MIAMBA ya soka nchini, Simba na Yanga leo zinashuka dimbani katika viwanja tofauti kusaka pointi tatu muhimu kwenye mechi za Ligi Kuu bara.
Kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, Yanga itaikaribisha Kagera Sugar wakati Simba itakuwa mgeni wa Mgambo JKT ya Tanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa kwenye uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera Yanga ilichapwa bao 1-0.
Yanga ilicheza mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Simba kwenye uwanja huo ambapo ilichapwa bao 1-0 wakati Kagera Sugar ilitoka na sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mgambo katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga.
Yanga inahitaji kushinda mchezo wa leo kama inataka kurudi na kuwa kinara katika msimamo wa ligi.
Baada ya mchezo wa juzi wa mabingwa watetezi, Azam Fc dhidi ya Ndanda, Yanga wameshushwa na kuwa nafasi ya pili, kwani Azam walipata ushindi wa bao 1-0 na hivyo kuwa kileleni kwa pointi 33 huku Yanga wakiwa na pointi 31.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa nyota wake sita ambapo wanne wanatumikia kadi nyekundu na njano na wawili ni majeruhi. Nyota hao ni Haruna Niyonzima (kadi nyekundu), Kevin Yondani, Dan Mrwanda, Said Juma (kadi za njano) wakati majeruhi ni Nadir Haroub na Andrey Coutinho.
Kwa upande wa Simba wako kwenye muelekeo mzuri wa kuwania taji baada ya kushinda michezo yao mitatu iliyopita dhidi ya Prisons (5-0), Yanga (1-0) na Mtibwa Sugar (1-0).
Timu wanayokutana nayo leo Mgambo JKT wametoka kushinda mabao 3-1 dhidi ya Ndanda Fc na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Kagera Sugar. Ushindi wa mechi tatu mfululizo uliifanya Simba kusogea hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 29.
Iwapo itashinda mchezo wa leo itasogea na kuwa na pointi 32 na kujisogeza karibu na wanaoongoza ligi Azam na Yanga.
Simba haikuwa na mwenendo mzuri kwenye ligi, mara kadhaa imekuwa ikipata tabu kushinda lakini kocha wake Goran Kopunovic alisema wataendeleza ushindi katika mchezo huo kwa ajili ya kuwa katika nafasi nzuri ya kuwania taji.
Mchezo mwingine wa ligi itakuwa ni Mbeya City wakiwakaribisha Stand United ya Shinyanga kwenye uwanja wa Sokoine.
0 comments:
Post a Comment