Mwaka huu historia ya nchi inatarajia kurejea katika kipindi cha
takriban miaka 20 iliyopita baada ya waliokuwa mawaziri waandamizi
katika serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Profesa Kighoma Malima na
Augustine Mrema, kujiondoa katika chama hicho na kujiunga upinzani.
Malima (marehemu) ambaye ni baba wa Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, alijiondoa CCM mwaka 1995 kama ilivyokuwa kwa Mrema.
Marehemu Malima alikuwa na sifa nyingi zilizomfanya akubalike kwa
watu, miongoni mwa hizo zikiwa ni jinsi alivyokuwa mkarimu, kiongozi
aliyekuwa na hulka ya kuwa karibu na wananchi wa kawaida aliyekuwa na
nguvu ya kupangua, kujibu na kujenga hoja.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Julai 16, 1995 wakati Tanzania ikiingia
katika mfumo wa vyama vingi vya siasa, ndipo Profesa Malima alijiengua
CCM na kujiunga katika chama cha National Reconciliation Alliance (NRA)
na kushiriki mkutano mkubwa wa hadhara mjini Tabora.
Kabla ya kujiondoa kwa Profesa Malima, Februari 1995, Rais
aliyekuwa madarakani, Ali Hassan Mwinyi, alitangaza kumvua uwaziri
aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana na Ajira, Augustine Mrema, kwa
kile kilichoelezwa kama utovu wa nidhamu kwa serikali.
Siku chache baadaye, Mrema alijiunga na chama cha NCCR-Mageuzi na
sababu ya kujiondoa kwake kutoka CCM zikitajwa kuwa ni kukataa kwake
kuwa sehemu ya fungamano la uhalifu ambao hivi sasa ni maarufu kama
ufisadi.
Mrema ambaye hivi sasa ni Mwenyekiti wa Taifa wa Tanzania Labour
Party (TLP), alipinga ndani ya Baraza la Mawaziri la Rais (mstaafu)
Mwinyi kuhusu wizi wa mabilioni ya shilingi yaliyotolewa kwa ajili ya
kufufua zao la mkonge.
Kashfa hiyo ikamhusisha mfanyabiashara maarufu wa wakati
huo,Vidyadhar Girdharlal Chavda aliyetajwa kuwa mnufaika wa kashfa hiyo
hivyo kuwa sehemu ya mabadiliko ya siasa ndani na nje ya Tanzania.
Mrema alifanikiwa kujieleza kwa umma kuhusu sababu zilizomtoa CCM,
akaeleweka, ingawa kwa watawala walijitahidi kuibua propaganda ya kwamba
hatua ya Mrema kujiondoa katika chama hicho ilitokana na uroho wa
madaraka.
EDWARD NGOYAI LOWASSA
Sasa ni dhahiri kwamba aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika
awamu ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa,
anaondoka CCM kujiunga na upinzani, hususani Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema).
Akiwa Chadema, Lowassa atafungamana na vyama vingine vinavyounda
vuguvugu la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambavyo ni Chama cha
Wananchi (CUF), National Convention for Construction and Reform –
Mageuzi (NCCR-Mageuzi) na National League for Democracy (NLD) ambavyo
tayari vimeshatoa tamko la kumkaribisha na kuahidi kumpatia nafasi (bila
shaka ya kuwania Urais).
KWA NINI LOWASSA ANAHAMA CCM?
Inawezekana orodha ya sababu zinazomfanya Lowassa kuihama CCM ni
ndefu kwa kadri anavyoweza kuzielezea yeye mwenyewe, lakini zipo zilizo
katika uhalisia na mazingira yanayoonekana katika siasa za kuelekea
Uchaguzi Mkuu.
Kwanza ni ukweli usiopingika kwamba Lowassa alitumia muda mrefu
kujiandaa kwa ajili ya kushika nafasi kubwa ya uongozi wa nchi hii.
Itakumbukwa kwamba mwaka 1995, Lowassa alikuwa miongoni mwa
wanachama wa CCM waliotia nia ya kutaka kuteuliwa kuwania urais. Akiwa
na Rais Jakaya Kikwete (wakati huo akiwa Waziri wa Fedha), Lowassa na
mshirika wake huyo wa kisiasa wakajulikana zaidi kwa jina la boys two
men (Boyz II Men).
Kwa bahati mbaya, wote wawili yaani Lowassa na Kikwete
hawakuteuliwa kuwania urais, badala yake nafasi hiyo ikachukuliwa na
Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa. Hali hiyo haikuwa mwisho wa
harakati na ushiriki wa siasa kwa wawili hao.
Ndio maana katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2005 ikiwa ni kipindi
cha mwisho wa utawala wa Rais (mstaafu) Mkapa, Lowassa na Kikwete
waliunganisha nguvu zao kisiasa, lakini tofauti na 1995, Lowassa
hakujitokeza kutaka kuwania urais badala yake alimuachia Kikwete
aliyeshinda na kuwa Rais wa awamu ya nne.
Kwa maana nyingine ni sawa na kuamini kwamba Lowassa ‘hakuketi
chini’ na kuachana na nia ya kuliongoza taifa hili tangu 1995.
Alijiandaa na kutenda kazi kwa mfumo uliowafanya wananchi kujenga imani
kwake.
Hata alipokuwa Waziri Mkuu, Lowassa alifikia hatua ya kufanya
maamuzi ambayo baadaye yalisemekana kuwachukiza baadhi ya walio kwenye
utawala akiwamo bosi wake, Rais Kikwete.
Hakuwa na kauli za kusubiri mchakato ama mlolongo wa uchunguzi
unaoligharimu taifa fedha nyingi, bali aliwachukuliwa hatua watumishi wa
umma waliobainika dhahiri kushiriki uzembe wa aina yoyote wenye
kuliathiri taifa ama wananchi.
