#Wakala_wa_Shetani -12............
Alijiuliza pori lile atakwenda wapi na maisha yake yatakuwaje? Muda huo wingu zito lilianza kutanda na kufanya eneo lote liwe na giza kuonesha mvua kubwa ingeteremka muda si mrefu. Aliamini kama mvua itateremka lazima mwanaye atakufa kwa vile hakukuwa na sehemu ya kujificha.
SASA ENDELEA...
Kwa uchungu mkubwa alipiga magoti na kunyoosha mikono juu kuomba msamaha wa Mungu.
“Eeh Mungu baba! Wewe ndiye uliyetuumba wanadamu na kutupa haki sawa japo tumezidiana madaraja. Lakini haki ya kuishi ni ya kila kiumbe. “Eeh, Mungu kosa langu nini kuendelea kuniadhibu kiasi hiki? Kama kweli kosa langu ni kuzaa mtoto albino basi Mungu nihukumu kwa hilo, nipo tayari kufa kifo cha aina yoyote kama kweli kosa langu ni kuzaa mtoto albino.
“Lakini naamini viumbe vyote vilivyopo duniani na mbiguni ni vyako wewe na hakuna binadamu aliye juu ya mwenzake bali wewe Mungu wetu peke yako. Eeh, Mungu nimepoteza mwanangu wa kwanza kwa imani za ushirikina bado tena muda mfupi nimepoteza mume wangu.
“Eeh, Mungu! Hebu nihurumie sijui hatima ya maisha yangu, hata uhai wa mwangu upo mashakani, Kwa nini Mungu umeendelea kuwaachia watu waovu waendelee kutenda unyama?
“Mungu umetukataza tusiuane kwa vile kuua ni dhambi, kwa nini umewapa nguvu watu wadhalimu wanaotoa roho za watu bila huruma? Baada ya kifo cha mume wangu sasa unataka kuniua mimi na mwanangu kwa mvua nzito. Narudia kama ni kosa au mkosi kujifungua mtoto albino nipo radhi kufa kifo chochote.
“Mimi ni kiumbe dhaifu nisiye na mamlaka yoyote juu yako, nakabidhi mwili wangu kwako na wa mwanangu ili utuhukumu kwa kosa letu. Lakini siku zote huamini Mungu wewe ni mpole mwenye huruma, hakika utasikia kilio changu na kunipa ulinzi wa milele...Asante Mungu kwa kusikiliza shida zangu, Asante Mungu wewe ni mfariji wa milele asante... asante Bwana wa Majeshi.”
Ngw’ana Bupilipili alifumbua macho taratibu na kukutana na maajabu mbele yake. Wingu lote lilisambaa na hali ya kawaida ilijirudia. Nilipiga tena magoti kumshukuru Mungu kwa kujibu maombi yake kwa muda mfupi. Kisha alimchukua mwanaye aliyekuwa amepitiwa na usingizi alipokuwa amemlaza.
Alimweka mgongoni, wakati akimfunga mtoto kwa mbali aliona kundi kubwa la wanakijiji waliokuwa na marungu, mapanga, mikuki, mishale na upinde wakielekea upande alipokuwa.
Alijua wamekuja kwa shari kuwatafuta, pia aliamini hawakuwa na habari kama Mathayo amekufa.
***
Baada ya kutokea mauaji ya kutisha, taarifa zilizowafikia kijijini ziliwaeleza vijana wote waliotumwa kumkamata Mathayo na mkewe wameuawa. Mbiu ya mgambo ilipigwa, wanakijiji wote walikusanyika na kupewa taarifa za kusikitisha za vifo vya vijana wao saba wa kijiji kile ambao waliuliwa na Mathayo na mkewe kisha kukimbia.
Kilikuwa kilio kizito kijijini pale, liliteuliwa kundi kubwa la wanakijiji na kuingia msituni kumsaka Mathayo na mkewe. Walijiandaa kwa silaha kali huku wakitanguliza vijana mashujaa ambao walitumika katika vita ya kijiji kwa kijiji.
Mke wa Mathayo aliwaona kwa mbali wakija, alijua hali ile lazima ingetokea. Alimfunga vizuri mtoto wake akiamini hata kama angeruka kutoka upande mmoja kwenda mwingine asingemuangusha.
Baada ya kujua mwanaye amekaa vizuri kifuani, naye alikaza nguo zake vizuri na kujifunga furushi la vitu vyake mgongoni. Alianza kuondoka eneo lile na kukimbia zaidi mbele kwa mwendo wa kasi huku akikimbia kwa kuruka mawe na mabonde.
Aliweza kukimbia bila kupumzika kwa mwendo wa saa mbili. Baada kufika katikati ya mbuga akiwa amechoka, alimteremsha mtoto wake na kumlaza pembeni na yeye kujilaza pembeni akiwa hoi. Kutokana na uchovu alipitiwa na usingizi mzito pembeni ya mti mkubwa.
Sauti za watu waliokuwa wakibishana pembeni yake, juu ya kuendelea na kumtafuta, zilimshtua Ngw’ana Bupilipili. Kwa haraka alipeleka macho kwa mwanaye aliyekuwa bado anauchapa usingizi asijue kuwa watoa roho walikuwa karibu yake wakipanga jinsi ya kuuchukua uhai wake.
Watu wale walikuwa wamempa mgongo wakijadiliana, ilionesha kabisa nyuma ya mti aliojilaza mbele yake ilikuwa ndiyo mwisho wao wa kuendelea kumtafuta.
“Jamani tutakwenda mpaka wapi kuwatafuta watu bila kujua wamekimbilia wapi?” sauti ya mwanakijiji mmoja ilisema ambayo haikuwa ngeni kwake.
“Ni kweli maana tunatafuta kama vipofu, huenda tumewapita huko nyuma,” mwingine alichangia.
“Sasa mnashauri tufanye nini?”
“Turudini muda huu ni mbaya mvua inaweza kushuka.”
Je, nini kitafuatia? Usikose
0 comments:
Post a Comment