Makada mbalimbali wa Chadema jana walirudisha fomu za kuwania kuteuliwa na chama hicho katika nafasi ya ubunge katika majimbo ambayo yanashikiliwa na CCM.
Mchakamchaka huo wa kurudisha fomu hizo ulifanyika katika maeneo mbalimbali nchini jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho.
Katika Jimbo la Monduli linaloshikiliwa na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa tayari makada watatu wamerudisha fomu.
Waliorudisha fomu ni Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya hiyo Josephat
Sironga, Mwenyekiti Baraza la Wanawake (Bawacha) Mkoa wa Arusha, Cecilia
Ndosi na Katibu Mwenezi wa chama hicho Monduli, Patrick Ngala ole
Mong’i.
Akizungumza jana Mong’i alisema: “Tumechukua fomu sisi watatu na tumerejesha ili kupisha vikao vya maamuzi.”
Mkoani Mbeya makada lukuki wa Chadema mkoani humo
walimiminika kurudisha fomu katika muda uliotakiwa huku wengine wengi
wakitajwa kucheleweshwa na kazi ya kuweka fedha benki.
Katika Jimbo la Mbarali linaloshikiliwa na
Modestus Kilufi (CCM), makada saba walirudisha fomu hadi saa 10.00 jioni
muda ambao ulikuwa wa mwisho.
Katibu wa chama hicho wilayani hapo, Nicolaus
Lyaumi aliwataja waliorudisha fomu kuwa ni Jidawaya Kazamoyo, Grace
Mboka, Dick Baragasi, Tazan Ndingo, Liberatus Mwang’ombe, Rajab Kilemile
na Machami Kasambala.
Katika Jimbo la Mbozi Mashariki, linaloshikiliwa
na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi, wanachama
27 wa Chadema walichukua fomu, lakini hadi saa 10.00 jioni, Katibu wa
chama hicho, Michael Mwamlima aliwataja waliorudisha kuwa ni Happness
Kwilabya, Abraham Msyete, Anastazia Nzowa, Abdul Nindi, Gerald Silwimba,
Eliud Msongole, Zablon Nzunda na Eliud Kibona.
Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Wilaya ya Vijijini,
Jackson Mwasenga alisema jimbo la wilaya hiyo ambalo linashikiliwa na
Mchungaji Luckson Mwanjale (CCM), waliorudisha fomu ni Daud Mponzi,
Edson Jisandu, Adam Zela, Anthony Mwaselela Hadson Sheyo, Benson
Mwamengo, Stephano Mwandiga, Frank Mwaisumbe Christina Kalisoto, William
Msokwa, Elias Songela na Jeremiah Mwaweza.
Katika jimbo la Kwela linaloshikiliwa na Ignas
Malocha (CCM), Daniel Ngogo pekee amerudisha fomu jana huku akitaja
vipaumbele vinne ambavyo ni elimu, afya, kuboresha miundombinu ya
barabara na ajira jimboni kupitia kilimo.
Pia katika jimbo la Sumbawanga Mjini
linaloshikiliwa na Aeshi Hilal(CCM) tayari mfanyabiashara wa mjini
Sumbawanga, Casiano Kaegele, maarufu kwa jina la Upendo alirudisha fomu
ya kuomba kuteuliwa na Chadema kuwania jimbo hilo.
Kaegele alisema amesukumwa na mambo kadhaa
kugombea ubunge katika hilo ikiwamo kuanzisha miradi ya wajasiriamali,
kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana na wanawake, sambamba na
miundombinu hususan uwanja cha ndege.
Katika jimbo la Morogoro Mjini linaloshikiliwa na Mohammed
Abood, makada wa 11 walijitokeza kuomba kuteuliwa baadhi yao ni Marcussy
Albaine, James Pawa Mabula, Batromeo Tarimo, Esther Tawete, Steven
Daza, Doris Kweka, Gerard Temba, Robert Mruge.
Katika jimbo la Kibaha Mjini linaloshikiliwa na Sylivestry Koka (CCM) wanachama sita kati ya saba waliochukua fomu waliorudisha.
Katibu wa Chadema Kibaha Mjini, Michael Nkobi
aliwataja waliorudisha kuwa ni Michael Mtally, Joachim Mahenga, Frank
Mzoo, Henry Msukwa, Bosco Mfundo na Isihaka Omari.
Katibu wa Chadema Kanda ya Pwani, Khalfan Mirambo
alisema Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, waliorudisha fomu za Ubunge
jumla yao ni 60 na kati ya hao, 56 ni viti maalumu. Hata hivyo alisema
bado majimbo matatu ya Mkuranga, Rufiji na Chalinze.
0 comments:
Post a Comment