Baada ya jina la Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuteuliwa na
Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuwa mgombea wa Urais katika uchaguzi wa
Oktoba, imebainika mke wake Janeth Magufuli, alikuwa hapendi kuitwa mke
wa waziri.
Janeth anafundisha katika Shule ya Msingi Mbuyuni, Oysterbay jijini
Dar es Salaam, ambayo pia ndiyo iliyomuibua Salma ambaye ni mke wa
Rais Jakaya Kikwete.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Doroth Malecela, katika mahojiano
maalumu, alisema Janeth anayefahamika kwa jina la ‘Mwalimu
Pombe’, amekuwa na maisha ya kipekee kutokana na kutopenda nafasi ya
mumewe kuwa kitambulisho chake na alijaribu kuishi katika mazingira ya
hali ya chini kiasi ambacho hakuweza kutambulika kirahisi kama ni mke wa
Waziri Magufuli.
MAISHA SHULENI
Akiwa shuleni hapo Mwalimu Janeth alifundisha darasa la tano na
masomo aliyomudu vizuri ni Historia, Uraia,Tehama na Haiba ya Michezo.
Malecela alisema kwa ujumla alikuwa akitekeleza wajibu wake bila
kusukumwa, alikuwa mpole, mkarimu na alionyesha ana wito na taaluma
yake.
“Ninaweza kusema ni mwanamke tofauti, alijituma sana na kila siku
alikuwa akiwahi shuleni na kusimamia usafi wa mazingira, kwa mtu kama
yeye ni vigumu kufanya vitu hivyo,” alisema mwalimu Malecela.
MKE WA WAZIRI
Mwalimu Malecela alisema katika muda wote wakifanya kazi pamoja
walikuwa wakiepuka kumuita kwa jina la mke wa waziri kutokana na
kutopenda kuitwa hivyo.
“Ukimuita mke wa waziri alionekana kuchukia na kweli mtagombana,
alitaka aitwe mama Pombe Magufuli, wanafunzi wake alitaka wasijue yeye
ni nani ili aonekane mtu wa hali ya chini kama walivyo wengine,” alisema
Malecela.
Aliongeza: “Unajua mama Pombe muda wote alikuwa anakaa na wanafunzi
akizungumza nao, hivyo hakutaka kujikweza ili kuharibu uhusiano wake na
wanafunzi.”
Alisema jambo lingine linalovutia kwa mama Janeth, ni tabia yake ya
kupenda kula pamoja na wanafunzi wake chini ya mti ulio jirani na
darasa lake kila siku mchana.
“Shule yetu ina mfumo wa kupika chakula cha wanafunzi, yeye
alipenda kula chakula aina ya kande akiwa na wanafunzi wake,” aliongeza
mwalimu mkuu huyo.
Alisema kwa kuonyesha ni jinsi gani hataki maisha ya juu, watoto
wake wote walipitia shuleni hapo na mtoto wa mwisho alimaliza mwaka juzi
na kufaulu Shule ya Sekondari ya Kata ya Oysterbay ambako anaendelea
kusoma.
NI MAHIRI KUIMBA
Kitu kingine ambacho kimetajwa kuwa cha kipekee kwa mama Pombe ni kuwa na uwezo mkubwa wa kutunga, kughani mashahiri.
Kutokana na kipaji hicho shule hiyo ilikuwa ikimtegemea katika
kutunga mashairi na wakati mwingine kughani katika shughuli mbalimbali.
Hata hivyo, mwalimu Janeth ni mahiri wa kutengeneza zana mbalimbali za kufundishia na kujifunzia.
WALIVYOPOKEA UTEUZI
Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Joseph Jonas maarufu kama ‘JJ’
alisema mara waliposikia Waziri Magufuli ameteuliwa kuwa mgombea urais,
walifurahi baada ya kujiona wana bahati kwa shule yao kutoa mke wa Rais
wa Awamu ya Nne na sasa mke wa rais mtarajiwa.
Mke wa Rais Jakaya Kikwete, mama Salma Kikwete kabla ya kuwa katika
nafasi ya 'First Lady' mwaka 2005, alikuwa akifundisha shule hiyo.
“Tulikuwa na furaha na baada ya jina la Magufuli kutajwa kuwa
mshindi, walimu na wazazi tulipigiana simu kujipongeza,” alisema mwalimu
JJ.
Mwanafunzi aliyekuwa akimfundisha, Jane Andrew (12), alisema
umefurahishwa na uteuzi huo, lakini wameumia kuondokewa na mwalimu
mwenye uwezo wa ufundishaji.
Alisema watamkumbuka Mwalimu Janeth kama mama yao kutokana na tabia yake ya kufundisha kwa kuelekeza bila kutumia fimbo.
Frank Peter (11) kwa upande wake alisema atamkumbuka katika somo
lake la michezo kwani amekuwa akifundisha huku mwenyewe akishiriki
kucheza.
“Hakuna mwanafunzi atakayejitokeza na kusema alikuwa haeleweki
alipotufundisha, masomo yake tulikuwa na alama nzuri kwenye mitihani ya
kawaida na kitaifa,” alisema Peter.
0 comments:
Post a Comment