#Wakala_wa_Shetani -13-.....
"Turudini, muda huu ni mbaya mvua inaweza kushuka si mnakumbuka kuna wingu lilitoweka kiajabu huenda likatuulia mbali. Kwanza sehemu hii haina maeneo ya kujificha na kama mvua itashuka kama ya juzi basi sote tutakufa tunajiona."
SASA ENDELEA...
"Basi turudini, maana tumekwenda sana bado kidogo tutaingia kijiji cha jirani, mnakumbuka wale ni mahasimu wetu wakubwa?"
"Haya jamani turudini, lakini bado nina uhakika tumewaacha nyuma."
"Lazima tutawapata kwani hawana sehemu ya kukimbilia."
Walikubaliana kwa pamoja kugeuza, ilikuwa ni ajabu ya Mungu kushindwa kuuvuka ule mti ambao ndipo alipokuwa wamejilaza Ngw'ana Bupilipili na mwanaye.
Wakati wakijadiliana, Ngw'ana Bupilipili huku akitetemeka, alifumba macho na kumuomba Mungu amuokoe na kikombe kile akiwa amemkumbatia mtoto wake na kuomba asilie. Kwani kama angelia angeharibu kila kitu, wakati akiomba huku amemkumbatia mwanaye alijisaidia haja ndogo.
Aliamini kwa kujisaidia kule lazima mikojo ingemuwasha na kumfanya alie na kutoa sauti na kuharibu kila kitu. Aliuweka mkono mdomoni kwa mtoto wake ili akitaka kutoa sauti basi amzibe.
Aliendelea kumlilia Mungu huku akijikabidhi mikononi mwake. Baada ya maombi yaliyochukua zaidi nusu saa alipofumbua macho hakukuta mtu yeyote. Aliamini kwa mara nyingine tena Mungu amemtendea muujiza.
Siku zote aliamini Mungu hutenda muujiza kwa kila amtegemeaye, watu wale kuishia nyuma ya mti aliokuwa amejilaza ulikuwa muujiza mwingine. Alinyanyuka alipokuwa amejilaza na kumbadili nguo mtoto.
Ajabu kubwa baada ya hali ya utulivu mtoto alianza kulia, kila kitu kilichomtokea kilikuwa kikimuonesha maajabu mengine. Mungu alizidi kudhihirisha uwezo wake kwa kumziba kauli mtoto wakati wa matatizo na kumuachia wakati wa hali ilipokuwa shwari.
Alimnyonyesha mtoto wake mpaka akashiba, baada ya kumaliza kumnyonyesha, naye alifungua mzigo wake na kutoa kipande cha muhogo wa kuchemsha kutokana na njaa kali iliyokuwa ikimuuma.
Baada ya kudanganya tumbo, alijikuta akiwa njia panda asijue aende wapi. Alisimama kwa muda akiwa hajui hatima ya maisha yake ya mbele.
Aliamini kilichokuwa kikifuata mbele yake kilikuwa mtihani mzito kuliko uliokuwa umekwisha muda mfupi wa kuokoka katika kinywa cha mauti. Alijiuliza ataishi wapi, atakula nini na nini hatima ya maisha ya mwanaye?
Kichwa kilikuwa kizito kupata jibu na kujikuta akitokwa na machozi huku akizungumza na Mungu wake amuoneshe njia.
Muda ulizidi kukatika asijue nini hatima yake katika mbuga ile ambayo kila muda ilizidi kutisha.
***
Usiku ulipoingia Ngw'ana Bupilipili na mwanaye walijilaza pembeni ya mti ule mkubwa huku akiendelea kumuomba Mungu asishushe mvua kwa vile hawakuwa na sehemu ya kujikinga, pia awalinde na wanyama wakali wapitao usiku.
Mungu aliwalinda na kulala bila tatizo mpaka asubuhi. Siku ya pili Ngw'ana Bupilipili alijinyanyua toka alipokuwa amelala na kumchukua mwanaye aliyekuwa bado yupo kwenye usingizi. Ilibidi waamke alfajiri kutokana na baridi kali na hali ya hewa bado ilikuwa haijapambazuka vizuri kwa wingu kuwa jeusi.
Alimfunga vizuri mwanaye na kuanza safari ya kuelekea kusikojulikana, alivuka mpaka wa kijiji na kuingia kijiji cha jirani. Aliamini huenda jamaa waliokuwa wakimtafuta wakadamka alfajiri kuanza msako upya na kumkuta, kwa hasira ya kupoteza ndugu zao, lazima wangewaua wote.
Baada ya kuamini mwanaye amekaa vizuri kifuani alianza safari ya kuelekea kusikojulikana. Moyoni aliapa kurudi kijijini alipokimbia kwa ajili ya kulipa kisasi. Alitembea mwendo wa saa saba bila kupumzika huku akikwepana na wanyama wakali kama simba, chui na baadhi ya wanyama waliokuwa katika pori lile la kutisha.
Baada ya mwendo mrefu huku akisumbuliwa na njaa na kiu kikali, alijikuta akiishiwa na nguvu na kuamua kujipumzisha chini ya mti mkubwa. Mtoto wake alianza kulia akionesha njaa inamsumbua. Alitoa titi nje na kumuwekea mtoto mdomoni na yeye kujilaza pembeni yake.
Kila mtoto alivyokuwa akiyavuta maziwa ya mama yake kwa nguvu kutokana na njaa ndivyo naye nguvu zilivyokuwa zikimuishia na kumfanya ahisi kizunguzungu kizito. Kiza kinene kilitanda mbele yake, hakujua chochote kilichoendelea.
***
Ngw'ana Bupilipili aliposhtuka alijikuta amelala kwenye kitanda cha chuma kilichokuwa kimetandikwa vizuri. Mkononi kulikuwa na mrija wa kuingizia maji mwilini mwake. Alitulia na kutafakari kwa muda huku akipepesa macho. Baada ya akili yake kutulia aligundua pale ni hospitali.
Itaendelea
0 comments:
Post a Comment