HANA MATARAJIO YOYOTE KWA CCM
Sababu nyingine inayomfanya Lowassa kuondoka CCM ni kwamba hivi
sasa hana matarajio yoyote kwa CCM. Baada ya kuwa Mbunge wa Monduli
tangu mwaka 1995, Lowassa amefanikiwa kushika nafasi tofauti za utumishi
wa umma ukiwamo Uwaziri Mkuu ambao hata hivyo alidumu kwa kitambo tu,
Desemba 2005 hadi Februari 2008 alipojiuzulu kwa kashfa ya Richmond.
Baada ya chama hicho kumuengua katika kuwania urais mapema mwezi
huu mjini Dodoma, hakuna tarajio lolote la Lowassa katika kuitumikia
nchi akiwa ndani ya CCM. Labda kuendelea kuwa kimya, `akiuguza’ yaliyo
moyoni mwake ikiwamo ndoto ya safari ya matumaini. Nje ya hapo hakuna!
Kutokana na nia yake ya kulitumikia taifa katika nafasi ya Urais
‘kuzimwa’ na CCM baada ya jina lake ‘kukatwa’ katika hatua za awali
kwenye Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, Lowassa alipaswa kufanya uamuzi
wa aina mbili.
Mosi, kuendelea kubaki na dhamira yake huku akiwa mtiifu kwa CCM,
ikibidi kuunga mkono hoja hata kama anaamini kwamba zinaiathiri jamii na
taifa kwa ujumla.
Kama ingekuwa hivyo, Lowassa angejielekeza zaidi katika kulinda
maslahi anayoyapata kupitia kuwapo kwake CCM na kwamba umma na mahitaji
yake visingekuwa vitu vyenye maana na umuhimu kwa maisha yake.
Pili, kujiaminisha kwamba umma na maslahi ya nchi vinapaswa
kutetewa, kulindwa na kuendelewa pasipo kujali mhusika yupo kwenye chama
gani cha siasa.
Sababu hiyo ndio msingi wa kufikia uamuzi wa kujiondoa CCM na
kujiunga Chadema, ili kupata fursa pana ya kujieleza kwa umma, ikibidi
kuonya, kukemea na kukaripia pale watawala wanapotenda kinyume cha
matarajio ya walio wengi.
Lowassa anaweza kutimiza nia hiyo kwa namna tofauti pasipo kujali
kama atawania Urais ama hatapata fursa hiyo kupitia upinzani hususan
Ukawa.
Ushawishi wa Lowassa kwa umma unaendeleo kutoa nafasi kubwa ya
kukubalika kwake kama ilivyokuwa wakati akiwa Waziri Mkuu na hata baada
ya ‘kuachia ngazi’ kutokana na kashfa ya Richmond.
Mathalan, hata alipojiuzulu kutoka nafasi ya Waziri Mkuu, Lowassa
alizidi kuwavutia watu wengi waliomuunga mkono hasa katika harambee za
kuchangia miradi ya maendeleo.
Licha ya kutokuwa Waziri Mkuu, bali Mbunge wa Monduli, Lowassa
alifanikisha kukamilika kwa miradi mbalimbali iliyoasisiwa na taasisi za
kijamii yakiwamo madhehebu ya dini na hatimaye akazidi kuaminika kwa
umma kwamba anafaa kuwa kiongozi wa umma.
Kufanikiwa huko kwa Lowassa kulirejesha historia yake alipokuwa
Waziri Mkuu na katika wizara nyingine ambapo alisimamia miradi mingi ya
maendeleo na ustawi wa watu, ikafanikiwa.
Miradi kama ujenzi wa shule za sekondari za kata na mradi wa maji
kutoka ziwa Victoria kwenda hadi mkoani Shinyanga ni miongoni mwa sehemu
ya udhihirisho wa kazi alizozifanya Lowassa.
UMMA WA WADHAMINI Vipo vielelezo kadhaa vinavyoashiria kuwa nyota
ya Lowassa bado inang’ara na hivyo kuendelea kukubalika kwa wananchi
walio wengi. Hatua hiyo itanufaisha upinzani kwa kufanikiwa kumshawishi
mwanasiasa huyo kujiunga huko.
Mathalani, wakati wa mchakato wa kutafuta wadhamini kwa ajili ya
kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais, Lowassa alipata wafuasi wengi
kiasi cha kuwapo hisia kwamba walinunuliwa ili washiriki mapokezi yake.
Kila mkoa alipokwenda, watu kwa maelfu walifuatilia taarifa zake na
kwenda kumpokea, kisha kumsindikiza hadi alipopata wadhamini na
kuondoka katika mkoa husika. Hali ikawa hivyo kutoka mkoa mmoja hadi
mwingine.
Hata orodha ya wadhamini wake ilipofika zaidi ya 800,000 kutoka 450
waliotakiwa na CCM, ikazidi kudhihirisha namna ambavyo Lowassa
alivyojiandaa na alivyokubalika miongoni mwa wengi kuwa kiongozi mkuu
wan chi.
Lakini hatimaye, kama ilivyonenwa kwenye vitabu vitakatifu, kwamba
jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni, ndivyo
inavyoonekana kwa Lowassa.
Uongozi wa CCM ulimkataa Lowassa kwa kadri ambavyo waashi
walivyolikataa jiwe muhimu, wapinzani wamemchukua Lowassa kama ambavyo
wasiokuwa waashi walivyolichukua jiwe lililokataliwa na kuliweka kuwa
jiwe kuu la pembeni.
0 comments:
Post a Comment