Fomu za Sumaye nusura zichanwe

Author
Kazi ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye ya kusaka wadhamini juzi nusura iingie dosari baada ya wanachama kutaka kuchana fomu zenye orodha ya wadhamini kwa madai kuwa hawakupewa “nauli” ya kwenda ofisi za CCM kufanya kazi hiyo.
Wakati tafrani hiyo ikitokea mjini Mbeya, Balozi Amina Salum Ali alisema mjini Tanga kuwa hajawahi kuona nchi ambayo mtu anaiba fedha, halafu anaambiwa azirejeshe bila ya kuchukuliwa hatua zozote, akisema huo ni udhaifu mkubwa katika kudhibiti ufisadi.
Katika sakata la Mbeya, kundi la baadhi ya wanachama kutoka kata nne waliokabidhi kadi na kuandikwa majina yao kwenye ofisi za CCM za Wilaya ya Mbeya Mjini, liliambiwa kuwa hakukuwapo na posho kwa ajili ya kazi hiyo.
Kauli hiyo ilisababisha wanachama hao kupora na kutaka kuchana fomu iliyokuwa na majina yao.
Katibu wa CCM wilaya hiyo, Kulwa Milonge alisema tukio hilo lilikuwa kubwa na kuhatarisha usalama, lakini chama kiliingilia kati na kusawazisha mambo.
Milonge alisema hadi mwisho wa tukio hilo, ofisa aliyetumwa na Sumaye kukusanya saini hizo aliondoka na majina 45 ya wadhamini.
Sumaye ni mmoja kati ya wanachama wengi waliojinadi kuwa wanachukia rushwa na ameeleza bayana kuwa iwapo CCM itampitisha mlarushwa, atajiondoa.

0 comments:

Post a Comment