#Wakala_wa_Shetani -24-...
Wale askari waliokuwa wakicheza karata walinyanyuka na kwenda hadi ndani ambako walikuta patupu. Walijikuta wakichanganyikiwa na kuanza msako kuzunguka hema lakini hakukuwa na mtu yoyote eneo hilo.
Walijikuta wakipagawa na kujiuliza watamwambia nini mkuu wao aliyewapa jukumu la kumlinda mwanamke huyo aliyeonekana dhaifu mbele ya macho ya watu lakini ni hatari kwa vitendo.
#SASA_ENDELEA...
Waliotumwa walirudisha taarifa za kutoweka kwa Ng'wana Bupilipili na kumtelekeza mtoto. Sherehe yote ya kumpata mtuhumiwa iliyeyuka na kuamuliwa ufanywe msako wa haraka. Kila askari alitawanyika kwenda anapopajua ili mradi arudi na mtuhumiwa.
Askari wote walitawanyika huku waliofanya makosa ya kizembe wakichanganyikiwa zaidi kwa kukimbia ovyo bila kujua wanakwenda wapi.
Askari wengine walibakia pamoja na mkuu wao kwa ajili ya kulinda usalama wa mtoto.
Msako ulifanyika mpaka usiku wa manane lakini hawakupata chochote, mkuu wa oparesheni ile aliwaeleza waliofanya uzembe wahakikishe
mtuhumiwa anapatikana la sivyo wasirudi. Hawakupata muda wa kupumzika, walirudi kufanya msako.
Waliona hawawezi kukaa na yule mtoto aliyeanza kumlilia mama yake. Kwa vile kituo cha kulea watu wanaoishi katika mazingira magumu kilikuwa
karibu, siku ya pili walimchukua na kumpeleka katika kituo kile. Walipofika mkuu wa kikosi cha kumsaka muuaji alijitambulisha kwa Father Joe, baada ya kujitambulisha walimueleza sababu ya kuwepo pale.
Father alikubali kumpokea mtoto yule na kumlea, lakini alishangaa kumuona ni mtoto wanayemfahamu.
"Ha! Huyu mtoto si wa hapahapa kambini?"
"Hapana Father huyu tumemuokota porini na mama yake," alijibu mkuu wa oparesheni.
"Huyu wa hapahapa kambini na mama yake anakaa hapahapa, jina lake anaitwa Kusekwa."
"Hapana huyu mama yake ni muuaji tena amekimbia baada ya kumkamata na kumtelekeza huyu mtoto," mkuu wa oparesheni alizidi kubisha.
"Hapana, mama yake ni mkimbizi wa Kijiji cha Nyasa, si muuaji," Father Joe alimtetea Ng'wana Bupilipili.
"Father hebu tuitie huyo mwanamke tumuone na amtambue mtoto wake," mkuu wa oparesheni alimuomba Father Joe.
Father Joe alinyanyua simu na kumwita sister mmoja, baada ya muda mfupi Sister Mary aliingia.
"Sister Mary naomba uniitie Ng'wana Bupilipili."
"Sawa Father," sister aligeuka na kuondoka.
Baada ya muda alirudi akiwa peke yake.
"Vipi yupo wapi?"
"Hayupo father."
"Atakuwa amekwenda wapi?"
"Kwa kweli jirani zake hawana taarifa zozote mpaka jana usiku wanakwenda kulala walikuwa wote."
"Chumba chake kina vitu vyake?"
"Ngoja nikahakikishe," sister alisema huku akiondoka.
Sister alitoka tena na kwenda chumba cha Ng'wana Bupilipili ambako hakukuwa na mabadiliko yoyote. Alirudi na kutoa taarifa, baada ya kusikia vile mkuu wa oparesheni aliuliza.
"Kwani huyo mnayemsema mnayo picha yake?"
"Ndiyo."
"Basi tupeni tuiangalie kama siyo yeye tuondoke tukaendelee na msako wetu."
Father Joe alifunua faili lililokuwa na picha za watu wote waliokuwa kwenye kambi ile. Alichambua picha mojamoja kwa umakini mpaka akaipata picha ya Ng'wana Bupilipili.
