WATANGAZAJI WA KIKE WANAVYO IPAMBA AZAM MEDIA

Author
Kila kampuni mpya inapotangaza nafasi za kazi, matarajio ni kuwa wanaume wengi ndio watakaoshinda usaili na kuajiriwa, lakini imani hii imekumbana na changamoto kwenye kampuni mpya ya utangazaji ya Azam Media.
Idadi ya watangazaji wa kike wa televisheni walioajiriwa katika mkakati wa kuiboresha Azam TV inaweza kuwa inakwenda sambamba na ya wanaume.
“Niliataka mabadiliko,” anasema Zainab Chondo (30) baada ya kuulizwa ni kitu gani kilimsukuma kuomba ajira Azam TV. “Kwa sababu nilifanya kazi ITV kwa miaka nane, nikaona ni bora niende sehemu nyingine ambapo nitakutana na changamoto mpya, watu wapya na mazingira mapya ya kazi.
“Kwa hiyo Azam tv ilivyoanza nikasema huku panaweza kunifaa nikatuma maombi yakakubaliwa na sasa nipo hapa. Nafurahi kuwa hapa.”
Chondo ni mmoja tu kati ya watangazaji nyota walioona fursa ya kufanya kazi kwenye kampuni hiyo mpya na wakaamua kupambana bila ya kujali changamoto ya idadi ya wanaume zinapotangazwa nafasi adimu kama hizo.
Orodha hiyo ya watangazaji wa kike waliojiunga na Azam TV pia inamjumuisha Fatma Almasi Nyangasa, Yvonna Kamuntu, Rehema Salum na Jane Shirima ambao wameshatambulishwa na kampuni hiyo na tayari wameanza kuruka hewani kwenye vipindi mbalimbali.
Chondo hakupata nafasi hiyo kwa sababu ya jinsi yake, bali uwezo na uzoefu wake katika tasnia ya habari.
Baada ya kumaliza mwaka mmoja katika shahada ya sanaa na habari nchini Uganda, Chondo alipata nafasi ya kufanya kazi Shirika la Utangazaji la Uganda (UBC), lakini mwaka uliofuata neema ikafunguka zaidi na akaajiriwa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akiwa mwaka wa tatu chuoni.
“Tangu nikiwa mdogo nilikuwa napenda sana masuala ya habari. Nakumbuka hata nilipokuwa shuleni nilipenda kujishughulisha na mambo ya habari hadi wenzangu wakawa wananiambia nitakuwa mwanahabari mzuri nikiendelea hivyo,”anasema Chondo ambaye aliwahi kuwa kiongozi mkuu wa shule akiwa mwanafunzi wa sekondari.
Akiwa nchini Uganda wakati yupo chuoni anasema alisoma mwaka wa kwanza na aliopoingia mwaka wa pili alipata kazi ya uandishi katika Shirika la Utangazaji Uganda (UBC).
“Baada ya kumaliza mwaka mmoja hapo nikiwa mwaka wa tatu nilipata kazi tena katika Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC-Swahili) kama mwandishi wa habari wa kawaida.
“Kwa hiyo hadi nahitimu nilikuwa nimefanya kazi na UBC na BBC Swahili, jambo ambalo lilinipatia uzoefu mkubwa na wa kutosha kwani nilijifunza mambo mengi sana kutoka kwao,” anasema Chondo ambaye alianza kuhusudu mambo ya utangazaji tangu akiwa mdogo.
Pengine, mtu ambaye ametofautiana nao kidogo ni Fatma Almasi ambaye alisema kuwa hakuwahi kufikiri kwamba siku moja angekuwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa televisheni.
“Sikuwa mpenzi wa uandishi wa habari. Nakumbuka wakati namwambia baba yangu nataka kuwa mwandishi wa habari akasema hataki, uandishi wa habari,” anasema Fatma ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia yao.
Lakini anasema alifanya bidii kubw akufikia hapo alipo kiasi cha kutafutwa na Azam TV.
“Nilifanya kazi kwa bidii. Nianza kama mwandishi wa mahakamani nikiandika habari za mahakamani. Nakumbuka mkurugenzi wetu wa wakati huo alikuwa na ushirikiano sana kwetu. Alinipa moyo.
“Aliniambia Fatma unaweza, naona jinsi unavyofanya kazi ukiendelea na hizi jitihada utakuwa mwandishi mzuri sana baadaye.”
Hakuna shaka kwamba Nyangasa aliendelea na jitihada hizo na sasa ni mmoja wa watangazaji wazuri nchini.

0 comments:

Post a Comment