#Wakala_wa_Shetani -11-......
Alipomkaribia mumewe alishtuka sana baada ya kumwona akiwa kama kaoga mvua ya damu, kila sehemu mwili ulikuwa ukitoka damu, nguo ilikuwa haionekani rangi zaidi ya damu kila kona ya mwili.
Sasa endelea...
Wakati huo, mumewe alikuwa amelala chini huku akitetemeka, machozi yakimtoka kama maji, alimsogelea mumewe na kumwita jina lake.
"Mathayo," hakukuwa na jibu.
"Mume wangu," alimwita kwa sauti huku akimuinamia.
"Na...na..ni? M..m..ke..ke wa..ngu?" Mathayo aliuliza akiwa hawezi kuona kutokana na damu kujaa machoni.
"Ndiyo mimi mume wangu, kulikoni kuwa katika hali hii?" mkewe aliuliza huku akilia kwa uchungu.
"M..m..mke wa..wa..ng..."
"Ni mimi mume wangu."
"Na..na..kufa...mke..wangu."
"Hapana usife mume wangu, nani kafanya hivi?"
"Wa..wa..na..na..ki...ki..jiji."
"Kwa ajili gani?"
"Ya mtoto wetu."
"Mungu wangu! Ndiyo wakufanye hivi?"
"Mm..mm..ke wa..wa..ngu."
"Abee mume wangu."
"Mm..tu..nze mtoto we..wetu...yupo..wa..wapi m..m..to..to?"
"Si atakuumiza mume wangu?" Ng'wana Bupilipili alimuonea huruma mumewe.
"Ha..ha..pana," Ng'wana Bupilipili alimpa mtoto mumewe aliyekuwa amejilaza kwenye mikono ya mke wake huku sehemu aliyoangukia ikitota kwa damu iliyokuwa imeanza kuganda. Baada ya kumpa mtoto alimkumbatia na kutabasamu huku machozi ya uchungu yakimtoka kwa kutengana na familia yake aliyoipenda sana katika maisha yake.
Akiwa amemkumbatia mwanaye ambaye alikuwa ametapakaa damu ya baba yake mwili wote, Mathayo aliacha kutabasamu na kuanza kulia huku akimuomba msamaha mkewe kwa fikra zote mbaya na alichotaka kumfanyia mtoto wao.
"Mm..ke ..wangu ..nisamehe..sa..sana, nilikuwa ..na..na mawazo mabaya ..kwa mtoto...lakini ..naomba unisemehe...m..m..ke wangu..ka..ka..b..b..bla ya kuf..f..f..fa," Mathayo alizungumza kwa shida.
"Huwezi kufa mume wangu Mungu atakusaidia," Ng'wana Bupilipili alilia kwa uchungu huku akiangalia majeraha makubwa yaliyokuwa katika mwili wa mume wake.
Aliamini kupoteza damu kule na majeraha ya visu, mapanga na marungu katika uso wa mumewe kungemsababishia mauti. Pia mdomo haukuwa na meno kutokana na kipigo cha wanakijiji. Alijiuliza ataishi vipi na mtoto yule na wapi atakwenda kuishi kama mumewe atakufa na nini hatima ya yeye na mwanaye?
"M..mm..mke ..wa..wangu," Mathayo aliita kwa shida.
"A..a..be..be..beee," Ngwana Bupilipili aliitikia huku akilia.
"Usilie..mke ...wa..ngu nakufa ..mimi ..la..lakini ...mtoto wetu..sa..salama..mm..mmtu..nze..na..na..na..ku..ku.f.f.f."
Matayo alimshika mkewe mkono kwa nguvu kisha alimuachia taratibu akiwa tayari amekata roho. Ng'wana Bupilipili aliangua kilio cha moyoni kwa kuogopa kupiga kelele ambazo zitawafanya wanakijiji wajue yupo wapi.
Kwa ujasiri mkubwa alimfunga vizuri mtoto wake kisha aliivuta maiti ya mumewe pembeni. Aliokota kipande cha mti na kuanza kuchimba kaburi la mume wake. Kutokana na ardhi kuwa laini, alichimba kwa urahisi kaburi fupi.
Baada ya kuchimba aliuvuta mwili wa mume wake uliokuwa umecharangwa kwa mapanga kama ng'ombe buchani. Kabla ya kuufukia alilia na kuapa kulipa kisasi kwa kifo cha mumewe na mtoto wao wa kwanza aliyeuawa na wanakijiji.
"Mume wangu nakuahidi nami nitakufa kama wewe, kifo chako lazima nilipe kisasi. Kwa hili Mungu atanisamehe. Umekufa katika kipindi kigumu sana maishani mwangu, umeondoka nikiwa bado nakuhitaji sana. Mwenetu Kusekwa alikuwa akihitaji malezi na busara zako. Mume wangu damu yako haitamwagika bure."
Baada ya kulia kwa uchungu alimzika peke yake na mwanaye aliyekuwa mgongoni asiyejua lolote lililokuwa likiendelea wakati ule. Baada ya kumzika, alisali sala ya mwisho na kuelekea juu ya kilima.
Ngw'ana Bupilipili baada ya kufika juu ya kilima alimuweka mtoto wake chini na kuangua kilio cha sauti ya juu kumlilia mume wake huku akiendelea kujiapiza kulipa kisasi kwa njia yoyote ile.
Alimuangalia mtoto wake aliyekuwa amelala huku akinyonya vidole vyake bila kujua nini kilichokuwa kinaendelea. Ndani ya muda mfupi aligeuka yatima baada ya baba yake kuuawa kikatili akimsaidia mwanaye aliyekuwa akiwindwa kutolewa uhai wake.
Alijiuliza pori lile atakwenda wapi na maisha yake yatakuwaje? Muda huo wingu zito lilianza kutanda na kufanya eneo lote liwe na giza kuonesha mvua kubwa ingeteremka muda si mrefu.
Aliamini kama mvua itanyesha lazima mwanaye atakufa kwa vile hakukuwa na sehemu ya kujificha.
Je, nini kitafuatia? Usikose kufuatilia inayofuata
0 comments:
Post a Comment