MIMBA YA JINI -38

Author

Hadithi ya kusisimuwa: #Mimba ya jini-38-

#LIKE_PAGE TWENDE SAWA STORY INAYOFUATA UWE WA KWANZA KUIPATA #SHARE KIPANDE HIKI UNIPE MOTISHA YAJUPOST MWENDELEZO

Ilipoishia
“Mmh! Shoga una haki ya kwenda muda huu kwa mzee Gogo.”
“Sasa tunafanyaje?”
“Nakusikiliza wewe.”
Sasa endelea...

“Basi kodi Bajaj nipitie nitalipa.”
“Nipe dakika ishirini nitakuwa hapo jiandae nikifika tunaondoka.”
“Wala sina shida ya kujiandaa utanikuta nje nakusubiri.”
Sara hakutaka kuoga alichukua pochi yenye pesa na kutoka kumsubiri shoga yake, baada ya muda Mwajuma alifika na Bajaj ambapo Sara aliingia na kuelekea Tandale kwa mzee Gogo. Kwa vile walipitia njia za nyuma walikwepa foleni na kufanikiwa kufika kwa mzee huyo mapema.
Walikuta watu bado hawajaondoka, walikaa kwenye benchi kusuburi muda wa kuingia ndani. Wakiwa wamekaa kwenye benchi alitoka mzee wa makamo kichwa chote kilikuwa kimejaa mvi aliyekuwa amevaa fulana ya mikanda chini alijifunga kaniki. Kwa vile alikuwa amezoeana na Mwaju alipomuona alishtuka na kumuuliza.
“Vipi tena mama, mbona usiku?”
“Shida tu mzee wangu.”
“Karibu hapa ndiyo kwa mzee Gogo asiyeshindwa na kitu.”
“Asante, vipi tutapata upendeleo?”
“Nipe dakika kumi nitakuiteni.”
Mzee Gogo alikwenda kwenye mti uliokuwa pale uani na kuchukua vitu kisha alirudi ndani kuendelea na kazi. Baada ya muda alitumwa mtu kwenda kuwaita, waliingia ndani na kukaa kwenye mkeka.
“Karibuni.”
“Asante.”
Mzee Gogo alitulia kwa muda akipanga vizuri dawa zake kisha alinyanyua macho na kusema:
“Mmh! Mabinti mna tatizo gani?”
“Shoga yangu ndiye mwenye tatizo.”
“Eti mama una tatizo gani?” alimgeukia Sara.
Sara alimueleza mikasa iliyomkuta na jinsi mganga aliyekwenda jioni ile kukataa kumtibu. Baada ya kumsikiliza alichukua kikopo kilichokuwa na unga mweupe ambapo alichota kidogo na kuumwaga mbele yake na kutulia kama anatazama kitu. Alitulia akikaza macho kwenye unga ule kisha alisema:
“Ni kweli kabisa ni jini.”
“Nani?”
“Huyu mpenzi wa bosi wako.”
“Mungu wangu una maanisha Shehna?”
“Ndiyo.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Wewe unataka tumfanyeje?”
“Tumpoteze kabisa.”
“Kumpoteza itakuwa vigumu kwa vile tayari amekuwa mpenzi wa bosi wako.”
“Na ndiye aliyenitesa vile?”
“Ndiyo.”
“Tumfanyeje ili kuvunja penzi na bosi wangu pia asinifuatefuate?”
“Kuvunja urafiki ni vigumu kwa vile tayari ana ujauzito wa bosi wako.”
“Sasa tutafanya nini?”
“Labda kumuua tu.”
“Sawa.”
Baada ya kusema vile alichukua chupa ndogo na bakuli dogo na kumimina maji yake kisha alizungumza maneno ambayo hawakuyaelewa. Ghafla mganga alinyamaza na kuanza kung’ata maneno mara mtetemeko mkubwa ulitokea ndani ya chumba cha uganga lakini nje hakuna aliyejua nini kinaendelea.
Wakiwa wameingiwa na wasiwasi walishtuka kumuona mganga akijishika mikono shingoni kama anamzuia mtu asimkabe na kuliacha bakuli likianguka chini na kumwaga maji.
Sara na shoga yake walishtuka kumuona mganga akihangaika kama anapigana na mtu aliyeonekana kumkaba shingoni ambaye hawakumuona. Mara walimuona akianguka kama mzigo huku mikono yake ikiwa bado shingoni na kuanza kurusha miguu na kufanya dawa zilizokuwa pembeni yake kutawanyika ovyo.
Walinyanyuka walipokuwa wamekaa kwa woga, mganga aliendelea kurusha miguu kama kuku aliyekatwa kichwa kisha alitulia. Baada ya kutulia waliogopa kumsogelea na kutoka nje kumwita msaidizi wake. Aliingia na kwenda alipokuwa amelala mzee Gogo. Walimkuta macho na ulimi vimemtoka nje akiwa amekufa.
Sara na shoga yake waliona msala utawageukia walitoka taratibu bila kuaga na kurudi nyumbani. Njia nzima Sara alijiuliza maswali na kukumbuka maneno ya mganga wa Vingunguti aliyemweleza kuwa mganga yeyote atakayetaka kuingilia kesi ile lazima moto umuwakie. Alipofika kwake aliteremka na kumuacha shoga yake akirudi nyumbani kwake Kigogo.

Itaendelea
SHARE STORY TWENDE SAWA NIPE MOTISHA YAKUPOST KIPANDE KINGNE

0 comments:

Post a Comment