuwa amelala lakini mwili nao haukuwa na nguvu, alijirudisha chini na kujilaza. Moyoni hakukubali kushikwa kirahisi namna ile. Lakini bado alikuwa katika kitendawili kizito mwanaye alikuwa wapi.
Alijitahidi kunyanyuka huku moyoni akiapa kupambana na yeyote atakayejitokeza mbele yake. Alijitahidi kujinyanyua na kukaa kitako kisikilizia hali yake.
Wazo lake kubwa ni kutafuta upenyo atoroke hospitalini ili kuikimbia kesi nzito ya mauaji iliyokuwa ikimkabili marehemu mume wake. Kuhusu mwanaye alikuwa amekata tamaa kwa kuamini lazima atakuwa amekwishakufa. Alikaa kitandani mawazo yakiwa mengi huku akivuta pumzi kwa ajili ya kupata nguvu zitakazomfanya atembee peke yake.
Wakati akitaka kuteremka kitandani, alisikia mlango wa chumba alicholala ukifunguliwa. Alirudi kitandani kwa haraka na kujifanya bado hajarudiwa fahamu. Akiwa amefumba macho na kupumua taratibu ili mtu asijue kama ameshaamka, alisikia nyayo za viatu zikisogea alipokuwa amejilaza.
Hakujitikisa, woga ulimjaa na kuanza kutetemeka kwa kuamini wamekuja kumwangalia kama karudiwa na fahamu ili wamkamate. Akiwa bado amefumba macho, alisikia wakizungumza:
"Dokta ina maana hadi sasa atakuwa bado hajarudiwa na fahamu?" Sauti ya kike iliuliza.
"Noo, lazima atakuwa amerudiwa na fahamu, hakuwa na tatizo kubwa, ni njaa na uchovu ndivyo vilivyomfanya awe vile," ilikuwa sauti ya dokta mwenye lafudhi ya kizungu.
"Mbona bado yupo vilevile?"
"Inawezekana kalala, dawa tulizomchanganyia kwenye dripu zina nguvu sana lazima atajisikia vizuri tu, huenda kulala huku ni usingizi na si kupoteza fahamu."
"Sasa dokta kama atapata fahamu ataweza kumnyonyesha mwanaye, maana mtoto yule kila tulichompa amekataa."
Kauli ile ilimshtua Ngw'ana Bupilipili na kuamini kumbe mwanaye bado yupo hai lakini bado alijawa na maswali pale ni wapi na watu wale ni akina nani. Na nini shida yao kwake, lakini kusikia kuwa mwanaye mzima na anahitaji ziwa la mama, aliamini sehemu ile ni salama na kuwa tayari kwa lolote.
Alijipindua na kujifanya kama mtu anayetoka usingizini, kabla hajafumbua macho, alisikia sauti ya kike ikisema.
"Dokta kweli ameamka."
"Hakuwa na tatizo kubwa sana."
"Kwa hiyo dokta?"
"Mpaka sasa hatujajua anatoka wapi na anaelekea wapi, ngoja apate nguvu tutaweza kumuhoji."
Ngw'ana Bupilipili alizidi kutoka mashaka kwa kuamini sehemu ile ni salama ambayo ilimuhifadhi baada ya kumuokota porini. Alifumbua macho na kumuona daktari mzungu aliyekuwa amevaa shati la rangi ya bluu bahari shingoni, alikuwa na kipimo cha mwenendo wa mzunguko wa damu.
Pembeni yake alikuwepo binti mmoja mrembo aliyekuwa ameshikilia faili na kalamu mkononi. Walipomuona amefumbua macho, wote walisogea mpaka kitandani. Daktari alimshika kichwani na kumwambia kwa sauti ya upole.
"Unajisikiaje sasa?"
"Sijambo," alijibu kwa sauti ya chini.
"Pole."
"Asante."
"Unaitwa nani?"
"Salome," alidanganya jina.
"Andika jina hilo," daktari mzungu alimgeukia msaidizi wake na kumweleza aandike jina la mgonjwa.
"Hali ya mwili unaisikiaje?"
"Mmh, uchovu tu na mwili kuishiwa nguvu."
"Okay, nafikiri ukipata chakula utapona kabisa."
"Nitashukuru, mwanangu yupo wapi?"
"Yupo, utaweza kumnyonyesha?" walimuuliza.
"Ndiyo."
"Okay, kamleteni mwanaye."
Baada ya kusema vile, msaidizi alitoka kumfuata mtoto na kubakia daktari mzungu ambaye aliendeleza kumdodosa mgonjwa.
"Eti mama umetokea sehemu gani?"
"Kabla sijakujibu naomba unieleze hapa ni wapi na nimefikaje?"
"Ooh vizuri mama, hapa ni kituo cha watumishi wa kiroho, tupo kwa ajili ya kutoa misaada kwa watu wa maeneo ya karibu kielimu na kiafya.

#Itaendelea

0 comments:

Post a Comment