WAKALA WA SHETANI -09

Author

#Wakala_wa_Shetani -9-........

Wakati mkewe akiondoka eneo lile, Mathayo alitoka nje ya pango lile kuondoa ushahidi huku akimuomba Mungu mkewe azidi kukimbia na kumuokoa mtoto wao. Alijikuta akipata ujasiri wa ajabu na kuwa tayari kufa kuliko kumpoteza mtoto wake.
SASA ENDELEA...

Kilichompa ujasiri kilikuwa kitu kimoja, matukio ya athari za mvua. Katika mvua ile sehemu nyingi zilizoharibika pamoja na mifugo kufa zilikuwa za majirani zao, lakini kwao palikuwa salama kama mvua ilipita ilinyesha kidogo. Hata uharibifu katika mashamba, shamba lao ndilo pekee lililosalimika.

Mawazo yake yalibadilika na kuamini mtoto wao si mkosi kama alivyofikiria.
Aliamini kama mtoto wao angekuwa mkosi basi balaa kubwa lingewakumba wao kuliko wanakijiji wenzao. Ilikuwa ajabu kubwa asilimia kubwa ya wananchi wa kijiji kile walipata matatizo ya kubomokewa nyumba na kuezuliwa paa. Kwao kulikuwa salama katika nyumba na mifugo hakuna uliokufa hata mmoja.

Kwa majirani zao ilikuwa kilio cha kusaga meno, mvua iliwatia hasara kubwa na hakuna hata mmoja aliyepona katika mvua ile ambayo iliacha simulizi kijijini pale.
Ajabu nyingine, mvua ile haikuua mtu hata mmoja zaidi ya kufanya uharibifu na hasara kubwa. Mathayo akiwa bado yupo nje ya pango kuangalia hali ya usalama huku akiomba kimoyomoyo mkewe asionekane, vijana wa kijiji walifika na kumuuliza.
"Mkeo yupo wapi?"

"Mke wangu wa nini? Na imeanza lini kuuliziana wake zetu?" Mathayo alikuwa mkali na hakutaka kutoa ushirikiano.
"Bado hujatujibu, mkeo yupo wapi?" Mmoja ya vijana wale alimuuliza kwa sauti kali.
"Sijui," Mathayo alijibu kwa mkato.
"Unajitia kiburi sio?" walimuuliza kwa sauti ya kitisho.

"Najitia kiburi ili iweje?" Mathayo bado hakutikiswa na kauli za vijana wale.
"Jamani kwa nini tunamchelewesha," mmoja alisema huku akitaka kumsukuma Mathayo.
"Jamani tuwe wapole, hili jambo hatujawa na uhakika nalo," mmoja alitaka watumie busara kuliko nguvu.
"Basi atujibu mke wake yupo wapi?"

"Kabla sijawajibu hii imeanza lini na leo iwe mara ya pili?" Mathayo bado alisimamia msimamo wake.
"Sikiliza Mathayo, mkeo alikuwa mjamzito na taarifa zilizotufikia ni kuwa ameshajifungua lakini mtoto wenu inasemekana mnamficha. Wasiwasi wa wanakijiji huenda ni albino na ndiye aliyesababisha balaa kubwa kijijini kwetu, hivyo tulikuwa tunataka tumuone ili tupate uhakika kwa kile kinachosemwa," mmoja aliyeonekana mwenye busara alisema kwa upole.

"Basi kwa taarifa yenu mke wangu bado hajajifungua na sijui nani aliyewadanganya kuwa mke wangu kajifungua."
"Bwana Mathayo, huu tunaoonesha hapa ni ustaarabu, lakini tunajua yote, hata jana usiku jinsi mlivyokuwa mkiongea baada ya mtoto wenu kulia na kushauriana jinsi ya sauti ilivyofika mbali.

"Sasa ndugu yangu hatukuja kupigana bali kuelewana, kwanza wewe ni kiongozi wa usalama kijijini, kwa nini tugombane kwa jambo la kuelewana? Tuoneshe huyo mtoto ili tumuone kama ni albino au la," kijana aliyeonekana ana busara alisema huku akiendelea kumbembeleza Mathayo.
"Nimewaambia mke wangu hajajifungua labda mlisikia nyumba ya jirani si kwangu," Mathayo bado alikuwa mbishi.
"Sawa nyumba ya jirani mke wako yupo wapi?"

"Suala la mke wangu haliwahusu, mke wangu ananihusu mimi na si mwingine."
"Sikiliza Mathayo, wewe si mgeni wa kijiji hiki, pia hata wewe ni kamanda wa baraza la usalama la kijiji. Unajua kabisa mtu anaposhukiwa na kitu lazima apekuliwe, lakini wewe tunakufanyia ustaarabu basi tuoneshe ushirikiano," hawakuchoka kumbembeleza.

"Si kwangu, napenda maisha yangu niishi nipendavyo mwenyewe na si kuingiliwa na mtu."
"Jamani tunamchelewesha," mmoja uzalendo ulimshinda.
Alijitokeza na kusukuma kifuani kwa nguvu na kumfanya Mathayo kudondoka chini na kufikia jiwe. Bila huruma walimpita na kuingia pangoni na kufanikiwa kuzikuta nguo za kike na vipande vya kanga kuonesha ni za mtoto mchanga.
Baada ya uchunguzi na kuridhika kuna kila dalili za kuwepo kwa mtoto mchanga, walimgeukia Mathayo na kumuuliza:

"Hizi nguo za nani?"
"Za mke wangu," alijibu kwa mkato.
"Na hivi vipande vya nguo vya nani?" alionesha vipande vya nepi.
"Sivijui," Mathayo alijibu kwa mkato.

Je, nini kitafuatia? Usikose

0 comments:

Post a Comment