Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Manyara,
imemhusisha Mbunge wa Babati Mjini, Kisyeri Chambiri (pichani), na
tuhuma za kutoa hongo katika kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Takukuru inadai kuwa mbunge huyio alinusurika kukamatwa juzi usiku akiwa na wapambe wake waliokuwa wanagawa rushwa.
Kamanda wa Takukuru mkoani Manyara, Mogasa Mogasa, alisema Chambiri
akiwa na wezake watatu ambao wanashikiliwa na taasisi hiyo, alinusurika
kwa kutimua mbio usiku majira ya saa nne na kuacha kitita chaSh. 500,
000 alizokuwa nazo katika kijiji cha Kiongozi akitaka kuzigawa kwa
baadhi ya watu wake.
Pia taarifa ya kamanda huyo ilieleza kuwa Chambiri alifanikiwa
kukimbia akiwa na viongozi kadhaa wa kijiji hicho ambao kamanda huyo
hakuta kuwataja majina, akisema kuwa wanaendelea kutafutwa na kumtaka
Chambiri ajisalimishe.
Kamanda huyo aliwataja waliyokamatwa kuwa ni Samuel John Barani
ambaye ni Katibu wa Uchumi na Fedha CCM wilaya; Thomas Cosmas Darabe na
Ally Ayubu Ramadhani, ambao walikuwa na mgombea huyo katika harakati
hizo.
Kamanda Mogasa paliongeza kuwa baada ya watuhumiwa hao kukutwa
katika eneo hilo na Chambiri kutokomea, walifanikiwa pia kukamata
makaratasi yenye majina ya watu waliokuwa wameandaliwa kwa ajili ya
mgawo huo.
Hata hivyo, alisema wanaendelea na mahojiano watuhumiwa hao na
kwamba baada ya taratibu kukamilika watafikishwa mahakamani na kuongeza
kuwa wanalishikilia gari la mbunge huyo.
Chambiri alipoulizwa, alikana kuhusika na kudai kuwa ni mbinu zinazotumiwa na baadhi ya watu wasiyomtakia mema.
Aidha, alidai kuwa yeye kama mgombea na mtetezi wa jimbo hilo,
amekuwa akipata taarifa mara kwa mara za kupangiwa njama kama hizo ili
kudhoofisha juhuddi zake za kurejea madarakani.
“Hivi walishindwaje kunikamata wakati wanadai walitukuta tukiwa
ndani kama siyo uzushi, mimi nafahamu kuna watu wamewekwa kunichunga
hata kama naenda nyumbani kisa tu mimi nisichanguliwe, na hiyo ni baada
ya kuona watu wameonyesha upendo kwangu,” alisema Chambiri.






0 comments:
Post a Comment