FAHAMU MIPAKA YA TANZANIA

Author
Image result for TANZANIA
KWA macho ya kawaida unaweza kuhisi suala la kutambua mipaka ya nchi na kuiingiza kwenye Katiba halina umuhimu kwa kuwa mipaka iliwekwa hata kabla ya Tanzania kupata uhuru na inajulikana.
Rasimu yazungumzia mipaka
Sura ya kwanza ibara ya pili inasema kuwa eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanzania bara ikiwa ni pamoja na eneo lake la bahari ambalo kabla ya muungano lilikuwa eneo la Tanganyika. Pili eneo la Zanzibar ni eneo lote la Zanzibar pamoja na eneo lake la bahari ambalo kabla ya muungano lilikuwa likiitwa Jamhuri ya Wa tu wa Zanzibar. Hivi ndivyo mipaka ya Jamhuri ya Muungano ilivyotambulishwa ndani ya rasimu.
Aidha nikumbushie kuwa kabla ya hati ya Muungano ya 1964 nchi hizi zote mbili ambazo zimeunganisha mipaka zilikuwa nchi huru na Jamhuri huru na ndio maana utaona kuwa kila moja kwanza inatambuliwa mipaka yake kabla ya kutaja mipaka ya jumla ya Muungano.
Tanzania haitakuwa ya kwanza Afrika kuingiza mipaka yake katika Katiba. Zipo nchi nyingi ambazo zimekwisha fanya hivyo kwa lengo kuondoa utata na kulinda maslahi ya Taifa kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Baadhi ya nchi hizo ni Kenya, Ethiopia, Uganda, na Sierra leone. Hata nchi changa kama Sudan kusini nayo tayari imekwishaweka mipaka yake bayana katika Katiba.Katiba pendekezwa imeainisha mipaka nane na kuelezwa kila mpaka kama ifuatavyo:
Nchi tunazopakana nazo na chanzo cha kila mpaka ( A )
Kwanza tunapakana na Burundi. Mpaka huu ulitengwa tarehe 5 Agosti 1924 na baadaye kurudiwa tena kwa kuthibitishwa tarehe 2 Novemba 1934. Makubaliano ya mpaka huu yalifanywa rasmi kati ya Serikali ya Uingereza na Serikali ya Ubelgiji. Hawa ndio chanzo cha mpaka huu ambao unatumika mpaka leo.
( B ) Pili, tunapakana na nchi ya Rwanda.Mpaka huu ulitengwa tarehe 22 Novemba 1934.Makubaliano ya mpaka huu yaliingiwa na nchi tatu yaani Uingereza, Ubelgiji na Ireland ya Kaskazini. Hawa ndio chanzo cha mpaka huu unaotumika mpaka leo.
( C ) Tatu, tunapakana na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Mpaka huu ulitengwa tarehe 11 Agosti 1910. Makubaliano ya mpaka huu yaliingiwa na Ujerumani, pamoja na Ubelgiji. Baadaye mpaka ulithibitishwa tarehe 5 Agosti 1934 kati ya Uingereza na Ubelgiji. Hawa ndio chanzo cha mpaka huu unaotumika mpaka leo.
( D ) Nne, tunapakana na Kenya . Mpaka huu ulitengwa tarehe 1 Julai 1890, tarehe 25 Julai 1893, tarehe 14 Februari 1900, tarehe 14 Julai 1914, na tarehe 20 Julai 1922.
Tarehe hizi zimetofautiana kutokana na kila sehemu ya mpaka kuhusisha tarehe yake. Wakati mwingine mpaka huhusisha eneo zaidi ya moja. Hata hivyo makubaliano ya tarehe tofauti za mipaka yote yaliingiwa kati ya Serikali ya Uingereza na Ujerumani. Hawa ndio chanzo cha mipaka hii ambayo inatumika mpaka leo.
( E ) Tano, tunapakana na nchi ya Msumbiji. Mpaka huu ulitengwa tarehe 30 Desemba 1886 na baadaye tarehe 11 Juni 1891. Makubaliano ya mpaka huu yaliingiwa kati ya Ureno na Ujerumani. Hawa ndio chanzo cha mpaka huu unaotumika mpaka leo.
( F ) Sita, tunapakana na nchi ya Uganda. Mpaka ulitengwa tarehe 29 Oktoba na 1 Novemba 1886 baadaye tarehe 1 Julai 1890 na baadaye tena 14 Mei 1910. Mpaka huu kwa vipindi vyote hivi ulikuwa ukitengwa na Ujerumani.
( G ) Saba, tunapakana na nchi ya Zambia . Mpaka huu ulitengwa tarehe 23 Februari 1901 . Makubaliano ya mpaka huu yaliingiwa kati ya Uingereza na Ujerumani.
( H ) Nane, tunapakana na nchi ya Malawi. Mpaka huu ulitengwa tarehe 1 Julai 1890 na 23 Februari 1901 baadaye tarehe 1 Julai 1890 na baadaye tena 11 Novemba 1898. Mpaka huu kwa vipindi vyote hivi ulikuwa ukitengwa na Ujerumani.
Hii ndio mipaka ya nchi yetu ambayo inaingia katika Katiba na mipaka hii iliridhiwa na Serikali ya Tanzania kipindi hicho Tanganyika na imekubaliwa mpaka leo isipokuwa mpaka wa Tanzania na Malawi eneo la Ziwa Nyasa.

0 comments:

Post a Comment