Lakini zengwe jipya limeibuliwa jana na kuenezwa
kwenye mitandao ya kijamii kwamba Lilian aliyepewa taji hilo baada ya
Sitti Mtemvu ambaye ni mshindi wa awali kujivua taji kutokana tuhuma za
kudanganya umri, si raia wa Tanzania bali ni Mnyarwanda.
Hashim Lundenga ambaye ni Mkurugenzu wa Miss
Tanzania, amekanusha vilivyo na kusisitiza kuwa ni uzushi kwa sababu wao
wanaangalia vyeti vya kuzaliwa ambavyo vinaonyesha uraia wa mshiriki.
Hayo yameibuka siku mbili tangu Lilian kukabidhiwa
taji la Miss Tanzania 2014, lililokuwa likishikiliwa na Sitti Mtemvu
aliyeamua kulivua baada ya kukumbwa na kashfa mbalimbali tangu kutawazwa
kwake Oktoba 11.
Lilian ambaye awali alikamata nafasi ya pili,
alisema: “Sikuwa na kinyongo ukizingatia urembo ni mambo mengi si sura,
ngozi, mwonekano pekee bali unajumuisha mambo mengi, ndiyo maana kipindi
cha usahili huwa kirefu. Binafsi niliamini kwamba (Sitti) alistahili
hasa kutokana na kuwa na vigezo vingi vinavyoonekana kwa macho hata
tulipokuwa kambini, nilikubali matokeo,” alisema Lilian.
Lilian alisema kipindi cha mwezi mmoja tangu
kutolewa kwa matokeo Oktoba 11, anaamini kilikuwa kigumu kwa Sitti, pia
kwake hasa ukizingatia tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili mrembo
huyo aliyetokea katika Kanda ya Temeke.
“Nina maono ya mbali na ninatamani miaka mitano
ijayo niione Tanzania iliyokua hasa katika nyanja ya elimu, napenda
kuona namba ya wanafunzi wanaofaulu ikiwa sawa vijijini na mijini ili
kuwa na taifa lenye watu werevu na wenye maendeleo, hivyo nitajitahidi
kutumia nafasi yangu kusongesha gurudumu hili,” alisema.
Mrembo huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Uganda kwa
shughuli za masuala ya mitindo, alisema anafurahia kupata nafasi hiyo
na anawaahidi Watanzania kuwa atafanya kazi kwa nguvu zote ili
kuhakikisha anatimiza malengo ya waandaaji wa mashindano hayo. Lilian
Kamazima ana miaka 18, alishiriki akitokea Mkoa wa Arusha.






0 comments:
Post a Comment