MTAMBUE JOHN POMBE MAGUFULI

Author
Mgombea wa urais wa chama cha CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2015 Daktari John Pombe Joseph Magufuli ni mbunge wa jimbo la Chato lililoko mkoa wa Geita na ni waziri wa ujenzi wa Tanzania.
Alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 wilayani Chato Mkoani Kagera.
Kielimu, daktari Magufuli ana Stashahada ya elimu ya sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati.
Mgombea huyo wa urais ana shahada ya umahiri wa Sayansi na shahada ya uzamivu ya kemia.
Aidha daktari Magufuli amewahi kufundisha katika shule ya sekondari Sengerema miaka ya themanini kisha akajiunga na mafunzo ya JKT 

Alizaliwa Oktoba 1959

Alipohitimu, daktari Magufuli na aliaanza kufanya kazi katika kiwanda cha ‘Nyanza Cooperative Union akiwa Mkemia kabla ya kuondoka hapo na kuwania ubunge.
Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995 katika jimbo la Chato na kushinda kisha akateuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa naibu waziri wa Miundombinu.
Katika uchaguzi wa Mwaka wa 2000 pia aligombea ubunge na kushinda na Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa miundombinu.

Alianza siasa mwaka 1995

Katika uchaguzi wa mwaka 2005 daktari Magufuli aligombea ubunge kwa mara ya tatu na kupita bila kupingwa.
Rais Kikwete alimteua kuongoza wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi na baadaye akamhamishia hadi wizara ya Mifugo na uvuvi.
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Miundombinu na ujenzi.
Daktari Magufuli anachukuliwa kuwa ni mwanasiasa mwenye msimamo thabiti, mchapa kazi na asiye yumbishwa au hata kufuata upepo wa kisaisa.

Anatambulika kuwa Mchapa kazi

Watanzaniania wanamkumbuka kwa usimamizi na ujenzi wa barabara na majengo thabiti.
Anakumbukwa kwa kuchukua hatua za kutoa amri za kubomolewa kwa majengo ya kifahari ambayo alihisi yalikiuka sheria za ujenzi.
Na alipokuwa waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Bwana John Magufuli alikwenda hadi bandari ya Dar-es-Salaam na kuizuia meli ya wachina iliyokuwa inashukiwa kufanya uvuvi haramu katika sehemu ya bahari ya Tanzania.

Mbio za ubunge
Dk Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36. Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika.
Mwaka 2005 aliendelea kutupa karata jimboni kwake kuwania ubunge kwa kipindi cha tatu. Akaingia kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Lakini safari hii, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne. Mara hii hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.
Katika uchaguzi ule alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa Chadema. Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.

