KIUNGO Jonas Gerald Mkude amesaini Mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba SC na kusema; “Bado nipo sana Msimbazi”.
Akizungumza
baada ya kusaini Mkataba huo mbele ya Waandishi wa Habari, katika
ukumbi wa Silver Pippe, Kawe, Dar es Salaam Mkude amesema kwamba
amesaini klabu hiyo baada ya kufikia kiwango cha fedha alichotaka.
Ingawa
Mkude mwenyewe hakusema ni kiasi gani amepewa, lakini habari ambazo tumezimezipata zinasema kiungo huyo amepewa Sh. Milioni 60, ingawa
mwenyewe alianzia Milioni 80.
“Nafurahi
kusaini Simba SC, klabu ambayo imenikuza kisoka tangu timu ya vijana
chini ya umri wa miaka 20 hadi leo, nawaahidi wana Simba SC kuendelea
kufanya kazi kwa juhudi ili kuiletea mafanikio klabu yangu,”amesema.
Lakini
Mkude hakutaka kuzungumzia kuhusu klabu za Yanga na Azam FC ambazo
ziliripotiwa kumuwania kabla ya kusaini Mkataba huo mpya, alisema;
“Mambo ya mpira unaweza kuangukia popote, nadhani huu si wakati wake
kuzungumzia Azam au Yanga,”.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans
Poppe amesema kwamba wameamua kumuongezea Mkataba mchezaji huyo wa
nafasi ya kiungo cha ulinzi, baada ya kugundua wapinzani wao, Yanga na
Azam walikuwa wanamghasi.
Kapteni huyo wa zamani wa
Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akamtania kidogo Mwenyekiti wa Yanga
SC, Yussuf Manji; “Baada ya sisi kumsaini Okwi (Emmanuel), Manji alisema
anaweza kusajili wachezaji wote wa Simba akawaweka Coco Beach. Sasa
hiyo kauli ndiyo imemkosesha Mkude, kwa sababu yeye hakutaka kwenda
mchangani, alitaka kucheza mpira uwanjani, ndiyo maana amesaini tena
Simba SC,”alisema.
Mkude ni mchezaji
aliyeibuliwa katika mfumo wa soka ya vijana wa Simba SC kabla ya mwaka
wa 2011 kupandishwa kikosi cha kwanza ambako hivi sasa ni tegemeo.
Alikuwa amebakiza miezi sita katika mkataba wake wa awali.






0 comments:
Post a Comment