"Picha yake hii hapa," Father Joe alisema huku akiwakabidhi.
Waliichukua ile picha na kuitazama kwa muda na kugundua kumbe mbaya wao hakuwa akikaa porini kama alivyojinadi bali alikuwa anakaa kwenye kambi ile.
"Father ndiye huyu!"
"Mna uhakika?" Father Joe aliuliza macho yakiwa yamemtoka pima.
"Kwa asilimia mia moja."
"Mmh! Mnataka kuniambia huyu mwanamke ni muuaji?" father alishtuka.
"Ndiyo father, ameua watu wengi Kijiji cha Nyasha na askari wenzetu wawili."
"Lakini si ndiyo kijiji alichokuwa akiishia zamani kabla ya kukimbia kuokoa maisha ya mwanaye huyu mlemavu wa ngozi na kujikuta akimpoteza mumewe aliyeuawa na wanakijiji na kufanikiwa kukimbilia hapa tulipowahifadhi siku zote za maisha yao?"
"Ni kweli father, maelezo yako na ya huyo mwanamke yapo sawa, aliahidi mbele yangu kuwa analipa kisasi na kama asiponyongwa baada ya
kumkamata, atahakikisha Kijiji cha Nyasha kinabakia historia, atakifagia chote," alisema askari aliyemkamata Ng'wana Bupilipili.
"Mmh, kumbe ndiyo hivyo, mbona mimi nilikuwa sijui!" father alishtuka huku Sister Mary naye akisikia habari ya kumshangaza.
"Basi father yule mwanamke ni zaidi ya gaidi, ameua watu wengi kwa sumu ya dawa ya kuulia wadudu katika maji."
"Dawa ya kuua wadudu ni dawa gani hiyo?"
"Kwa kauli yao nakubaliana nao, Ng'wana Bupilipili anahusika, chumbani kwake chini ya godoro nimeikuta hiyo dawa zaidi ya paketi tatu," Sister Mary aliwaunga mkono.
"Mmh, kama ni hivyo yule mwanamke ni mbaya sana, nilikaa naye na kumueleza awasamehe na kumuachia Mungu na kunikubalia. Kumbe alikuwa na siri yake nzito moyoni ambayo sote humu ndani tulikuwa hatujui," Father Joe alisema kwa masikitiko.
"Kwa kuonesha huyu mwanamke ni mzoefu hii ni mara ya pili tunamkamata na kutoroka juzi tulimkamata lakini alifanikiwa kututoroka."
"Mmh, sasa napata picha inawezekana siku hiyo ndiyo aliyokimbia na kuangukia mlango wa kuingilia getini na kudanganya alikimbizwa na mnyama mkali," Father alitoa ushuhuda.
"Kwa usemi huo ni kweli kabisa, mmh! Mwanamke yule basi ni mzoefu kama ameweza kukaa hapa na kufanya mauaji bila mtu yeyote hapa kambini kujua ni mzoefu wa hali ya juu," Sister Mary alisema kwa masikitiko makubwa.
"Sasa atakuwa wapi?" Father Joe aliwauliza wale askari.
"Kwa kweli mpaka sasa hatufahamu kakimbilia wapi, kwa sababu mazingira ya kututoroka ni ya hali ya juu. Inawezekana alishapitia mafunzo fulani ya jeshi, si rahisi mtu wa kawaida akawa na uwezo wa kufanya vile hata kuweza kutembea porini peke yake na kukimbia kwa umbali mrefu."
"Sasa mtafanya nini?"
"Tutaondoka na picha hii ambayo tutaiweka katika vyombo vya habari, lazima atakamatwa tu."
"Lakini nina imani kama ni tabia yake ya kurudi kambini basi lazima atarudi na sisi tutawajulisha mara moja," Father Joe alitoa wazo.
"Mtatusaidia sana."
Walikubaliana wamuache mtoto Kusekwa ambaye ni mlemavu wa ngozi na kuamua kuendelea kumsaka Ng'wana Bupilipili.
Je, nini kitaendelea? Fuatilia...
0 comments:
Post a Comment