Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Waziri aliyejiuzulu kutokana
na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta
Escrow, Profesa Sospeter Muhongo, jana aliumbuka baada ya Chama chake
kukataa kupokea lundo la makasha ya CD (santuri) zenye picha za
wadhamini wake 675.
Badala yake, alielezwa kwamba, hakuna kipengele kinachoruhusu kuwa na kumbukumbu hiyo.
Profesa Muhongo, alirejesha fomu yake ya kuomba kuteuliwa na chama
hicho kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, saa 9:57 asubuhi
na kumkabidhi Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na
Oganaizesheni, Mohamed Seif Khatibu kwenye makao makuu ya chama hicho
mjini Dodoma.
Baada ya kukabidhi fomu za wadhamini wake katika mikoa 15
aliyopita, Profesa Muhongo alitoa pia makasha 15 yenye CD za picha
ambazo alidai amefanya hivyo ili kuonyesha hajapita njia ya mkato akidai
anaamini mtu sahihi atakayeweza kuwavusha watanzania kwa sasa, ni yeye
na si mgombea mwingine kati ya makada wote waliojitokeza kutaka kumrithi
Rais Jakaya Kikwete.
Alipomaliza kuzungumza na kisha kukabidhi CD hizo, Khatibu
alisema:”Bahati mbaya katika Daftari la kurejesha fomu za CCM za
kugombea kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015
hakuna mahala panapoonyesha kwamba utapaswa kukabidhi CD
ulizonipa…wanaangua (vicheko).”
Baada ya kuelezwa hivyo, aliondoka na kuziacha CD hizo kwa Khatibu.
Profesa Muhongo alijiuzulu uwaziri wa Nishati na Madini, baada ya
kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka
akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na
baadaye kutangaza nia ya kugombea urais.
MULENDA AREJESHA FOMU
Kwa upande wake, Leonce Mulenda ambaye naye alirejesha fomu yake ya
kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais, aliiga mfumo uliotumiwa na
watangulizi wake, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Waziri wa Mambo
ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, kugoma kuzungumzia safari yake ya
kusaka wadhamini mikoani na kurejesha fomu kimya kimya.
Mulenda alirejesha fomu hiyo saa 5:35 asubuhi na kumkabidhi Khatibu
na kumweleza kwamba amepata wadhamini katika mikoa 15 ikiwamo mitatu ya
Zanzibar na baadaye kuagana na kuondoka huku akikwepa kuzungumzia
safari yake.
LOWASSA AZOA WADHAMINI 42,405 MANYARA
Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Kiseryi Chambiri, amesema anamuomba
Mungu jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa liwe ni miongoni
mwa majina matatu ya wagombea urais yatakayofika katika Mkutano Mkuu wa
CCM kwani litakapoonekana watakuwa wamemaliza kazi na uchaguzi.
Kauli hiyo aliitoa jana katika uwanja wa Old Majengo wilayani
Babati wakati wa kukabidhi wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini
Lowassa katika mbio zake za kusaka urais kwa tiketi ya chama hicho.
Katika Mkoa huo alipata jumla ya wadhamini 42,405.
Chambiri alisema safari ya Lowassa ni ndefu lakini karibu wanafika
mwisho na anachoomba katika majina matatu yatakayofika katika himaya
yao kama wajumbe wa Mkutano huo jina lake liwemo kusudi waweze kufanya
kazi.
“Kwa sababu kwa mujibu wa taratibu za CCM majina yale matatu
huletwa ili yaweze kupigiwa kura, kama jina lako halipo hatuwezi kufanya
kazi na mimi nakuombea kwa mungu basi katika yale majina matatu
yatakayoletwa kwaajili ya kupigiwa kura na lako liwepo,” alisema
Chambiri.
Alisema endapo jina hilo litakuwapo watakuwa wamemaliza kazi na uchaguzi utakuwa umemalizika.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Onesmo Nangole, alisema
matumaini yaliyopo ni makubwa kwani Lowassa ni mtu mkarimu na mpole na
chakula chake huliwa na masikini na mtu mwenye nywele nyeupe anautukufu.
Akizungumza na wanachama na wananchi, Lowassa aliwashukuru kwa
kujitokeza kumdhamini na kusema imani huzaa imani na kwamba atahakikisha
akipata nafasi hiyo atawatumikia.
“Nawashukuru kwa wale walionidhamini najua CCM wanahitaji wachache
lakini nimedhaminiwa na wengi, nitaenda kuyahifadhi nyumbani kwangu
kama kumbukumbu na historia ya maisha yangu nasema nashukuru sana,”
alisema Lowassa.
Aidha alisema wakimchagua wahakikishe wanapenda kuchapa kazi maana
anataka kuendesha nchi mchakachaka ili kuondokana na umasikini.
Aliwawakumbusha kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha
katika daftari la kupigia kura kwani ni haki yao ya msingi na kikatiba.
“Natamani niongee mengi lakini kanuni haziruhusi ibaki kusema
naomba muendelee kuniombea katika hili na nina wapenda sana,” alisema
Lowassa.
Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Babati, Daniel Ole Porokwa, alisema
wanachama wa CCM 42,405 wamejitokeza kumdhamini Lowassa katika mkoa huo
tofauti na wengine waliodai hatapata wadhamini wengi Manyara.
“Waliokudhamini wote wamejitolea na ndiyo maana wapo hapa, haya ni
mapenzi tu ya wananchi na naamini wewe ndio utakayekuwa Rais wa
Tanzania…Hakatwi mtu hapa,”alisema.