Nguvu zake kwenye urais

Nguvu ya kwanza ya Magufuli iko katika uwezo wake wa kielimu. Inawezekana kuwa elimu si kila kitu katika siasa, lakini ukweli unabakia kuwa mwanasiasa mwenye elimu ya kutosha akiwa na sifa nyingine za kushika wadhifa fulani, ana nafasi kubwa sana ya kufikiriwa kuliko yule ambaye hana elimu. Katika hili Magufuli amejizatiti na amebobea sana. Elimu ukiichanganya na ujana vinamfanya awe mgombea wa umri ambao ni karata muhimu ndani ya CCM.
Lakini jambo lingine linalompa nguvu, ni kukaa kwa muda mrefu katika wizara zake. Amekuwa Naibu Waziri wa Miundombinu kwa miaka mitano na pia Waziri wa Miundombinu wakati wa Mkapa; akaongoza wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa miaka mitatu kabla ya kuongoza ile ya Uvuvi na Mifugo kwa miaka miwili. Lakini pia tangu mwaka 2010 hadi hivi leo ameiongoza Wizara ya Miundombinu bila kuhamishwa. Jambo hili hulikuti kwa mawaziri wengi sana, hasa katika serikali ya Kikwete.
Jambo la tatu linalompa nguvu ni umakini na na uwezo wa kusoma na kuchambua nyaraka. Watu wanaofanya kazi na Dk Magufuli, kote alikopita wanasema kuwa, tofauti na mawaziri wengi waliowazoea ambao huhitaji kuchambuliwa taarifa hadi zirahisishwe, kwake ni tofauti. Yeye husoma kila jambo na kwamba anatumia muda mwingi sana kusoma kila taarifa na hadi anaweka mistari na michoro kwenye taarifa.
Mhandisi mmoja ambaye amewahi kufungiwa leseni na Magufuli anasema kuwa kosa moja kubwa alilofanya ni kumwandikia Magufuli taarifa ndefu lakini yenye uongo kwenye aya moja. Anasema kuwa aya hiyo ilikuwa iko ukurasa wa 20 lakini ndani ya muda mfupi “Magufuli aliibaini na kibarua chake kiliota nyasi”. Utendaji huu wa kufuatilia hadi vilivyomo kwenye maandishi ndani kabisa, umewashinda wanasiasa na viongozi wengi, Magufuli anabebwa na jambo hilo.
Udhaifu wake
Moja ya udhaifu mkubwa wa Dk Magufuli ni tabia ya “kufanya maamuzi haraka”. Baadhi ya watendaji wa wizara yake wanasema kuwa anafanya maamuzi haraka mno na kuna wakati inaonekana maamuzi yake hayana tija, au ni ya kung’ang’ania tu kwa sababu za kimsimamo. Kuna mambo kadhaa ambayo yamekuwa na madhara makubwa katika wizara alizoziongoza:
Kwa mfano, uamuzi alioufanya wa kukamata meli iliyotuhumiwa kufanya uvuvi haramu na kukiuka sharia, haukuwa na tija kwa taifa kwani baada ya kesi ile kwisha, serikali iliamriwa kulipa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 2.8 pamoja na kurudisha meli husika kwani mahakama ilijiridhisha kuwa ilikuwa inafanya shughuli zake kihalali.
Lakini pia amewahi kufanya mazoezi ya “bomoa bomoa” kwa haraka mno tena kuna wakati bila kuzingatia haki za binadamu za wanaovunjiwa nyumba na makazi yao. Hii, ndiyo sababu Waziri Mkuu Mizengo Pinda, tena akiwa katika ziara ya Wilaya ya Chato alimtaka kutumia nguvu hizo kutumikia wananchi. Baadaye Rais Kikwete alifafanua watu wanaostahili kubomolewa nyumba kuwa ni wale waliofuata barabara na siyo wale wa asili na ambao barabara imewafuata. Kwa hiyo, wale ambao wamefuatwa na barabara wanastahili kulipwa fidia.
Kosa jingine kubwa linalompa Magufuli udhaifu usiomithilika, ni uamuzi na ushiriki wake katika mpango haramu wa uuzaji wa nyumba za serikali ambao ulilalamikiwa sana wakati akiwa Waziri wa Nyumba. Katika nchi ambayo wafanyakazi hawana nyumba na serikali inahitaji sana viwanja katika maeneo maalum, haikutarajiwa uamuzi wa namna ile ungekuwa na tija. Uamuzi ule uliisababishia serikali hasara kubwa na uliacha manung’uniko mengi maana hata wasio wafanyakazi wa serikali, nao walinufaika na nyumba zile.

Dk. John Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 Chato (sasa Mkoa wa Geita).
Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
 
Mwaka 1991 – 1994 alisoma shahada ya uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza.
Mwaka 1985 – 1988 alisoma Shahada ya Kwanza ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemiua na Hisabati. 
 
Mwaka 1981 – 1982: alisoma diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1979 – 1981 alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Juu ya Sekondari Mkwawa, Iringa. 
 
Mwaka 1977 – 1978 alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.
Mwaka 1975 – 1977 alisema Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera. 
 
Mwaka 1967 – 1974 alisoma Shule ya Msingi, Chato.
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma. 
 
Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha. Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma. 
 
Uzoefu wa kazi
-Mwaka 2010 – hadi sasa; Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato. Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato). 
 
Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato). Mwaka 2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki. 
 
Mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki. Mwaka 1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) Mwanza.
 
Mwaka 1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati). 
 
Amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi. Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa. 
 
Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa na ana watoto kadhaa.


0 comments:

Post a Comment