WAKALA WA SHETANI

Author

#Wakala_Wa_Shetani -1-

UTANGULIZI:
KILA binadamu yupo duniani kwa ajili ya kuishi. Hakuna aliyeumbwa kupata mali kwa ajili ya kumpoteza mwenzake bali imeumbwa riziki ya mtu ipitie kwa mtu. Wengi wamesahau kila kiumbe kitaonja mauti siku yake ikifika lakini si kwa utashi au tamaa za watu bali kwa mapenzi ya Mungu. Wengi huamini wataishi milele na kuwageuza wenzao kama chambo au ngazi ya kufikia utajiri au mafanikio kwa vile uhai wao unanukia harufu ya fedha. Ili kujua kwa nini uhai wa watu wengine una harufu ya fedha ungana tena na yuleyule mwandishi wako mahiri katika riwaya nyingine ya kusisimua

Kilikuwa kiumbe cha ajabu ambacho japokuwa kilifanana na umbile la kibinadamu lakini kilikuwa na matendo ya kinyama. Wengi walifikiri ni mzimu lakini haukuwa mzimu, alikuwa binadamu tena albino ambaye alionekana kuishi maisha marefu kama mnyama wa porini huku akiwa hana kiungo kimoja cha mwili, mkono wa kulia.

Umbile lake lilikuwa lenye afya njema, akiwa na nywele nyingi nyeupe na ndefu kama rasta. Ndevu nyingi, kucha ndefu na mavazi yaliyochakaa yaliyoonesha kutojua maji kwa kipindi kirefu zaidi ya mvua iliyomnyeshea.

Chakula chake kilikuwa nyama mbichi na matunda ya msituni. Macho yake yaliyokuwa mekundu na muda mwingi aliangalia chini. Alionekana kuwachukia binadamu kuliko kitu chochote.
Siku ya kwanza kukutana naye, aliua watu zaidi ya watatu, ikabidi itumike nguvu kwa kumpiga risasi ya kupoteza fahamu ndipo walipoweza kumkamata.

Daktari aliyepelekwa kwa ajili ya kumchunguza alinyongwa kwa kamba alizokuwa amefungwa nazo. Japo alikuwa kiumbe wa kawaida lakini mazingira yalimfanya aonekane kama mnyama. Baada ya kumkata nywele na kucha, bado alionekana mtu mwenye hasira, asiyependa kutazama watu usoni.

Mkono mmoja uliokuwa umekatwa ulibaki na kovu la muda mrefu, lingekuwa bichi labda wangesema ni mmoja wa majeruhi wa kukatwa kiungo cha mkono katika janga lililolikumba taifa la kuuawa kwa kukatwa viungo walemavu wa ngozi, albino.
Lakini alionekana mtu aliyeishi maisha ya porini kwa kipindi kirefu japo haikufahamika ni muda gani alioishi porini.

Kingine kilichowashangaza watu ni hali ya kuwa kama mnyama asiyependa wanadamu zaidi ya wanyama. Tofauti yake nyingine, alikuwa na roho mbaya kuliko ya simba.
Hakupenda chakula kilichopikwa, alipenda vyakula vibichi kama nyama mbichi na matunda, hivyo ndivyo vilikuwa vyakula vyake vikuu.

Wataalamu wa kujua matatizo ya binadamu walikutana na kumchunguza kwa muda. Vipimo vyote vilionesha yupo katika hali ya kawaida. Umri wake ulionesha kuwa na miaka kati ya 35 na 40. Mmoja wa wataalamu aligundua kuwa mtu yule aliishi maisha ya porini kwa muda mrefu hali iliyosababisha awe na hulka kama mnyama.

Walikubaliana kumtengenezea mazingira ya kumrudisha katika hali ya ubinadamu. Pamoja na kuwa haongei lakini alionesha dalili za kusikia kwani alikuwa makini kusikiliza kila kilichokuwa kikizungumzwa.
Mtaalamu wa saikolojia ya binadamu aliwaeleza kuwa baada ya muda atarudi katika hali ya kawaida na kuamini mtu yule alikuwa na siri nzito ya kumfanya aishi maisha kama mnyama kwa muda mrefu porini na kuwa kiumbe mwenye hasira, asiyependa kutazama watu machoni.

