WAKALA WA SHETANI -10

Author

#Wakala_wa_Shetani -10-.......

Baada ya uchunguzi na kuridhika kuna kila dalili za kuwepo na mtoto mchanga, walimgeukia Mathayo na kumuuliza:
"Hizi nguo za nani?"
"Za mke wangu," alijibu kwa mkato.
"Na hivi vipande vya nguo vya nani?" alionesha vipande vya nepi.
"Sijui," Mathayo alijibu kwa mkato. SASA ENDELEA...

"Sisi hatutaki shari na mtu, hebu tuione mimba ya mkeo kisha tuendelee na mambo mengine, sisi tumetumwa kuna watu wanasubiri majibu, tukirudi tutawajibu nini?"
"Nimeshawaeleza kuwa mambo ya mke wangu ni ya ndani, hayamhusu mtu yoyote kuyajua, kama mtoto akizaliwa mtamuona tu wala hamtamtafuta kama jambazi."
"Jamani hatukuja kufanya mjadala wa albino au kumtafuta, tusipoteze muda. Tumwekeni chini ya ulinzi ili aseme mkewe yupo wapi," mmoja aliyekuwa hana subira aliingilia kati baada ya kuona Mathayo hataki kuonesha ushirikiano.

Walipotaka kumweka chini ya ulinzi, Mathayo hakukubali kushikwa kirahisi. Hapo ndipo ugomvi mzito ulipoanza. Ikawa piga nikupige, Mathayo katika ugomvi ule alijikuta akimkumbuka mtoto wake wa kwanza albino aliyeuawa na wanakijiji na kujikuta akipandisha mori ya ugomvi.
Wanakijiji walimshambulia Mathayo kwa marungu na mapanga, naye alikuwa na ubavu wa kupigana hivyo alikabiliana nao vilivyo. Baada ya kuzidi kujeruhiwa na kumwaga damu nyingi, alikumbuka silaha yake shambani.

Alitimua mbio kuelekea shambani, vijana wale nao hawakumuacha walimkimbiza. Alipofika shambani alichukua silaha yake. Kwa vile alijua uhai wake upo mikononi mwake, alijibu mashambulizi. Damu ikawa inamwagika ovyo, kila mmoja alitetea uhai wake kwani vita ilikuwa kubwa. Kila mmoja alipigania roho yake.
Japokuwa Mathayo alikuwa peke yake lakini aliweza kupigana kwa nguvu zake zote kutetea uhai wake. Pamoja na kipigo alichokipata kuwa kizito kwa kupasuliwa sehemu kubwa ya mwili wake, bado aliendelea kutetea uhai wake kwa nguvu zake zote mpaka tone la mwisho la damu yake.

Hakukubali kufa kikondoo, alipigana kwa uzoefu, alikuwa ni mmoja wa wapiganaji waliokuwa wakitegemewa na kijiji wakati wa kupambana na wezi wa ng'ombe. Aliweza kuwamaliza vijana wote kwa panga lake. Pamoja na kuwamaliza wote, hali yake ilikuwa mbaya sana kutokana na kupata majeraha mengi na kupoteza damu nyingi.

Alijaribu kutembea kumfuata mkewe, lakini alishindwa kutokana na kusikia kizunguzungu kikali kilichosababishwa na kutokwa na damu nyingi kwenye majeraha mazito ya visu, mapanga na marungu aliyopigwa na wanakijiji wenzake.
Mathayo alitembea kama mlevi, mwili wote ukiwa umemjaa damu kama alikuwa akiogelea kwenye dimbwi la damu.
Aliyaona mauti mbele yake yakimuomba kumpa msaada wa kumfikisha ahera. Lakini hakuwa tayari kuiacha dunia na mwanaye kipenzi ambaye mapenzi ya dhati yalikuja muda mfupi kabla ya kifo chake.

Alijifikiria mkewe atabaki katika hali gani, mwanaye naye maisha yake yatakuwa katika hali gani kama yeye akifa. Aliamini bora yeye angekufa kwa kipigo kile lakini alihisi hata akifa bado maisha ya mwanaye yapo hatarini. Ilikuwa lazima mkewe angetafutwa na kuuawa kama walivyomfanya yeye pamoja na mtoto wao kipenzi ambaye mpaka muda ule alikuwa hajapewa jina.
Moyo ulimuuma sana, alijitahidi kunyanyuka alipokuwa ameanguka na kuanza kutembea kwa magoti kwani miguu haikuwa na nguvu ya kusimama.
Hakukubali, alijitahidi kutembea kwa shida kwa kujilazimisha kufuata njia aliyokimbilia mkewe. Kila hatua macho yalipunguza nguvu ya kuona kwa mbali, ilikuwa kama kibatari kilichoishiwa mafuta kilichokuwa kinataka kuzimika.

Dunia aliiona ikizunguka, kila hatua mbili alianguka chini. Kiza kinene kilizidi kutanda mbele yake, alipoanguka hakuweza kunyanyuka tena.
Mkewe Ngw'ana Bupilipili alikuwa amefanikiwa kukimbia na kwenda kujificha juu kilima kimoja. Sehemu aliyojificha aliamini mtu akitokea kwa mbali lazima angemuona.
Akiwa amepumzika baada ya kutembea umbali mrefu na kumfanya pumzi zimjae kifuani na kukaa chini huku akitweta, kwa mbali alimwona mtu kama mumewe akija huku akipepesuka na kila hatua mbili alianguka chini.

Baada ya muda alimuona akidondoka chini na hakuweza kunyanyuka tena. Alisubiri labda atanyanyuka lakini ilionesha hawezi tena.
Kitendo kile kilimpa nguvu na kujikuta akimpitia mwanaye huku akijisemea; ‘liwalo na liwe.' Alimfunga mwanaye kwapani na kuteremka kumfuata mumewe ili kutaka kujua amepatwa na masaibu gani.

Alikwenda kwa mwendo wa kukimbia bila kuangalia hata chini, kuna wakati alianguka na kugaagaa na mwanaye, hilo hakuliona zaidi ya kumkimbilia mumewe ili ajue anakumbwa na nini.
Alipomkaribia mumewe, alishtuka sana baada ya kumwona akiwa kama kaoga mvua ya damu, kila kona mwili ulikuwa ukitoka damu, nguo ilikuwa haionekani rangi zaidi ya damu kila sehemu.

Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia

0 comments:

Post a Comment