Wazee wa kimila wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai (Malaigwanan)
kutoka Wilaya ya Monduli wamemuomba waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa kubaki na kuendelea kuwa kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa
sababu ndicho kilichomlea na anakijua.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Monduli
kwa niaba ya Malaigwanan, Mzee Joseph Mesopiro kutoka Kata ya Sepeko
wilayani humo alisema viongozi wa mila wanakusudia kutuma ujumbe maalumu
kwa Lowassa kumshauri asihame CCM kama baadhi ya watu aliowaita wapambe
wanavyomshauri.
“Sote Monduli tumesononeka kwa jinsi vikao vya
chama vilivyomtendea mbunge wetu. Bado tunampenda kama ambavyo
tunakipenda chama chetu. Tunaamini ataendelea kubaki CCM na kupigania
ushindi wa chama katika uchaguzi ujao,” alisema Mzee Mesopiro
Alizungumza hayo wakati wa hafla ya kuchukua fomu
na kuomba kuteuliwa na CCM kugombea ubunge Jimbo la Monduli, mwanasiasa
wa siku nyingi Loata Sanare.
Kwa upande wake Laigwanan Julius Laizer kutoka
Kata ya Moita, alisema licha ya mizengwe iliyotawala vikao vya uteuzi
vya CCM vilivyomalizika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na
kusababisha ufa miongoni mwa viongozi na wanachama, bado anaamini chama
hicho kitaendelea kubaki imara hata kama baadhi ya watu watakihama.
“Kama viongozi tuliolelewa na kukuzwa na CCM, tunaamini chama hiki
kitaendelea kuwa imara na hatuko tayari kukubali ushawishi wowote wa
kututaka tuhamie upinzani,” alisema Laizer.
Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Lepurko wilayani
Monduli, Njoput Alami alibeza taarifa za kushawishi watu kuhama CCM kwa
kisingizio Lowassa kukatwa akiziita ni kelele za wapambe wanaohofia
kukosa fursa walizozitarajia iwapo Lowassa angeteuliwa kuwa mgombea wa
CCM.
Akizungumzia taarifa za wanaCCM wilayani Monduli
kughadhabika na kutishia kukihama chama hicho kutokana na Lowassa
kukatwa, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro alikiri baadhi
ya wanachama kuchana kadi na kuchoma bendera za chama hicho, lakini
akasema ni idadi ndogo ikilinganishwa na wanachama waliopo wilayani
humo.
“Kuna taarifa za kadi na bendera za CCM kuchomwa
moto katika baadhi ya maeneo kama Migungani, Mto wa Mbu, Makuyuni na
Nalaarani. Tunaendelea kukusanya taarifa sahihi na kufanya tathmini ya
matukio hayo,” alisema Kimaro.
0 comments:
Post a Comment