Walimtengenezea mazingira ya upendo huku muda wote akiachwa peke yake akiwa amewekewa muziki wa taratibu wa vyombo vitupu. Mtaalamu aliwaambia kupitia muziki wa vyombo vitupu, taratibu ataanza kujengeka kifikra na kujiona ni binadamu. Pia walikuwa wakimwekea picha za sinema zenye kuonesha maisha ya upendo ya watu tofauti wakiwemo albino na watu wa kawaida.
***
Mtu yule aligunduliwa katika msitu mnene pembezoni mwa Mji wa Mangu na wataalamu wa masuala ya utengenezaji wa mvua ambao waliletwa nchini kukabiliana na ukame baada ya taifa kukumbwa na janga kubwa la ukame uliosababisha mabwawa ya maji katika vyanzo vya umeme kukauka, hali iliyosababisha mgao mkubwa wa umeme.

Marafiki wahisani wa nchi zilizoendelea, walijitolea kuleta wataalamu wake kwa ajili ya kutengeneza mvua kwa bei nafuu. Nchi ya Thailand, moja ya marafiki walikubali kusaidia wataalamu pamoja na mitambo ili kumaliza tatizo la ukame lililoikumba nchi yetu iliyokuwa katika hatari ya kuingia gizani baada ya mabwawa yote kuwa

kwenye hali mbaya kwa kina cha maji kuendelea kupungua kila kukicha.
Kikosi cha wataalamu kilizunguka sehemu yenye milima yenye miti mingi ambayo wangeweza kuitumia kutengeneza mvua. Msitu wa Nyashana uliokuwa pembezoni mwa Mji wa Mangu ulionekana kufaa kuzalishia mvua.
Baada ya kuuchagua msitu ule, kazi ilianza mara moja kwa kuanza kupima. Wakiwa wanapima kwa kutumia kiona mbali, waliweza kumuona mtu ambaye baada ya kumvuta karibu kwa mitambo ya kiona mbali, walihisi ni mzimu, wakashawishika kusogea karibu zaidi ili wamuone vizuri.

Walipomkaribia yule mtu ambaye wao walijua ni mzimu, alikimbia na kupotelea mapangoni. Walisitisha kazi ya kupima na kuanza kumtafuta yule mtu kutaka kujua mwisho wake na kwa nini yupo sehemu ile. Siku ya kwanza, mpaka giza linaingia hawakufanikiwa kumuona.
Wataalamu hawakukubali kumkosa, wakapanga kurudi siku ya pili alfajiri na kujificha. Walifanikiwa kumuona majira ya saa moja asubuhi akitoka kwenye pango lake, akawa anajinyoosha mwili.

Alipopiga miayo, meno yake yalionekana yamebadilika rangi na kuwa kama ya simba. Weupe wa meno yake ulipotea kabisa. Mzungu mmoja alijitokeza mbele yake, yule mtu alipomuona alishtuka na kutimua mbio kwa kukwea miti na mawe kwa mkono mmoja kama sokwe.
Kila mmoja alipigwa na butwaa na kujiuliza kwa nini mtu yule yuko vile, suala ya mzimu walilifuta japo alikuwa na nywele nyingi ndefu, kucha ndefu na nguo chakavu.

Wapo waliodhani ni msukule, baada ya kukimbia waliingia sehemu aliyotoka, ndani ya pango lililokuwa na giza nene. Kwa msaada wa tochi yenye mwanga mkali, walifika hadi ndani ya pango. Ndani ya pango hilo walikuta mifupa mingi ya wanyama, matunda yaliyoliwa nusu na nguo chakavu zilizokuwa kama godoro.
Hawakuishia hapo, walizunguka kila kona lakini hawakukuta kitu kingine zaidi ya vile vitu walivyoviona. Kutokana na kuonekana mtu yule ni vigumu kumkamata, walitengeneza mtego na kuondoka.

Itaendelea.......
..

0 comments:

Post a Comment