TUSOME NA KUIELEWA KATIBA MPYA

Author

KATIBA ya nchi ni nyaraka muhimu mno katika Taifa lolote; na ndiyo maana mataifa mengi duniani, yamekuwa yakitumia gharama kubwa kuiboresha.
Kwa Tanzania, kuna mchakato wa kuandika Katiba mpya, unaoendelea kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Mchakato huo ulianza na uanzishaji wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Tume hiyo iliyokuwa na wajumbe kadhaa, ilitoa Rasimu ya Kwanza na ya Pili na kisha kufuatiwa na Bunge Maalumu la Katiba, ambalo lilitoa Katiba Inayopendekezwa, ambayo itapigiwa Kura ya Maoni nchini kote Aprili 30, mwaka huu.
Kwa hivi sasa suala la katiba hiyo, ndilo linalotawala mijadala kwa vyama vya siasa, shuleni, vyuoni, nyumbani, madhehebu ya dini na ofisini.
Kutokana na hali hiyo, tunaunga mkono kauli ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd aliyotoa katika tamasha la kuhamasisha uzalendo, lililofanyika Zanzibar mwishoni mwa wiki.
Balozi Seif aliwataka Watanzania kuisoma na kuielewa Katiba Inayopendekezwa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga Kura za Maoni muda utakapofika.
Anasema Watanzania waisome kwa makini kuona jinsi haki za makundi mbalimbali katika jamii, zimeainishwa na namna watakavyonufaika.
Wananchi wanapaswa wapewe fursa hiyo, kisha wachukue maamuzi wao wenyewe bila kushinikizwa na mtu, watu au kikundi chochote kuhusu kura hiyo ya maoni.
Tunaomba nakala za Katiba Inayopendekezwa, zisambazwe kwa wingi katika taasisi mbalimbali na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu hapa nchini.
Kuna nakala milioni mbili za katiba, zimeshapelekwa katika maeneo mbalimbali, ambapo kila kata nchini itapata nakala 300. Tayari nakala 700,000 zimeanza kugawiwa katika taasisi za kidini, wizara na mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali.
Tunahimiza nakala hizo zisambazwe kwa wingi na kwa haraka na ziwafikie watanzania wote na kila mtu apate fursa ya kusoma katiba hiyo, kabla ya muda wa kuipigia kura kufika.
Tunaomba kila mtu ajitahidi atenge muda wa kusoma nyaraka hiyo, kwa sababu ina mambo mengi yenye manufaa kwa mtu binafsi na Taifa.
Vyombo vya habari, yaani magazeti, redio na televisheni, vina kazi kubwa mno ya kuelimisha wananchi katika muda mfupi uliobaki kuhusu katiba hiyo nzuri, inayompa kila mtu haki na kuleta maendeleo kwa taifa letu.

0 comments:

Post a Comment