Wakati CCM ikiendelea kupokea msururu wa makada wanaowania
kuteuliwa kugombea urais, vyama vingine vya upinzani vinaendelea na
mchakato wao wa ndani wa uchaguzi, huku Chadema kikijikita katika
uhamasishaji wa uandikishaji wa wapigakura.
Chadema imesema kwa sasa wanaelekeza nguvu katika uandikishaji wa wapigakura ili kutengeneza mazingira mazuri ya ushindi.
Kauli hiyo ya Chadema inakuja zikiwa zimesalia
siku tisa kuelekea siku ya mwisho ya kurudisha fomu kwa watiania wa
ubunge na udiwani katika maeneo yasiyo na uwakilishi wa madiwani na
wabunge.
Mkurugenzi wa mafunzo na uchaguzi wa chama hicho,
Benson Kigaila alilimbia gazeti hili jana kuwa asilimia kubwa ya
watiania kwa sasa wanahamasisha uandikishaji wapiga kura kwa kutumia
teknolojia ya Biometric Voters Registration (BVR) na kwamba, muda
uliobaki unatosha kuchukua na kurudisha fomu.
Mapema Mei, Chadema ilitoa ratiba ya mchakato wa
kutafuta wagombea wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu kwa
kubainisha maeneo yasiyo na madiwani na wabunge kuwa wangewahi kuchukua
fomu kuanzia Mei, 18 hadi Juni, 25 mwaka. “Idadi ya watiania kwa kila
jimbo sio kubwa, kwa kuwa wastani wao ni watu 15 wakati kiwango cha juu
zaidi ni wagombea 30.
“Hakutakuwa na ucheleweshaji wowote, hata malipo ya fomu yanafanywa kupitia benki.”
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema kwa upande wa chama chake, uchaguzi wa ndani unaendelea vizuri
katika ngazi zote na mgombea wa urais ameshachukua fomu anasubiri
kuteuliwa na chama hicho ili aingie kwenye kinyang’anyiro cha Ukawa.
CUF wanaendelea na mchakato wa uchaguzi wa ndani
ambao mwishoni mwa wiki iliyopita Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim
Lipumba alichukua fomu ya kugombea urais wakati hatua za awali za uteuzi
wa wanao gombea ubunge na udiwani zikiendelea kwa Mkoa wa Dar es Salaam
na Zanzibar.
Chama cha ADC, watiania ya kugombea ubunge na
udiwani wanaendelea kuchukua fomu, huku wale wanaotaka kuwania urais
wakitarajiwa kuanza kuchukua na kurejesha fomu kuanzia Julai, 15 hadi
Julai 31 kabla ya vikao vya bodi ya uongozi na mkutano mkuu wa chama
hicho kuketi ili kuteua wagombea.
Naibu Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo alisema
jana kuwa Agosti Mosi hadi 8, watafanya kazi ya kuteua wagombea wa
nafasi za ubunge na urais.
0 comments:
Post a Comment