AJALI HIZI ZINAEPUKIKA!

Author

HABARI za leo wapendwa wasomaji. Ni matumaini yangu kuwa Mwenyezi Mungu ameendelea kuwa upande wetu kama ilivyo siku zote. Ni faraja sana kuona kila jambo zuri au baya, limetokea kutokana na karama yake.
Ninapenda kwa mara nyingine, kuchukua fursa hii kuwashauri kuendelea kuamini katika Mungu, kwani kwake yeye, kila jambo linawezekana, tena kwa wepesi wa aina yake.
Baada ya kusema hayo, sasa naomba niende moja kwa moja kwenye mada yetu ya leo. Tumekuwa tukisema mara kwa mara juu ya ajali nyingi zinazotokea kila siku, iwe barabarani au katika vyombo vya majini. Ajali hizi ni nyingi kiasi kwamba zinatia hofu kubwa, hasa zinapohusisha mabasi ya abiria ambazo hupoteza maisha ya watu wengi.
Ingawa tunasema ajali haina kinga, lakini ukweli ni kwamba nyingi za ajali zinazotokea, zinatokana na uzembe ambao kama ungedhibitiwa, zingeweza kuepukika. Uzembe huu upo sehemu nyingi, mwingine ukifanywa na madereva, abiria na zaidi askari wa usalama barabarani.
Madereva ndiyo wanaoongoza kwa kusababisha ajali, kwani wengi wao huendesha vyombo vyao bila kuwa na weledi wa kutosha juu ya kazi wanayoifanya. Wanakimbia kwa kasi zaidi ya ilivyokubaliwa, wanakiuka sheria nyingi za barabarani kiasi kwamba inasikitisha kila siku kusikia juu ya ajali zinavyopoteza maisha ya watu wengi.
Kwa mfano, mabasi yaendayo mikoani yamepangiwa muda wa kufika, kuanzia kituo kimoja hadi kingine. Kwa mfano, basi la abiria liendalo Mwanza, linatakiwa kufika Dodoma tuseme saa sita mchana, lakini madereva hukimbiza sana magari na kujikuta wakiingia mapema, huenda hata saa moja nyuma.
Wanachokifanya ni kusimama sehemu ili kufidia muda au kupunguza mwendo hatua chache kabla ya kufika. Magari yanayofanya mchezo huu yanafahamika, lakini hatua dhidi yao hazichukuliwi.
Lakini wakati mwingine hali inakuwa mbaya zaidi kwa abiria wenyewe kuwalazimisha madereva kuongeza mwendo pale wanapoona gari halikimbii. Humpigia kelele dereva kwa kumuona kama mshamba kwa kuendesha mwendo wa polepole. Huwa tunajimaliza wenyewe bila kujua, ni bora kuchelewa kufika tunakokwenda kuliko kutokufika kabisa.
Halafu tatizo la msingi kabisa lipo kwa ndugu zangu wa usalama barabarani. Kwanza, hawana kabisa utaratibu wa kukagua magari kabla ya kuanza safari, hasa ya mikoani. Magari mengi yanakosa sifa ya kuwepo barabarani kutokana na ubovu, mengine hayana breki, mengine yana matatizo madogo ambayo kadiri yanavyoachwa yaendelee, ndivyo yanavyokuwa hatari kwa usalama wa abiria.
Matrafiki wana tabia ya kuomba na kupokea rushwa. Hii ni tabia ambayo inawafanya madereva kutojali sana sheria kwa sababu wanajua wakienda nyuma ya gari na kuzungumza kikubwa na askari, wataachiwa. Askari hawa wanayajua magari yenye makosa, lakini kwa sababu wanashikishwa kitu kidogo, wanakaa kimya.
Siku hizi kuna hizi wenyewe wanaziita tochi, yaani vifaa ambavyo askari huvitumia kumulika gari linalokuja kwa mbele na kuweza kubaini mwendo wake. Lengo ni kuwataka madereva kutokimbia zaidi ya spidi iliyopangwa. Askari wanatumia vibaya utaratibu huu kwa sababu unawaona wazi kuwa ni watu wenye kuvizia.
Inashangaza sana kuona badala ya askari hawa kukaa barabarani na kuifanya kazi hiyo kwa uwazi, wao hujificha kwenye vichaka na baadaye kujitokeza ghafla na kuwasimamisha madereva wanaokiuka taratibu. Lengo lao ni kuomba rushwa kwa magari yanayoendeshwa kwa kasi.
Inauma sana kuona kila siku ndugu zetu wanapoteza maisha kutokana na rushwa, uzembe na kutowajibika kwa madereva na askari. Ipo haja kwa mamlaka zetu kuangalia upya sheria za usalama barabarani kwa lengo la kuziboresha, ikiwa ni pamoja na kuongeza adhabu, ikiwemo vifungo vya muda mrefu gerezani.
Ajali kama iliyotokea hivi majuzi pale Makongo, jijini Dar es Salaam, ajali ya Mikumi na nyingine nyingi ambazo zimetokea hivi karibuni na kuua ndugu zetuwengi huku wengine wakijeruhiwa vibaya, ni uzembe mkubwa wa madereva wetu.
Suala la usalama barabarani halipaswi kuwa jambo la msimu, tunapaswa kulipa kipaumbele kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

0 comments:

Post a Comment