MIMBA YA JINI -42

Author

Hadithi ya kusisimua  #Mimba_ya_Jini -42-

#SOON NASHUSHA BONGE LA STORY ILI USIPITWE NA NEW STORY #LIKE_PAGE HII UWE WA KWANZA KUIPATA BONGE LA STORY  SHARE HADITHI HII TWENDE SAWA

ILIPOISHIA:
Kabla hajafika kwa mlinzi simu yake iliita alipoangalia ilikuwa inatoka kwa npenzi wake Shehna.
Aliipokea na kuzungumza.
"Haloo mpenzi." SASA ENDELEA...

"Haloo laaziz, vipi mpenzi wangu?"
"Safi tu."
"Mbona kama mnyonge?"
"Bwana huyu msichana ananichanganya sana."
"Kafanya nini?" Shehna alijifanya kuuliza.
"Hajafika mpaka saa hizi yaani ofisi chafu."
"Basi usikonde mpenzi wangu baada ya dakika mbili watakuja wasichana wangu kuja kufanya usafi uwape nafasi tu."
"Hakuna tabu."
Baada ya muda kidogo wasichana wawili warembo walibisha hodi kwenye geti, Mustafa alipowatazama alijua ndiyo waliotumwa na mpenzi wake Shehna.
"Asalaam aleykum," wale wasichana waliwasalimia kwa bashasha na sauti tamu.
"Waleykum salaam, nina imani ninyi ni wageni wangu?" Mustafa aliuliza.
"Swadakta, hatuna muda tuoneshe hiyo kazi."
Mustafa aliongozana nao hadi ofisini, baada ya kuwaonesha mmoja alisema:
"Haya tupishe tufanye usafi."
"Hakuna tatizo," Mustafa alijibu huku akitoka nje na kuwaacha wale wasichana.
Baada ya kutoka walipiga makofi, haikuchukua muda waliongezeka wengine ambao walifanya kazi ya usafi kwa muda mfupi. Baada ya usafi wenzao walitoweka na kuwaacha wale wawili. Nao walitoka hadi alipokuwa amekaa Mustafa getini na mlinzi walipokuwa wakizungumza tabia za Sara zilivyobadilika tofauti na zamani.
Walipofika walimweleza kwa sauti tamu yenye lafudhi ya kimwambao.
"Bwana sisi tunakukimbia tuna imani utafurahia usafi wetu."
"Nina waamini, nashukuru sana."
"Haya si tukukimbie."
"Haya, msalimieni sana Shehna."
"Salamu zimefika."
Wasichana wale walitoka nje ya geti na kutembea kufuata barabara, baada ya kuwa sehemu ambayo walijua Mustafa hawaoni walitoweka ghafla kurudi chini ya bahari.
Mustafa alirudi ofisini na kuikuta ofisi inapendeza kila kitu kilikuwa kimesafishwa ndani kulikuwa na hewa na harufu nzuri ya manukato. Alikaa kitini na kuanza kazi huku akiamini kama atamuoa Shehna basi ataishi maisha sawa na peponi.
***
Kila usiku Mustafa alifuatwa akiwa ndotoni na kujikuta yupo sehemu nzuri akiwa amelala pembeni ya Shehna aliyekuwa amelala huku tumbo lake likizidi kukua. Lakini alikuwa amevaa gauni jepesi lililoziba tumbo lake. Usiku sana Shehna alizima taa na kuondoa nguo zake na kumruhusu Mustafa alichezee tumbo lake lakini ikiwa gizani.
Siku zote Mustafa alifurahi kuwa karibu na mpenzi wake na kutamani siku zote awe karibu yake. Tumbo la Shehna halikuwa likimsisimua lakini hakupata nafasi ya kuliona, siku zote alimbembeleza kuliona Shehna alimwambia avute subira. Mustafa alikubaliana na mpenzi wake.
Katika siku alizolala alishangaa tumbo la Shehna kuwa kubwa akilala akiwa hana nguo tofauti na akimkuta amevaa nguo. Ile ilimfanya apange kumvizia wakati amelala ili awashe taa aone sababu ya tumbo lile kuwa kubwa tofauti na matumbo ya kawaida ya wanawake wenye mimba.
Wakati huo Sara aliendelea kuteseka na baridi na njaa hakutoka kwenye nyumba ile mbovu mpaka kiza kilipoingia, aliogopa kutoka muda ule kwa kuhofia kupigwa na kuumizwa. Kiza kilipoingia ndipo alipotoka na kurudi nyumbani, lakini alipofika sehemu ya chumba chake ambacho kilikuwa kimefungwa alisikia mtu akisema:
"Jamani yule mbwa wa asubuhi amerudi tena."
"Jamani huyu mbwa atakuwa ametumwa tu, tena amesimama kwenye chumba cha Sara."
"Jamani lazima kutakuwa na tatizo, Sara jana si alilala chumbani kwake ajabu asubuhi tukumuona na kukuta mlango upo wazi na mbwa huyu alitoka ndani. Ajabu tulimfukuza asubuhi usiku amerudi," shoga yake Happy alisema.
"Sasa na Sara atakuwa wapi?"
"Hapa ndipo tunachanganyikiwa maana hajaaga kama amepata dharura usiku."
Sara yote aliyasikia akiwa bado amesimama kwenye mlango wake, lakini alishindwa kuzungumza kwa kuhofia kubweka na kuwatisha kitu kitakachowafanya wamfukuze kwa kumpiga.

Itaendelea

NAKUELEWA SANA MTU WANGU WA NGUVU #SHARE HADITHI HIII UNIPE MOTISHA YAKUPOST STORY NYINGINE #LIKE_PAGE UWE WA KWANZA KUPATA #NEW_STORY

0 comments:

Post a Comment