HARAKATI ZA VIJANA TOKA CHADEMA KWA KUWEKA BENDERA NCHI NZIMA

Author
Nembo ya bendera kwa vyama vya siasa mara nyingi hutumika kutambulisha uwapo wa chama katika eneo fulani na ndiyo ishara kuu ya kuonyesha uimara au uhai wa chama.
 
Ili chama chochote kiweze kushiriki katika chaguzi mbalimbali na kupata ushindi, lazima kuwa hai na hilo ndilo linalosababisha vyama vingi vya siasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, kufanya kila jitihada zinazolenga kufufua chama.
 
Pamoja na jitihada nyingine zikiwamo za kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali ili kuzungumzia kero za wananchi na namna zinavyoweza kupatiwa ufumbuzi, pia vyama hutumia fursa hiyo kusimika bendera hasa katika maeneo wanayoona vinakubalika ili kuthibitisha uhai wa chama.
 
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni miongoni mwa vyama vya siasa vyenye nguvu hapa nchini, ambavyo vimeanzisha mpango wa kusimika bendera katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kujiimarisha.
 
Miongoni mwa maeneo ambayo Chadema kupitia Baraza la vijana wa chama hicho (Bavicha), wamekwishasimika bendera zao ni katika jimbo la Muleba Kaskazini. Na inaelezwa kuwa kazi hiyo itakuwa endelevu mkoani humo na kwingineko nchini.
 
Hadi sasa,bendera hizo zimeshasimikwa katikavituo 14 katika kata za Kamachumu, Ibuga, Bulyakashaju, Ruhanga, Muhutwe , Izigo, Katoke na Kagoma.
 
Mbali na kusimika bendera hizo, viongozi wa Bavicha walifanya mikutano mbalimbali ya hadhara ukiwamo wa Kijiji cha Muyenje katika jimbo la Muleba Kaskazini na Rwamishenye katika Manispaa ya Bukoba.
 
Naibu Katibu Mkuu wa Bavicha Tanzania Bara, Gertrude Ndibalema, akizungumza katika mikutano hiyo ya hadhara anasema usimikaji wa bendera za Chadema pamoja na kuimarisha chama, unalenga pia kuleta chachu ya mabadiliko katika siasa za nchi.
 
Ndibalema anawataka wananchi, hasa wanawake, kutosahau machungu wanayokumbana nayo kutokana na viongozi walioko madarakani kutowajali na kuwataka kusonga mbele katika kuleta mabadiliko ili kupunguza changamoto zinazowakabili.
 
“Wananchi, hasa wanawake, mnapewa zawadi mnapokea… lakini mkipokea mtambue kuwa mtazilipa kwa kukosa huduma bora hospitalini, kupita katika barabara mbovu na watoto wenu kuendelea kusomea kandili,” anasema.
 
Anasema serikali ya CCM, imewaletea wananchi bajaji kwa ajili ya kuwabeba wajawazito wanapokwenda kujifungua na kuhoji namna bajaji hizo zitakavyopita katika mabonde na milima huku zikiwa na wajawazito,  hasa katika maeneo ya vijijini.
 
“Hizi siyo fikira sahihi, leo hii mama akipata ujauzito na baba naye anakuwa mjamzito, maana muda mwingi anafikiria mke wake atajifungua katika mazingira ya namna gani… huduma zilizopo ni za kiwango cha chini mno,” anasema Ndibalema.
 
Anadai hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hajapumzika kwa amani kama ilivyopaswa kwa sababu anawaona aliowaachia nchi wameshindwa kuwatumikia wananchi.
 
Katibu Mwenezi wa Bavicha Tanzania Bara, Edward Simbei anawataka viongozi wa Chadema waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana kuwatumikia wananchi waliowachagua, na kwamba atakayejaribu kwenda kinyume cha matakwa ya wananchi, kamwe hatavumiliwa na chama chao.
 
