Yanga imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar kwenye mechi iliyopigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati mahasimu wao, Simba wakiendelea kutaabika mbele ya Mgambo Shooting katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Simba ambayo jana iliangukia kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Mgambo
Shooting, zote pamoja na Yanga hazijawahi kuifunga timu hiyo katika
Uwanja wa Mkwakwani tangu ilipopanda daraja misimu miwili iliyopita.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi 34 moja mbele ya
Azam zote zikiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya baadhi ya timu pamoja
na Simba yenye pointi 29 ikiwa nafasi ya tatu.
Taifa
Katika mchezo wa jana, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao la
kuongoza dakika ya saba baada ya mwamuzi Andrew Shamba kuamuru ipigwe
penalti kufuatia Simon Msuva kuchezewa madhambi ndani ya eneo la hatari
ambaye alizamisha kimyani tuta hilo.
Vinara hao wa Ligi Kuu waliendeleza mashambulizi na katika dakika
ya 15 walipata bao la pili kupitia kwa Amissi Tambwe ambaye
aliunganisha pasi ya Mrisho Ngasa aliyewatoka mabeki wa Kagera Sugar.
Dakika ya 35 Kagera Sugar ilimtoa Atupele Green na kumuingiza Adam
Kingwande, wakati kwa upande wa Yanga, Tambwe akimpisha Hussein Javu
ambaye dakika tatu baadaye alimwangusha Atupele Green ndani ya 18
aliyekuwa akielekea kufunga hivyo refa akaamuru litengwe tuta.
Rashid Mandawa aliyekabidhiwa jukumu hilo hakufanya makosa kwa
kuzamisha mpira kimyani hivyo kufanya matokeo kuwa 2-1 dakika ya 38.
Dakika ya 53, Kpah Sherman alikosa bao la wazi baada ya kuzembea
wakati akiwa amebaki na kipa kabla ya beki wa Kagera Sugar Erick Kyaruzi
kuwahi na kuokoa hatari hiyo.
Barthez alifanya kazi ya ziada dakika ya 56 baada ya kuruka na
kupangua shuti la Mandawa na kuikosesha Kagera Sugar nafasi ya kufunga.
Sherman alimpisha Jerry Tegete katika dakika ya 74 ambaye alipata
pasi nzuri ya juu kutoka kwa Ngasa dakika ya 88 lakini mpira wake wa
kichwa haukuwa na macho.
Yanga: Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Oscar Joshua, Rajab
Zahir, Mbuyu Twite, Salum Telela, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Amissi
Tambwe, Kpah Sherman na Mrisho Ngasa.
Kagera: Andrew Ntala, Benjamini Asukile, Salum Kanoni, Ibrahim Job,
Errick Kyaruz, George Kavila, Daud Jumanne, Babu Ali, Rashid Mandawa,
Atupele Green na Paul Ngwai.
Mkwakwani
Katika mechi hiyo, Mgambo Shooting ilianza kwa kasi na kupata kona
ambayo hata hivyo haikuzaa bao kutokana na uimara wa Ivo Mapunda.
Dakika ya 13 Emmanuel Okwi aliumia mguu baada ya kugongana na beki
wa pembeni wa Mgambo, Bashiru Chanacha, hivyo kutibiwa kwa dakika nne
nje ya uwanja kabla ya kurejea dimbani akiwa anachechemea.
Kazi nzuri iliyofanywa na Fully Maganga kwa kuwalamba chenga mabeki
wa Simba kabla ya kumpasia Ally Nassoro aliyeachia shuti kali usawa wa
nyuzi 90 lililomfanya kipa Ivo kuishia kulisindikiza nyavuni kwa macho
katika dakika ya nyongeza (45+1), iliifanya Mgambo Shooting kwenda
mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Hadi mapumziko takwimu zilikuwa zinaonyesha Simba ikiwa na kona
1-1, mashuti 3-4, faulo 10-6, kuotea 1-0, hapakuwa na njano wala
nyekundu kwa timu zote.
Nafasi nzuri kwa Simba katika kipindi cha kwanza zilikuwa katika
dakika ya 16, 23, 36, na 45, lakini washambuliaji wake, Okwi, Ibrahim
Ajibu hawakuwa makini katika umaliziaji huku kipa Godson Mmasa naye
akiwa kikwazo kwao.
Benchi la ufundi la Simba chini ya Mserbia Goran Kopunovic
lilifanya mabadiliko mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa kumtoa Ajibu na
nafasi yake kuchukuliwa na Elias Maguli.
Simba ililazimika kubaki wachezaji 10 uwanjani dakika ya 68 baada
ya Ivo kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na kumshika mguu winga
Azazi Gila ndani ya 18 huku Mgamgo ikizawadiwa penalti ambayo
ilizamishwa kimyani na Malimi Busungu baada ya Manyika Peter aliyeingia
kuchukua nafasi ya Said Ndemla kushindwa kuicheza.
Purukushani za Okwi langoni kwa Mgambo ziliendelea dakika ya 62
wakati huu akigongana na kipa Mmasa ambaye alilazimika kutoka na
kumpisha Said Lubawa baada ya kuumia. Dakika ya 80 Okwi alimpisha Simon
Sserunkuma huku Azizi Gilla wa Mgambo akimpisha Kheri Chacha dakika ya
90, mabadiliko ambayo hayakuwa na madhara pande zote.
Kwa kifupi Simba ilizidiwa hususan kipindi cha pili na kama si
ubora wa Manyika langoni, wangeweza kuumizwa zaidi na mabao kutoka kwa
washambuliaji Busungu, Gilla na Maganga.
Wakati Mserbia Kopunovic wa Simba akiondoka bila kuzungumza na
waandishi mara baada ya mechi hiyo kumalizika, Kocha wa Mgambo Shooting,
Bakar Shime alisema: "Ninawashukuru wachezaji wangu kwa kiasi kikubwa
kufuata maelekezo yangu, niliwaambia Simba ni timu ya kawaida na kweli
wameona."
Mgambo: Godson Mmasa, Bashiru Chanacha, Salim Mlima, Ramadhan
Malim, Salim Kipanga, Mohamed Samata, Malimi Busungu, Ally Nassoro,
Novatus Lufuga, Fully Maganga na Salim Azizi Gilla.
Simba: Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohamed Hussen, Hassan Isihaka,
Juuko Murshid, Jonas Mkude, Abdi Banda, Said Ndemla, Ibrahim Ajibu,
Emmanuel Okwi na Ramadhani Singano 'Messi'.
Sokoine
Kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, jana wenyeji
Mbeya City waliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Stand United, mabao
yakifungwa na Yusuph Abdallah kwa penalti na Paul Nonga.
Pamoja na ushindi huo, bado Mbeya City inaendelea kubaki nafasi ya
pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 20 huku ndugu zao Tanzania Prisons
wakiburuza mkia.
0 comments:
Post a Comment