Alisema katika wilaya ya Mbulu wamemdhamini 9,500, Babati Mjini
12,500, Babati Vijijini 6,000, Hanang' 5,700, Kiteto 5,550 na Simanjiro
10,300.
NYALANDU: TISIGOMBANE
Mgombea mwingine wa urais, Lazaro Nyalandu, amewataka wanachama wa
CCM wasigombanishwe na uwingi wa wagombea wanaowania kuteuliwa.
Akizungumzia mjini Songea, mkoani Ruvuma, baada ya kupata
udhamini, Nyalandu alisema kuwapo kwa idadi kubwa ya wagombea kisiwe
chanzo cha mpasuko ndani ya chama bali iwe chachu ya kukiimarisha.
Alisema mwisho wa mchakato huo watia nia wote watapaswa kusimama
juu ya yaliyofanywa na yatakayopangwa kufanywa na CCM na kuwa hakuna
sababu ya kuwapo kwa mgawanyiko miongoni mwao.
Alihadharisha kuwa ikiwa kutatokea mgawanyiko ndani ya chama au
watia nia hao na wanachama itakuwa sawa na familia isiyo na shukrani
ambayo haitakaa isimame katika mafanikio.
MAKAMBA AMWAGA CHOZI
Kada wa CCM, January Makamba amejikuta katika wakati mgumu na
kumwaga machozi jukwaani alipokuwa akielezea historia ya maisha yake na
jinsi walivyoishi na bibi yake mzaa mama katika kijiji cha Kyaka,
wilaya ya Misenyi mkoani Kagera.
Makamba alipanda jukwaani juzi jioni kwa lengo la kuwashuruku wana
CCM kwa kumdhamini,lakini kabla ya hajaanza kufanya hivyo alianza
kuelezea maisha yake binafsi na bibi yake wakati huo wakiishi kijijini
mwishoni mwa miaka ya 70.
Wakati Makamba akielezea maisha yake yalivyokuwa wakati akiishi na
bibi yake, alijikuta sauti ikikwama na kulengwa lengwa na machozi jambo
lililomfanya akatishe hotuba na kushuka jukwaani.
Kada huyo ambaye alikuwa mkoani Kagera kusaka wadhamini, baada ya
kushuka jukwaani kwa kushindwa kuzungumza alikwenda kwenye kiti
alipokuwa amekaa na kukaa kwa muda kabla ya kurudi jukwaani tena
kuendelea kutoa shukrani kwa wanachama.
Hata hivyo, baada ya kurudi jukwaani hakutaka tena kuelezea maisha
yake na bibi yake walivyokuwa wakiishi, badala yake alianza kuzungumzia
changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kijiji cha Kyaka pamoja
na mkoa mzima wa Kagera.
Kabla ya kumwaga machozi jukwaani, Makamba aliwaambia wananchi hao
kwamba alikaa na bibi yake akiwa anamfundisha kulima, kusalimia watu
wakubwa pamoja na kuchunga mbuzi.
Aliwaambia wananchi hao kwamba anayajua maisha ya kijijini kwa
kuwa ameishi huko, hivyo anadhamiria kupambana na ugumu wake ikiwa
atapata ridhaa ya CCM kugombea urais kisha kuwa kiongozi wa nchi.
“Nimeishi huku na bibi yangu, najua maisha halisi ya huku na ndiyo
maana nasema nataka kuleta majawabu ya changamoto zinazowakabili nyinyi
wananchi,” alisema.
Makamba ambaye aliwasili kijijini hapo akitokea Bukoba mjini,
alipata mapokezi makubwa ya Pikipiki na magari binafsi ambayo yaliongoza
msafara wake hadi ofisi za CCM wilaya ya Misenyi na kupata wadhamini.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho cha Kyaka walisikika wakiimba
nyimbo za Kihaya maalum kwa ajili ya kumkabirisha huku wakisema Makamba
amerudi nyumbani.
Baada ya kupata wadhamini, Makamba alipita katika shule ya msingi
ya Kyaka ambayo alisoma kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu ambako
alikutana na mwalimu wake aliyemfundisha darasa la kwanza na kisha
alielekea nyumbani kwa bibi yake.
MWINGINE ACHUKUA FOMU
Hellena Elinewinga, Mtaalam wa masuala ya utafiti, amekuwa kada wa
40 wa CCM kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho, kugombea
urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia hatua hiyo baada ya kuchukua fomu hiyo jana, Hellena
alisema ameamua kujitosa katika kinuanganyiro hicho, kwa kuwa
anachukizwa na baadhi ya aina ya viongozi wanaoshindwa kutoa huduma
stahiki kwa watanzania na kujinufaisha wenyewe.
Hellena alikabidhiwa fomu hiyo jana, na Khatibu, saa 7:20 mchana
huku akisisitiza kwamba kama chama chake kitamteua kugombea kiti hicho,
atahakikisha viongozi wanaokwamisha mchakato wa maendeleo au kulihujumu
taifa, wanahukumiwa adhabu ya kifo kutokana na mchango mbovu walioutoa.
Mgombea huyo anayefanya kazi na Asasi za Kiraia na Taasisi za
Kilimo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini; ni mkazi wa Tarafa ya Masama,
Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.
Hellena (40), sasa anakuwa mwanamke wa sita kujitosa kuomba ridhaa
ya chama chake. Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha- Rose
Migiro; Naibu Waziri wa zamani wa Fedha na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Monica Mbega; Balozi Amina Salum Ali; Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti
wa Magonjwa ya Binadamu, Dk. Mwele Malecela na Ofisa Maendeleo ya Jamii,
Ritha Ngowi.
0 comments:
Post a Comment