Simbei anadai kuwa wananchi wengi nchini wamepoteza imani na viongozi walioko madarakani, hasa kutokana na wengi wao (viongozi) kutokuwa na huruma kwa wananchi.
 
“Chadema ina viongozi waadilifu. Kwa hiyo viongozi mliochaguliwa kupitia chama hiki, watumikieni wananchi na kuhakikisha wanapunguziwa kero mbalimbali zinazowakabili,” anasema.
 
Anasema Tanzania imejaa wawekezaji wengi, lakini wananchi walio wengi hawajaona manufaa na kuwapo kwa uwekezaji huo maana badala ya kupata faraja kutokana na kuwapo kwao, baadhi yao wamekuwa wakiwasumbua na kusababisha kuzuka kwa migogoro isiyo na sababu za msingi.
 
“Tumetembea vijijini na kukuta migogoro mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji. Badala ya wananchi kupata amani na uchumi wao kuongezeka kutokana na uwekezaji, sasa imegeuka kuwa kilio kwao,” anasema.
 
Makamu Mwenyekiti wa Bavicha taifa, Patrick Ole Sosopi, 
anawataka wakazi wa mkoa wa Kagera kuwa makini katika kila uchaguzi ili kuepuka kuwapata viongozi wanaojali maslahi yao binafsi badala ya kuutumikia umma.
 
“Wananchi tuungeni mkono katika kulikomboa taifa hili, ambalo hivi sasa wananchi wake wengi wanalia kutokana na kuporwa haki zao,” anasema.
 
Sosopi anasema kuwa kama Kagera wanahitaji kuthibitisha aina ya viongozi ambao wamekuwa wakiwachagua, hasa wabunge, waangalie kinachotokea kila mara yanapofanyika mabadiliko ya baraza la mawaziri.
 
“Kagera, kila likibadilishwa baraza la mawaziri kutokana na tuhuma mbalimbali, watu mliowachagua huwa hawakosi,'' anasema. 
 
 “Huu ni mfano tosha wa kuwaonyesha kuwa baadhi ya viongozi mnaowachagua siyo wawakilishi wazuri…  sasa ni wakati wa kubadilika,” anasema.
 
Akizungumzia hali ya uchumi, Sosopi anasema kuwa hakuna nchi yoyote duniani iliyowahi kupata maendeleo kutokana na michango ya maendeleo, bali nchi hupata maendeleo kutokana na umakini katika kukusanya kodi na kuzitumia vizuri raslimali zilizopo.
 
“Kodi za Watanzania zinaendelea kukusanywa na kugawanywa badala ya kufanya masuala ya maendeleo ya wananchi, matokeo yake serikali inaendelea kuwakamua wananchi hata kwa kidogo walicho nacho, mfano kuwalazimisha wananchi kuchangia michango ya ujenzi wa maabara,” anasema.
 
Sosopi anasema kwa raslimali zilizopo hapa Tanzania, kama zingekuwa zinatumiwa vizuri, serikali ingekuwa na uwezo wa kujenga maabara na miundombinu mingine inayohitajika katika shule za msingi na sekondari, tena bila kuwachangisha wananchi kama ilivyo sasa.
 
“Chadema hatupingi ujenzi wa maabara na wala hatupingi wananchi kuchangia maendeleo yao… tunachokataa ni utaratibu huu inaoutumia serikali wa kuwakamua wananchi wanaopata kwa shida mlo mmoja kwa siku,” anasema.
 
Anasema kuwa hatua hiyo imesababisha baadhi ya watu wasio na uwezo wa kutoa michango hiyo kukimbia familia zao kwa kuhofia kukamatwa na watendaji wa mitaa, vijiji na kata.
 
Wakiwa mkoani Kagera, viongozi hao wa Bavicha taifa walitembelea na kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara katika wilaya za Bukoba, Muleba, Missenyi na Karagwe.

0 comments:

Post a Comment