MIMBA YA JINI -40

Author

Hadithi ya kusisimuwa: #Mimba_ya_Jini-40-

ONYESHA UPENDO SHARE STORY KUNIPA MOTISHA YA KUANZISHA STORY NYINGINE ILI USIPITWE NA STORY INAYOFUATA #LIKE_PAGE UWE WA KWANZA KUPATA STORY HYOOO...

ILIPOISHIA:
"Sara sitakusamehe ukichelewa kuchagua adhabu yako nitakugeuza kiumbe cha ajabu kisicho na mfano."
SASA ENDELEA...

Sara alijikuta kwenye wakati mgumu wa kuamua ageuzwe kiumbe gani, kabla hajapata jibu Shehna alipiga makofi wakatokea viumbe wawili wa ajabu wanaotisha sana tofauti na waliotangulia.
"Naam binti wa mfalme wa bahari ya dhahabu una shida gani?"
"Enyi watwana wenye roho chafu nataka mumtafutie adhabu yoyote kali huyu mwanadamu, mnataka nimpe adhabu gani?"
"Kwa nini tusimbanike kama mbuzi karibu na jua?" mmoja alipendekeza adhabu.
"Hapana adhabu hiyo kali sana, nataka ya kumtesa ili atambue siri aliyoitaka kuijua faida yake ni nini."
"Sisi hatuwezi kuchagua adhabu ndogo binti wa mfalme, tunaomba wewe uchague adhabu yoyote kwake tunajua amekuudhi sana. Adhabu yetu kwake ni kifo tena cha maumivu makali zaidi ya hapo hatuna adhabu nyingine."
"Basi mnaweza kunipisha nitoe adhabu yangu."
Baada ya kusema vile wale viumbe wa ajabu walitoweka na kubakia Shehna katika umbile la kawaida la mwanamke mrembo katika vazi pana kutokana na ujauzito wake na Sara ambaye alikuwa akitetemeka mpaka utumbo. Alimuangalia kwa muda Sara aliyekuwa amejikunyata kwa woga ubavuni mwa kitanda, kwa sauti ya upole alimwita.
"Sara."
"A...a...bee."
"Unaniweka kwenye wakati mgumu katika maisha yangu wa kukufanya kitu kibaya. Sikupenda kukufanyia chochote kibaya, narudia nimejitahidi kukuelekeza lakini umekuwa na masikio ya kenge mpaka utoke damu. Kwa vile umekataa kuchagua adhabu mimi nitakuchagulia adhabu. Nilifikiria nikugeuze nguruwe lakini hiyo kwangu ni adhabu kubwa, nimejifikiria kukugeuza funza wa kwenye kinyesi maisha yako nayo nimeona ni adhabu kubwa.
"Adhabu ndogo kuliko zote nimeonelea nikugeuze uwe mbwa ambaye atakuwa unazurura mitaani na kupigwa mawe lakini sitaruhusu wakuue. Chakula chako nitakijua mimi, utakula mara moja kwa siku. Nina imani utajua thamani ya kiburi chako."
"Nitakuwa mbwa mpaka lini?" Sara alijitahidi kuuliza.
"Mpaka nitakapojifungua."
"Shehna shoga yangu hakuna adhabu nyingine zaidi ya hiyo?"
"Sara mimi huwa sitoi adhabu bali umewaona watoa adhabu na adhabu zao, kama ningewaachia sijui ungekuwa kwenye hali gani?"
"Nipunguzie shoga yangu."
"Sara unanichelewesha muda wangu umekwisha."
Baada ya kusema vile alinyoosha kidole ghafla Sara aligeuka mbwa, kisha Shehna alipiga makofi na viumbe wa ajabu walitokea. Aliwaonesha ishara ya macho huku akipanda kwenye kiti chake. Walikibeba juu ghafla ardhi ilipasuka na wao kuzama ndani yake kisha alijifunga na kuwa kama mwanzo.
Sara alibakia juu ya kitanda huku akiamini yeye ni mtu wala siyo mbwa, lakini bado hakuamini kilichotokea ni kweli zaidi ya kuota ndotoni. Siku ya pili aliamka asubuhi kama kawaida na kutoka nje kwenda kuoga ili awahi kazini lakini watoto wa jirani walipiga kelele kumuona mbwa.
Kitendo kile kilimfanya Sara arudi ndani lakini alishangaa kusikia.
"Amekimbilia ndani kwa ma' mdogo Sara," alisema mtoto mmoja.
"Kwani Sara yupo wapi?" alimsikia jirani yake mama Saidi akiuliza.
"Sara...Sara," Happy alimwita kwa sauti.
Sara aliyekuwa chumbani kwake aliitika kwa sauti.
"Abee nimo ndani," lakini ilitoka sauti ya mbwa kufoka.
"Jamani mbwa huyu katokea wapi na Sara kaenda wapi asubuhi yote na kuacha mlango wazi," jirani mwingine alisikika akisema.
"Jamani tufanyeni msaada wa kumtoa huyo mbwa ndani," mtu mwingine alitoa wazo huku majirani wakizidi kukusanyika.
"Kweli labda kichaa anaweza kutuuma pia hata watoto wetu."
Jirani mmoja alishika fimbo na kuingia chumbani kwa Sara na kushtuka kumuona mbwa juu ya kitanda .

Itaendelea

KUWA WA KWANZA KUPATA STORY MPYA #LIKE_PAGE USIPITWE NA STORY INAYOFUATA.

0 comments:

Post a Comment