Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe jana alitaja
sababu tano za kujiunga na chama cha ACT-Tanzania huku akijigamba kuwa
yeye ni mchapakazi asiyeyumbishwa.
Akinukuu maneno ya Rais wa zamani wa Ghana, Hayati
Kwame Nkrumah aliyewahi kusema, ‘forward forever, backward never’,
Zitto alisema huu ni wakati wa kuangalia mbele badala ya kurudi nyuma.
“Mimi ni mchapakazi, siangalii nyuma tena,
naangalia mbele. Mapambano yanaanza matokeo mtayaona baada ya Uchaguzi
Mkuu wa Oktoba,”alisema Zitto.
Ikiwa ni siku moja tu baada ya kukabidhiwa kadi ya
ACT, Zitto ambaye aling’atuka kutoka kwenye nafasi ya Ubunge Ijumaa
iliyopita, aliweka wazi kuwa alijiunga na ACT Machi 20 na kukabidhiwa
kadi katika Tawi la Tegeta, Dar es Salaam.
“Hii ilikuwa siku muhimu katika maisha yangu ya
kisiasa,” alisema Zitto na kuongeza kuwa amelipa ada ya uanachama hadi
mwaka 2025.
Kauli hiyo ilithibitishwa na Mwenyekiti wa ACT,
Lugano Mwaikenda ambaye alisema Zitto alijiunga na chama hicho na kupewa
kadi namba 7184.
Zitto ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alizisifu sera za chama hicho.
“Nimejiunga na ACT kwa sababu huku ndiko kunaendana na kile ambacho mimi
nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa ya kuweka masilahi ya
Taifa mbele,” alisema Zitto.
Alisema sababu nyingine ni kutokana na ACT kuwa
chama pekee nchini kinachokubaliana na itikadi ya ujamaa na kinaamini
katika falsafa ya Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema misingi mikuu ya chama hicho ni pamoja na uwajibikaji na uwazi aliyosema ni muhimu kwa mustakabali wa nchi.
“Hakuna namna nchi yetu inaweza kupiga hatua ya
kimaendeleo bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia
umakini na weledi,” alisema Zitto.
Wanachama wengine 13 wapokewa
Ujio wa Zitto ndani ya ATC ni kama umefungua njia
kwa watu wengine kujiunga na chama hicho. Jana wanachama wengine 13
walijiunga akiwamo mwanamuziki wa kizazi kipya, Selemani Msindi maarufu
kama Afande Sele.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alisema: “Tunaamini
kutokana na nia thabiti ya chama hiki chenye misingi ya kutaka kuleta
maendeleo kwa nchi, ndiyo umekuwa chachu ya wanachama kujiunga nasi,”
alisema Mwigamba.
Mmoja wa wanachama hao wapya, Dickson Ng’ili
alisema mbali na kuvutiwa na itikadi za chama chake kipya,
hakufurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Chadema dhidi ya Zitto.
Msanii Msindi ambaye alikuwa mwanachama wa
Chadema, aliunga mkono kauli ya Ng’ili akisema kuwa Chadema hawakufanya
uamuzi wa busara wa kumfukuza Zitto.
Wanachama wengine wapya ni pamoja na Askofu Gerald
Mpango, aliyekuwa, Jaji mstaafu Musa Kwikima na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Chadema Mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk.
Wengine ni Jorum Mbogo, Meck Mzirai, Charles
Lubala na Albert Msando ambaye alikuwa wakili wa Zitto katika kesi yake
dhidi ya Chadema.
0 comments:
Post a Comment