Rais Kikwete pia huenda akatolewa nyuzi katika siku tatu zijazo, ikiwa maendeleo yake yataendelea kuwa ya kasi kama ambavyo imekuwa tangu alipofanyiwa upasuaji wa tezi dume Novemba 8, mwaka huu katika Hospitali ya Johns Hopkins, Baltimore, Maryland, Marekani.
Alikutana na kuzungumza na Jaji Othman na ujumbe wake, waliofika kumjulia hali katika Hoteli Maalumu ambako Rais Kikwete anaishi baada ya kutolewa hospitali.
Hoteli hiyo iliyopo Baltimore ina uhusiano wa karibu na Hospitali ya Johns Hopkins. Rais alimhakikishia Jaji Mkuu na ujumbe wake pamoja na Watanzania wote kwa ujumla kwamba hali yake imeimarika na kwamba anachosubiri sasa ni kuondolewa nyuzi katika sehemu aliyofanyiwa upasuaji.
Alisema baada ya kuondolewa nyuzi, ndipo madaktari wake watakapofanya tathmini ya mwisho kabla ya kumruhusu kurejea nyumbani.
Jaji Mkuu amekuwa kiongozi wa kwanza wa kitaifa, kumtembelea Rais Kikwete tangu alipofanyiwa upasuaji. Rais Kikwete alimwambia Jaji Mkuu kuwa sasa afya yake imeimarika zaidi, huku akiendelea kufanya mazoezi kiasi cha mara nne ama tano kwa siku.
Rais aliwakumbusha Watanzania kuhusu umuhimu kwa watu kuwa na utamaduni wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuondoa shaka ya kupata tatizo kubwa kwa kuchelewa kugundua ugonjwa kwa wakati. Alisema kwa upande wake yeye aliwahi kwenda kuchunguzwa na kwamba tatizo liligundulika mapema.
Kuhusu hali yake, Rais alisema masharti ya daktari ni kwamba nyuzi za upasuaji wa tezi dume aliofanyiwa huondolewa siku 12 baada ya kufanyiwa huo upasuaji, na kwamba Novemba 20, 2014 ndiyo siku ambayo amepangiwa kurudi hospitali kufanya hivyo na kama halitaonekana tatizo lolote, ataruhusiwa kurudi nyumbani.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amewashukuru wananchi kwa salamu za upendo za kumtakia nafuu wakati akiwa anaendelea na matitabu yake nchini Marekani, huku akisema ameguswa na kufarijika sana kwa maelfu ya salamu anazopokea kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (SMS) kupitia namba maalumu ya kuwasiliana naye.
Kwa wastani hupokea sms 1,200 kwa siku.
“Kwa kweli nimeguswa, nimefarijika na kutiwa moyo sana, sana kwa salamu za upendo za kunitakia heri nipate nafuu haraka pamoja na dua za wananchi kutoka kila kona ya nchi na kila pembe ya dunia. Sina cha kuwalipa, zaidi ya kusema tafadhalini pokeeni shukurani zangu nyingi sana kwa salamu hizo za upendo,” alisema Rais Kikwete.
Pia, alitoa shukurani nyingi kwa viongozi wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali, ambao nao wamekuwa wakimtumia ujumbe wa kumpa pole kwa njia mbalimbali.






0 comments:
Post a Comment