CHADEMA HAKIJAELEWEKA KUHUSU URAIS

Author
Wakati leo saa 10 jioni ndiyo muda wa mwisho uliopangwa kurejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais ndani ya Chadema, hadi sasa hakuna mwanachama hata mmoja aliyejitokeza kuzichukua.

Badala yake zimetolewa kauli tofauti kuhusu kusuasua kwa mchakato wa kumpata mgombea urais hadi chama hicho kulazimika kusogeza mbele tarehe ya mwisho ya kuchukua na kurejesha fomu.

Hali hiyo inazidisha sintofahamu iliyougubika mchakato wa urais ndani ya chama hicho na ndani ya Ukawa, kuwa huenda kuna ‘mtu wa nne’ anayesubiriwa kutoka nje ya chama hicho, kama ilivyoripotiwa na gazeti hili, wiki iliyopita.

Likikariri chanzo cha kuaminika ndani ya Ukawa, gazeti liliandika kuwa huenda umoja huo na hasa Chadema, wanasubiri mgombea kutoka nje ya chama kwa kuwa hata baada ya wajumbe wa vikao vya mashauriano kukubaliana kuwa mgombea wa Ukawa awe Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, baadhi ya wajumbe kutoka katika chama hicho wanadaiwa kukataa kutangazwa kwake.

Hata baadaye walipoulizwa nini msimamo wao kuhusu tetesi za mpango wa kumkaribisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutoka CCM, viongozi na wabunge wa chama hicho walisema anakaribishwa mradi tu afuate kanuni na taratibu.

Suala la mgombea urais wa Chadema na Ukawa limeendelea kuteka mjadala wa kisiasa nchini huku Watanzania wakisubiri kufahamu nani atateuliwa kupambana na yule wa CCM, Dk John Magufuli, hali inayosababisha baadhi ya watu kudai mchakato huo una mizengwe.

Hata hivyo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha mkoani Iringa, Gaudence Mpangala alisema anadhani hakuna mizengwe inayowazuia baadhi ya wanachama wasiwanie nafasi hiyo kwa kuwa kanuni na taratibu za vyama ziko wazi. Alisema anachokiona ni kwamba wanachama hawajajipanga kuwania nafasi hiyo ya juu.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo alisema wako watu ambao hawawezi kugombea nafasi ya urais kuwakilisha vyama vyao kwa sababu wanawaogopa viongozi wa juu wa vyama hivyo.

“Jambo la msingi la kuangalia ni haki kutendeka katika kila mchakato katika uteuzi lakini watu wanawania nafasi kulingana na walivyojipanga,” alisema.

Alisema wingi wa wagombea urais katika vyama si kigezo pekee cha kukua kwa demokrasia bali mchakato wa kuwapata wagombea hao ukiendeshwa kwa haki ndiyo demokrasia.

Alisema kuwa hakuna ubaya hata kama kuna mgombea mmoja anayewania urais bali kinachotakiwa kuangaliwa ni ubora wa mchakato.

Hakijaeleweka

Katika mkutano wake uliofanyika mjini Mwanza Jumatano ambao ulipangwa kutumika kumtangaza mgombea urais wa chama hicho, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe aliwaomba Watanzania wavumilie wakati wanakamilisha taratibu za kumpata mgombea huyo.

Pia, ilielezwa kuwa chama hicho kilikuwa kinasubiri mkutano wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF unaofanyika leo, huku taarifa nyingine zikisema chama hicho kilikuwa hakijampata mgombea mwenza kutoka Zanzibar.

Wakati hayo yakiendelea, bado ratiba ya kuchukua fomu za urais na kurudisha ilikuwa inaonyesha ni leo na hakukuwa na dalili zinazoonyesha watu kujitokeza kuwania nafasi hiyo ya juu, ambayo mara kadhaa viongozi wa chama hicho wametamka kuwa tayari wamempata mgombea anayefahamika ndani na nje ya nchi.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Slaa aliliambia Mwananchi jana kuwa asingeweza kusema lolote kuhusiana na suala hilo kwa sababu alikuwa nje ya ofisi.
“Wasiliana na watu walioko ofisini, wao wataweza kujibu vizuri swali lako,” alisema Dk Slaa.

Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Dk Slaa aligombea urais na kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.

Gazeti hili lilipotaka kufahamu iwapo safari hii Dk Slaa amechukua fomu, alikataa kusema lolote akidai taarifa hizo zitapatikana kwa walioko ofisini.

Wabadili ratiba

Akizungumzia hali hiyo jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema kuna marekebisho yamefanyika katika tarehe hiyo ya mwisho kurejesha fomu ambayo yatatangazwa ndani ya simu mbili au tatu ambayo yalilenga kupisha mchakato wa kura za maoni.

“Unajua viongozi wanatakiwa kusimamia kura za maoni majimboni, kwa hiyo tuliona kwanza tumalize hili, suala la mgombea urais lisubiri kwanza. Tunatarajia kutangaza tarehe mpya ya kurejesha fomu ndani ya siku mbili,” alisema Mwalimu na kuthibitisha kuwa hadi wanasimamisha shughuli hiyo hakukuwa na mwanachama yeyote aliyechukua fomu za kuomba kuteuliwa kugombea urais.

Baadaye jioni jana, chama hicho kilitoa taarifa ya kusogeza mbele tarehe ya kurudisha fomu hadi Julai 31, 2015 saa 10 jioni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watiania wote watapaswa kurejesha fomu hizo katika Ofisi ya Katibu Mkuu, Makao Makuu ya Chadema, Kinondoni, Dar es Salaam.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa ratiba ya awali iliathiriwa na kitendo cha kusogeza mbele tarehe za uchukuaji na urejeshaji wa fomu za ubunge baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza majimbo mapya 26.

“Hatua hiyo iliathiri ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania uteuzi wa kugombea urais kupitia Chadema ambapo awali wanachama wenye sifa walipaswa kuanza kuchukua fomu 20-25 Julai, mwaka huu,” ilisema taarifa hiyo.

Mkutano Mbeya waahirishwa

Katika hatua nyingine, ziara ya Dk Slaa aliyetarajiwa kuwasili na kuhutubia mkutano jijini Mbeya leo imefutwa hadi itakapotangazwa tena.

Mratibu wa chama hicho Kanda ya Nyasa (Chadema), Frank Mwaisumbe alisema sababu ya kufutwa ni viongozi wa kitaifa kuendelea na vikao vya ngazi ya juu jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Chadema mkoani hapa, Joseph China alisema ziara hiyo imefutwa kutokana na viongozi wakuu wa kitaifa kutingwa na vikao vya Ukawa.

Viongozi wa kitaifa wa Chadema wakiwa Mwanza walitangaza kwamba wangefanya mikutano mingine, Mbeya, Arusha na Dar es Salaam.

0 comments:

Post a Comment